Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 14 Agosti, 2024 na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu na kusainiwa na Kaimu Mkurungenzi, Bi. Sharifa Nyanga, Mhe. Dkt. Feleshi ataapishwa kesho tarehe 15 Agosti, 2024 kushika wadhifa huo katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Feleshi alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ambayo aliitumikia tangu tarehe 12 Septemba, 2021.
Kwa sasa, wadhifa huo unachukuliwa na Bw. Hamza Johari ambaye ameteuliwa na Rais Samia akitokea kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe.Dkt. Feleshi alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo alitumikia nafasi hiyo kuanzia tarehe 2 Juni, 2018.
Kama Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Feleshi alishiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika usimamizi wa Mahakama na maboresho yaliyoongozwa na Mahakama chini ya uongozi wa Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jaji Feleshi alifanya kazi kwa karibu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama na wajumbe wengine waandamizi wa Mahakama katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2015/16–2019/20 kuelekea Utoaji wa Huduma za Haki unaowazingatia Wananchi. Aidha, alishiriki kufanyia kazi Mpango Mkakati wa sasa wa Mahakama wa 2020/21–2024/25.
Mhe. Dkt. Feleshi alikuwa pia Jaji wa Mahakama Kuu kuanzia Agosti, 2014 hadi Septemba, 2021 ambapo alifanya kazi katika kituo cha Dar es Salaam kuanzia Agosti, 2014 hadi Februari, 2017; Masjala ya Iringa kuanzia Februari, 2017 hadi Juni, 2018 na Masjala Kuu kuanzia Juni, 2018 hadi Septemba, 2021.
Akiwa Jaji Kiongozi na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Feleshi aliongoza Masjala Kuu ya Mahakama Kuu ya Tanzania na kushiriki katika utoaji maamuzi ya mashauri, pia alishiriki katika usimamizi wa usikilizwaji na utoaji wa uamuzi ya mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Mwanzo nchini. Katika kipindi hicho, Mhe. Dkt. Feleshi aliamua idadi kubwa ya mashauri yanayohusiana na madai ya Katiba, uchaguzi, ardhi, biashara, uasili na ndoa.
Aidha, aliamua idadi kubwa ya mashauri yanayohusiana na jinai kwa mashauri yanayohusiana na uhujumu uchumi na rushwa.
Vilevile, Mhe. Dkt. Feleshi alifanikiwa kufanya mapitio ya mashauri mbalimbali ya jinai na madai na alihakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati.
Taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inaonesha Rais Samia pia amefanya uteuzi wa Viongozi wengine, wakiwemo Mawaziri, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, uteuzi wa Katibu Tawala wa Wilaya, uteuzi wa Wakuu wa Taasisi na uhamisho wa Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni