Jumatatu, 19 Agosti 2024

JAJI MANSOOR AWAAPISHA WAJUMBE WA KAMATI ZA MAADILI WILAYA ZA KILOMBERO, MALINYI NA ULANGA

 Na Evelina Odemba – Mahakama Ifakara Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor amewaapisha Wenyeviti pamoja na wajumbe wa Kamati za maadili ya Maafisa Mahakama wa Wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro

Mhe. Mansoor aliwaapisha wajumbe hao wanaotoka wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi tarehe 16 Agosti, 2024 kwenye ukumbi wa Mahakama ulioko ndani ya Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kilombero.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mhe. Mansoor alisema kuwa kamati zilizokuwepo awali zilikuwa na mapungufu ikiwemo baadhi ya wajumbe kuhama vituo vya kazi hivyo alitoa rai kwa wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa usahihi.

“Nategemea mara baada ya kiapo hiki mtakachokula hivi leo kamati hizi zitakaa, na kutekeleza majukumu yake” alisema Mhe. Mansoor na kuongeza kuwa Mahakama Kanda ya Morogoro itaandaa mafunzo ya ndani ili kuzinoa kamati hizo na kukumbushana mambo mbalimbali ya msingi ya kuzingatia wakati wa utekelezaji wa majukumu.

Sambamba na hilo pia Mhe. Mansoor alizipatia kamati hizo miongozo ambayo itawarahisishia katika utendaji kazi wa kamati hizo na kuwaeleza kuwa mambo hayo yote yamezungumziwa ndani ya miongozo hiyo.

Aidha Akizungumza kwa niaba ya wanakamati wengine, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya  Alisema kuwa wanaahidi kuisimamia kazi hiyo kwa kufuata miongozo na misingi ya sheria ili mwananchi aweze kupatiwa haki yake. “Tunakuahidi kutekeleza vyema kazi yetu kama ambavyo viapo vyetu vimesema” alimaliza Mhe. Kyobya.

Wakuu wa wilaya walioapishwa kuwa Wenyeviti wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwenye wilaya zao pamoja na wajumbe wengine wa Kamati hizo ni Bw. Danstan Kyobya (Kilombero), Bw. Sebastian Waryuba (Malinyi) na Dkt. Julius Ningu (Ulanga).

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inahusisha wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor akizungumza wakati wa zoezi la kuapishwa kwa Wajumbe wa  Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor (kulia) akimuapisha Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyobya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wa Wilaya ya Kolombero.

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akila kiapo cha uadilifu kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wa Wilaya ya Malinyi.

  Sehemu ya Viongozi na Wajumbe walioshiriki hafla ya Kuapishwa kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wa wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

 

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor (kulia) akikabidhi muongozo wa utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwa  Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyobya kwa niaba ya wajumbe wote walioapishwa. 


(Imehaririwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni