• Jaji Mfawidhi aungana na Watumishi wake katika mazoezi hayo
• Ni jitihada za kuboresha afya kwa utendaji kazi bora
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewaongoza watumishi wa Kanda hiyo kufanya mazoezi ya viungo mahakamani hapo mara baada ya saa za kazi.
Akizungumza na Mwandishi wetu jana tarehe 16 Agosti, 2024 mara baada ya kumaliza mazoezi, Mhe. Rwizile alisema kufanya mazoezi ni jambo zuri kwa kuwa linaimarisha afya.
“Ukipendelea kufanya mazoezi, mwili unazoea mazoezi unakuwa imara hivyo kwakuwa tunatumia muda mwingi kukaa na kuhudumia wateja wetu basi rai yangu kuwa tutumie muda huo kidogo tulioupanga kunyoosha misuli na viungo mbalimbali vya mwili kwa afya,” alisema Jaji Rwizile.
Kwa upande wa watumishi wa Mahakama hiyo, wameonyesha muamko mkubwa wa kufanya mazoezi hayo kwa kujitokeza kwa wingi na kufurahia mazoezi hayo ya viungo.
Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Kanda ya Kigoma, Bw. Prosper Bonaventure alisema mazoezi hayo yamekuja muda muafaka.
“Mazoezi haya yamekuja kwa muda muafaka kwakuwa watumishi wengi hatupendelei mazoezi aidha mazoezi yamekuwa gharama huko mtaani hivyo tunapopata fursa kama hii ni vema kuitumia vizuri ili kijiimarisha kiafya zaidi,” alisema Bw. Bonaventure.
Kuanzishwa kwa mazoezi hayo ni pamoja na kuimarisha mwili na kuweka vizuri afya za watumishi.
Aidha, watumishi wa Kanda hiyo walijitokeza kwa wingi na kuonesha kufurahia mazoezi hayo ambapo wameomba yawe endelevu kwakuwa yanawaleta pamoja lakini pia yanachangamsha mwili wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mazoezi hayo yalifanyika kwenye eneo la wazi lililopo juu ya jengo la Mahakama hiyo na yaliungwa mkono na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki pamoja Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay.
Ratiba ya mazoezi hayo imepangwa mara mbili kwa wiki kwa siku ya Jumatano jioni na Ijumaa jioni ili iwe sehemu ya kuboresha afya za watumishi hao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akishiriki kufanya mazoezi ya viungo pamoja na watumishi mbalimbali wa Kanda hiyo jana tarehe 16 Agosti, 2024 katika eneo la wazi lililopo juu ya jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki (wa kwanza kulia mstari wa pili) akishiriki kufanya mazoezi ya viungo pamoja na watumishi mbalimbali wa Kanda hiyo katika eneo la wazi lililopo juu ya jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni