· Waelezwa majukumu yao
Na FRANCISCA SWAI, Mahakama – Musoma
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma,
Mhe. Fahamu Mtulya amewaapisha Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya katika
Mkoa wa Mara na kuwataka kuzingatia viapo vyao.
Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya
Wilaya walioapishwa jana tarehe 2 Julai, 2024 ni Wakuu wa wilaya za Musoma,
Bunda, Tarime na Rorya ambao ni
Wenyeviti wa kamati hizo pamoja na Makatibu Tawala wa wilaya hizo ambao ni
Makatibu wa Kamati hizo. Aidha, wajumbe wengine wa Kamati hizo pia waliapishwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mtulya alisema kamati
hizo zipo kwa mujibu wa sheria hivyo aliwataka wajumbe hao kuzingatia maadili
ya viapo vyao na kutekeleza jukumu hilo la Kisheria kwa usiri na weledi mkubwa.
‘‘Sheria ya mienendo ya maadili ya Mahakimu inaeleza kwa
undani hakimu aweje, aishije na namna ya kufanya kazi zake. Pale anapovunja
sheria hizi au kukosea katika mwenendo wake ndipo kamati zenu zinafanya kazi,’’
alisema Mtulya.
Mhe. Mtulya aliwaasa wajumbe kuwa kazi zao si
ndogo bali ni kubwa kwani wanatekeleza jukumu la kikatiba na kwa mujibu wa
sheria zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ili
kuhakikisha uwazi na uwajibikaji kamati hizi zinahusisha wajumbe wa namna
mbalimbali ikiwemo wananchi wa kawaida, viongozi wa dini na viongozi wa
kiserikali.
Aidha, Mhe. Mtulya amesisitiza wajumbe katika kutekeleza
majukumu yao wakumbuke kuwa hawatekelezi majukumu hayo kwa vyeo vyao bali kama
wawakilishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Katika zoezi hilo, wajumbe na viongozi wa kamati hizo
walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kupewa ufafanuzi wa maswali
yao. Pia walipewa elimu juu ya sheria mbalimbali zinazoelezea uwepo wa kamati
hizo, namna wanavyoteuliwa, kazi za kamati husika, majukumu ya kila mjumbe
katika kamati hizo pamoja na kuapa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu
na weledi.
Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu
Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe
wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa
na Jaji Mfawidhi.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya
watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia
kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama
Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake
kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati
za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja
na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Sura ya 237.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Salome Mshasha (aliyesimama), akifafanua jambo lililoulizwa na wajumbe katika hafla fupi ya uapisho wa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya, Kanda ya Musoma uliofanyika Mahakama Kuu Musoma.
(Imehaririwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni