Na. IMAN MZUMBWE-Mahakama, Songwe
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga juzi tarehe 7 Agosti, 2024 alitembelea Gereza la Wilaya Mbozi mkoani Songwe na kuongea na Wafungwa na Mahabausu waliopo.
Akiwa katika Gereza hilo, Mhe. Tiganga alipokea taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Gereza Zebedayo Ilomo ambaye alibainisha kuwa Gereza hilo lina jumla ya wafungwa na mahabausu 227.
Mkuu huyo wa Gereza alieleza changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo umbali uliopo kutoka gerezani hapo kwenda katika Mahakama ya Wilaya Songwe na Mahakama ya Mwanzo Kamsamba wilayani Momba.
Akiwa ndani ya Gereza hilo, Mhe. Tiganga alitembelea maeneo mbalimbali kama vile sehemu ya kulala Wafungwa na Mahabusu, jikoni na Zahati na baadaye kuzungumza na Wafungwa na Mahabusu wa kiume na kike kwa nyakati tofauti.
Katika tukio hilo, Jaji Mfawidhi alipokea risala zao na kusilikiliza hoja mbalimbali, changamoto na maswali amabayo baadhi yalijibiwa palepaple na changamoto zingine aliwaelekeza wasaidizi wake wazitatue ndani ya siku 14.
Katika mwendelezo wa ziara yake, Mhe. Tiganga alimtembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo Jaji Mfawidhi alipata wasaa wa kueleza changamoto ambazo amekutana nazo alipokuwa katika Gereza la Wilaya ya Mbozi.
Mhe. Tiganga alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa Mahakama inaendelea na maboresho ya hudumu zake, ikiwa ni pamoja na kumaliza mashauri kwa wakati.
Alitumia fursa hiyo kumwomba Mkuu wa Mkoa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kuwaelekeza Jeshi la Polisi kuharakisha na kumaliza upelelezi kwa wakati.
Kadhalika, alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa changamoto ya ukosefu wa Gereza la kuhifadhi Wafungwa na Mahabusu katika Wilaya ya Songwe na kumuomba kunusuru hali hiyo.
Kwa upande wake, Mhe. Chongolo alimweleza Jaji Mfawidhi kuwa anafanya kazi kwa kushirikiana na Mahakama na kumhakikishia kuwa wataendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kimahakama.
Mkuu wa Mkoa aliiomba Mahakama kutilia mkazo juu ya kesi za mimba za utotoni, ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo, kwani imekuwa changamoto kubwa ndani ya Mkoa huo.
Mhe. Chongolo alieleza kuwa adhabu kali zikitolewa kwa wanaofanya uhalifu huo itasaidia kupunguza na kumaliza changamoto hizo katika Mkoa wake.
Wakati huo huo, Jaji Mfawidhi alifanya kikao na wadau Mahakama wa Mkoa wa Songwe, akiwemo Mkuu wa Ofisi ya Mashtaka,TAKUKURU, Mkuu wa Upelelezi, Mkuu wa Gereza, Uhamiaji na Mawakili wa Kujitegemea.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Tiganga aligusia majukumu, mafanikio na changamoto zinazoikabili Mahakama katika utekelezaji wa shughuli za utoaji hakia kama ucheleweshwaji wa upelelezi katika kesi za kijinai.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Jaji Mfawidhi alitembelea mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi Songwe na kukagua maendeleo ya utekelezaji wake.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo, Mhe. Tiganga alimsisitiza Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha kazi ndani ya wakati waliokubaliana kwenye makataba.
Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi aliambatana na baadhi ya Viongozi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, akiwepo Naibu Msajili, Mhe. Aziza Temu, Mtendaji wa Mahakama Mbeya, Bi Mavis Miti, Mhe, Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Bi. Sostenes Mayoka.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Gereza Mbozi mkoani Songwe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga akipitia taarifa ya Mkuu wa Gereza la Mbozi, Zebedayo Ilomo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga katika picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza, Viongozi alioambatana nao na wadau wengine wa Mahakama wa Mkoa wa Songwe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga pamoja na Viongozi alioambatana nao wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo.
Sehemu ya Wadau walio katika kikao na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe, Joachim Tiganga akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi Kituo Jumishi Songwe.
Muonekano wa baadhi ya maeneo ya ujenzi wa kituo hicho.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni