Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amefungua jengo la Mahakama ya Mwanzo Uvinza na kuwataka Watumishi wa Mahakama hiyo kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kuwahudumia vema wananchi.
Hafla ya ufunguzi wa jengo hilo lililojengwa kwa fedha za ndani ilifanyika tarehe 03 Agosti, 2024 Mtaa wa Plantoni ilipojengwa Mahakama hiyo.
Mhe. Rwizile alisema kuwa, urejeshaji wa huduma katika kituo hicho unaunga kwa vitendo kaulimbiu ya Serikali ya “kazi iendelee” na kwa namna moja au nyingine Mahakama nayo inaendeleza na kazi kwa mtindo huo.
“Mahakama imeongeza neno kuwa tufanye kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji, hivyo, kazi inayoendelea iendelee kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji dhana hizi zinakwenda sambamba katika kuwahudumia wananchi,” alisema Jaji Rwizile.
Jaji Mfawidhi huyo, aliwasisitiza Mahakimu na watumishi wengine watakaotumia jengo hilo kuzingatia hayo ili taswira ya Mahakama ibaki kuwa njema.
Mhe. Rwizile aliendelea kusema kuwa, lengo la kujenga jengo hilo ni kurudisha huduma za Mahakama ya Mwanzo Uvinza ambazo zilifungwa kutokana na uchakavu wa jengo la awali.
Aliongeza kuwa, awali katika utatuzi wa kuendelea kutoa huduma za Mahakama ya Mwanzo, huduma za Mahakama hiyo zilihamishiwa katika jengo la Mahakama ya Wilaya Uvinza lililoko eneo la Lugufu takribani kilometa 25. Adha ya kusafiri kwa wananchi kwenda Lugufu wastani wa kilometa 50 kwenda na kurudi, hali hiyo ilisukuma Uongozi wa Mahakama Kigoma kuanza ujenzi wa Jengo hilo ili kuwarejeshea huduma za Mahakama wananchi wa eneo hilo.
Mhe Rwizile aliipongeza Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma akiwemo Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw. Filbert Matotay, Naibu Msajili Mhe Gadiel Mariki na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Rose Kangwa na Viongozi wengine Waandamizi kwa kuharakisha mchakato huo wa kurejesha huduma ya Mahakama kwa kutumia fedha kidogo zinazopatikana kuhakikisha wanasogeza huduma karibu na wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya Uvinza, Mhe. Dinah Mathamani alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mahakama ili kuendelea kuwahudumia wananchi wa Wilaya hiyo.
Mhe. Mathamani aliongeza kuwa, wananchi wa Kata hiyo wanayo fursa ya kutumia vema Mahakama hiyo na kulitunza jengo hilo.
Sambamba na pongezi kwa Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Mkuu huyo wa Wilaya alisema amejifunza kuwa rasilimali fedha ikitumika vizuri inaweza kuleta tija kwa wananchi hivyo alizitaka Taasisi nyingine katika Wilaya hiyo kuiga mfano wa Mahakama kwani urejeshaji wa Huduma hiyo ni faraja kwa wananchi wa Wilaya ya Uvinza.
Aliongeza kuwa, Ofisi yake haijapokea malalamiko yanayotokana na huduma za Mahakama na kwamba hiyo ni ishara kuwa Mahakama inafanya kazi vizuri na kuisihi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.
Mhe. Mathamani alimuhakikishia Jaji Mfawidhi, Mhe. Rwizile kuwa, Wilaya ya Uvinza inakua kwa kasi kwa Taasisi zote ambazo zinatoa huduma kwa wananchi, na kuhusu usalama amemuhakikishia kuwa Uvinza ni salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji na kujipatia kipato cha kila siku.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinah Mathamani, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rose Kangwa, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Wilaya ya Uvinza, Kigoma, Kibondo, Kasulu, Buhigwe na Kakonko, Maafisa wa Kada mbalimbali kutoka Mahakama za Wilaya zote pamoja na wananchi wa Kata ya Uvinza waliojitokeza katika hafla hiyo ya ufunguzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Uvinza.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinah Mathamani akitoa neno la ukaribisho kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati). Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi katika hafla ya ufunguzi wa Mahakama ya Mwanzo Uvinza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni