Jumanne, 27 Agosti 2024

JAJI MFAWIDHI KITUO JUMUISHI TEMEKE APALILIA USULUHISHI KWENYE MASHAURI YA FAMILIA

NA MAGRETH KINABO -Mahakama,Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa amewahimiza wananchi na wadau kutilia mkazo suala la usuluhishi katika kushughulikia masuala ya familia ili kuimarisha udugu na ustawi wa familia.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 27 Agosti, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho kuhusu miaka mitatu ya utendaji kazi wa kituoni hapo, Mhe. Mnyukwa alisema wanapokea idadi kubwa ya mashauri kwa mwaka, hivyo ni vema yakashughulikiwa kwa njia ya usuluhishi.

Jaji Mfawidhi huyo alisema suala la usuluhishi limeshazungumzwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dk.Samia Suluhu Hassan kwenye hotuba yake siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yaliyofanyika Dodoma tarehe 1 Februari, 2023 na kumnukuu.

Rais Samia alisema, ‘‘Matarajio yangu Watanzania wafike hatua kwenda mahakamani isiwe jambo la     lazima sana,badala yake suala la usuluhishi ndio liwe jambo la lazima.’’  

Aidha, katika kutilia mkazo suala hilo, pia Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Mhe.  Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hotuba yake siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yaliyofanyika Dodoma tarehe 1, Februari,2023 ambapo alimnukuu.

“Baada ya mwaka mmoja wa kusikiliza mashauri ya ndoa na mirathi katika              Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke uzoefu umeonyesha kuwa usuluhishi unahitajika na unaweza kufanyika kwa ufanisi katika mashauri ya ndoa na mirathi.”

Mhe. Jaji Mnyukwa aliongeza kwamba ni dhahiri mashauri ya familia kwa asili yake, yanahitaji usuluhishi ili kuimarisha udugu na kustawisha ustawi wa familia.

“Usuluhishi unaweza kufanyika katika hatua mbalimbali za mashauri yahusuyo ndoa, talaka na watoto.  Kwa kutambua umuhimu wa usuluhishi katika kushughulikia mashauri ya familia wakati tunasherehekea miaka mitatu ya Kituo..

“…tumeazimia kushirikiana  na Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi katika kutoa mafunzo kwa mabaraza ya usuluhishi, Maafisa Ustawi Jamii  na viongozi wa dini ikiwa ni mojawapo ya matukio muhimu yatakayofanyika katika kuadhimisha miaka mitatu,” alisema Mhe. Jaji Mnyukwa. 

Alifafanua kuwa  wameazimia kutoa mafunzo hayo kwa makundi tajwa hapo juu kwa kuwa sheria inawataka kufanya usuluhishi na kutambua mashauri ya ndoa lazima yapite baraza la usuluhushi kabla ya kuja mahakamani.

Hata hivyo Mhe. Jaji Mnyukwa alisema katika kuhudumia wananchi, Kituo kimesadifu jina lake la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Mirathi na Familia ambacho kinajulikana kama One Stop Centre, na watahakikisha upatikanaji wa huduma zote za mashauri ya kifamilia  zinapatikakana kituoni hapo. 

“Katika kufanikisha hilo, Kituo kimekuwa kinafanya kazi kwa karibu na watoa huduma wa msaada wa sheria ambao wanatoa huduma hiyo bure kwa wananchi wanaofika hapa kituoni na huduma hizo kutolewa ndani ya jengo hili. Watoa msaada wa hudma za kisheria bure waliopo katika jengo hili ni LHRC, WLAC, WiLDAF. Pia katika kufanikisha adhma ya kuwa na huduma za familia zinazopatikana kwa pamoja,” alisisitiza.

Alibainisha kuwa Kituo kimekuwa kinafanya kazi kwa karibu na maafisa wanaotoka ustawi wa jamii. Hivyo wadau hao, wamekuwa na msaada mkubwa kwa wananchi wanaopata huduma  ya msaada wa kisheria bure ambapo wanawezesha upatikaji haki kwa wakati. 

Vilevile maafisa ustawi wa jamii wamekuwa wakitoa ushauri nasaha kwa wateja ambao wana mashauri ya familia. Sambamba na wadau hao, Kituo pia kimekuwa kinafanya kazi na Dawati la Jinsia la Polisi pamoja na viongozi wa dini. Wadau wote hawa wanasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati. Hivyo kufikia adhma ya kuhakikisha mwananchi anayekuja kupata huduma katika Kituo hicho anapata pia huduma sanjari za masuala ya kifamilia. 

Mhe. Jaji Mnyukwa alisema katika mwelekeo wa baadae dhamira yao ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu masuala ya mirathi na familia.Kwa kushirikiana na wadau wanatarajia kuendesha kampeni za uandishi wa wosia kwa lengo la kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kuandika wosia. Pia wanatarajia kuwa na vipindi mbalimbali katika vyombo vya habari kuhamasisha wananchii kuandika wosia.

Kadhalika alisema wataendesha kongamano (symposium) ambalo litawakutanisha wadau wao kujadiliana changamoto za mashauri ya familia na namna bora zaidi ya kushughulikia changamoto hizo bila ya kuacha alama ya uadui na chuki miongoni mwa wanafamilia.  

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (katikati) akiwasilisha taarifa ya miaka mitatu ya utendaji kazi wa Kituo hicho kwa Waandishi wa Habari leo tarehe 27 Agosti, 2024. Wengine katika picha ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni, Bi. Mary Shirima.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kituo hicho, Mhe. Gladys Nancy Barthy (wa kwanza kulia katika picha ya juu) akiwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama (juu na picha mbili chini) katika hafla hiyo. Picha pia zinaonesha Waandishi wa Habari wakiwa kazini.



Picha na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni