Na TAWANI SALUM, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Abdallah Maruma hivi karibuni alipokea ugeni wa wadaawa wa mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 ambao ulifanikiwa kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi.
Akizungumza tarehe 23 Julai, 2024 kwenye Ofisi ya Kituo hicho, iliyopo kwenye jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam, Mhe. Maruma alisema bado suala la usuluhishi lina nafasi ya kuchukuliwa uzito unaostahili na hii ni kutokana na kuendelea kuwepo kwa migogoro isiyo na ufumbuzi kwa muda mrefu.
"Si jambo lililozoeleka kwa wadaawa kurudi mahakamani kutoa mrejesho kama ilivyofanyika kwa shauri hili, nawashukuru wadaawa waliokuwa na mgogoro na pia nawashauri wadau mbalimbali pamoja na wananchi kutumia Kituo hiki kwani husaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya upatanishi (Mediation) na hivyo kusaidia kupunguza muda mrefu ambao ungetumika kwa njia ya kawaida ya uendeshwaji wa mashauri ndani ya Mahakama," alisema Mhe. Maruma.
Alitolea mfano wa mgogoro huo wa ardhi wa muda mrefu kati ya Wastaafu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) katika eneo la Kitalu ‘B’ Tabata Liwiti jijini Dar es Salaam pamoja na Kanisa la Moravian lililopo Tabata Jijini Dar es Salaam.
“Mgogoro huu umechukua takribani miaka 20 sasa, lakini ndani ya vikao sita kwa kupitia njia ya majadiliano katika Kituo hiki cha Usuluhishi imewezakana kutatua mgogoro huu kwa amani na utulivu,” alisema Jaji Maruma.
Akizungumza na wahusika hao Jaji Mfawidhi huyo alisema, kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya majadiliano na maridhiano (mediation) kunatoa fursa wa watu kutoa machungu na hasira zao na hatimaye kukubali kutatua mgogoro wao.
“Kiukweli tumefurahi sana kupata mrejesho kama huu hii inamaanisha kwamba hawa wahusika wapo tayari kuwaelezea wenzao faida za kutatua mgogoro bila ya kutumia ile njia ndefu ya Mahakama, kutumia fursa hii ya majadiliano inamaliza kila kitu hata vile tulivyoviona haviwezekani kwa kutumia usuluhishi vimewezekana,” alieleza Jaji Mfawidhi.
Kuhusu mgogoro huo, Mhe. Maruma alisema kuwa, ulikuwa ni wa kutokuelewana na kukubaliana, huku akieleza kwamba, mara nyingi kila upande unakuwa na taarifa ambazo sio sahihi na pia unakuwa na msimamo au kitu ambacho unakiamini na wakati mwingine sio sahihi.
“Vilevile kwenye huu mgogoro kila upande ulikubali kupoteza kidogo na kupata kidogo, sio rahisi kumwambia mtu aondoke kwenye ardhi ambayo anaamini anamiliki kihalali na pia kumwambia mtu kumlipa mwenzie fedha kwa ardhi ambayo anaamini kuwa alipewa kwa utaratibu, kwa hiyo ni vitu ambavyo mmeridhiana wenyewe, kupatikana kwa fursa hii ya kukaa pamoja na kujadiliana kumesaidia sana kutatua mgogoro huu,” alieleza Jaji Mfawidhi huyo.
Aliongeza kwamba, anaamini wote waliohusika katika mgogoro huo watakuwa ni Mabalozi wazuri wa kuelezea faida za usuluhishi na kuwahamasisha wenzao katika jamii kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro.
Alisema, pamoja na shukrani alizopata kutoka kwa pande hizo mbili, yeye hakufanya maajabu yoyote bali ni wadaawa wenyewe walikuwa na utayari, na hivyo kazi yake ilikuwa ni kuwasukuma wazungumze na kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro huo baada ya kuona uhalisia wa jambo lenyewe.
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando alimshukuru Jaji Maruma kwa kufanya kazi kubwa ya kutatua mgogoro huo kwa njia ya usuluhishi na kusema kuwa umeokoa muda mwingi ambao ungepotezwa kwa njia ya kawaida ya Kimahakama.
Mhe. Mmbando aliwapongeza pia wahusika wa mgogoro huo kwa kuleta mrejesho na shukrani kwa Kituo hicho cha Usuluhishi na kuwaomba kuwa mabalozi wa kukisemea vizuri Kituo hicho kwakuwa kinasaidia kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na hivyo, kuokoa muda ambao ungepotezwa kwa kutumia njia ya kawaida ya kimahakama.
Naye, Wakili aliyeliwakilisha Kanisa la Moravian lilipo Tabata jijini Dar es Salaam, Bw. Barnaba Luguwa alisema kuwa, wamefanikiwa kufuatia hekima ya uongozi wa Kituo hicho.
“Tumefanikiwa kufika mahali hapa, tukasema hii ndio haki na tukakubaliana na kusaini muafaka na baadae wakalipana fedha, hivyo tuliona ni jambo la busara kuleta mrejesho kuwa, sasa mgogoro umeisha hakuna tena malalamiko na amani imetawala,” alisema Wakili Luguwa.
Kadhalika, Wakili wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Isack Kifwoka, naye aliupongeza uongozi wa Kituo cha Usuluhishi na pande zote mbili kwa kutoka walipokuwa awali kwa kuwa kila mmoja wa pande hizo aliona mwenzake ni adui.
“Mmeamua kukaa pamoja kumaliza tofauti zenu kwa njia ya usuluhishi kupitia Kituo hiki, kiukweli sisi kwetu tunaona ni maajabu makubwa sana kiukweli kituo hiki kimefanya kazi kubwa sana kusuluhisha mgogoro huu na hatimaye sasa kila mmoja hapa hakuna mshindi na mmekuwa ndugu,” alisema Wakili Kifwoka.
Naye, Afisa Mtendaji wa Mtaa Tabata Liwiti, Bi. Editha Rugakingira alimshukuru Mhe. Maruma kwa kumaliza mgogoro huo uliochukua miaka mingi na hatimaye kumalizika ndani ya vikao sita. Vilevile aliwapongeza watu wa Kanisa pamoja na wastaafu wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia kwa kumaliza mgogoro huo kwa amani na utulivu.
Kadhalika Mwangalizi wa Kanisa la Moravian lililopo Tabata Jijini Dar es Salaam, Bw. Lyson Kijalo alimshukuru Mungu pamoja na Kituo cha Usuluhishi kinachosimamiwa na Jaji Maruma kwa kumaliza mgogoro huo ambao ulizifanya pande hizo mbili kuwa maadui wakubwa lakini mpaka sasa mgogoro umekwisha na pande zote mbili zimekuwa kitu kimoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni