- Apogeza mbinu ya kuanya kazi masaa 24
Na. JAMES KAPELE –Mahakama, Katavi
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 28 Agosti, 2024 alikagua shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Katavi na kutoa maelekezo mahsusi ya kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na katika viwango na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba.
Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Ltd chini ya Mkandarasi Mshauri Kiongozi M/s Crystal Consultants.
Awali, kabla ya kufika eneo la mradi, Mtendaji Mkuu alifika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Albert Msovela ambapo, pamoja na mambo mengine, ameiomba menejimenti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutembelea mradi huo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Akiwa katika eneo la mradi, Prof. Ole Gabriel alipokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Ltd, Mhandisi Shaban Kapinga ambaye alibainisha changamoto mbalimbali ambazo zimepelekea ujenzi kuchelewa.
“Mradi wetu umekuwa na changamoto nyingi ambazo sehemu kubwa zimetatuliwa. Kwa sasa tumejiwekea mikakati mbalimbali ya kukamilisha kazi kwa kuhakikisha malighafi zote zinazotakiwa zinafika katika eneo la ujenzi na kuongeza kasi ya kazi kufanyika kwa masaa 24 ili tukamilisha ifikapo tarere 22 Disemba, 2024,” alisema.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mtendaji Mkuu alifanya ukaguzi na kuelekeza ujenzi huo kukamilika kwa wakati. Alionesha kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa za kukamilisha ujenzi kwa kuzingatia matakwa ya mkataba na maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa.
“Niseme tu kwamba ubora wa kazi hauna mashaka kabisa, tatizo ni muda wa kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba. Nimefurahishwa na juhudi mlizofanya za kutatua changamoto mlizokuwa nazo, hasa hii ya kufanya kazi kwa masaa 24 na hii ya kuleta maligafi zote zinazohitajika kwenye eneo la mradi,” alisema.
Aliwataka kuhakikisha mikataba ya wakandarasi wengine saidizi (Sub Contractors) iwe tayari tarehe 30 Agosti, 2024 ili kazi za ujenzi zisikwame kwa sababu hiyo.
Mtendaji Mkuu pia aliwahimiza Wakandarasi kuzingatia kalenda ya shughuli zilizopangwa kufanyika kwa kipindi cha utekelezaji wa makataba pamoja na ubora wa vifaa vinayonunuliwa, licha ya kuhofia bei ya manunuzi.
Alisisitiza kwamba vifaa vyote viwepo tayari katika eneo la mradi, ikiwa ni pamoja na mpangilio wa nguvu kazi iliyopo ili kukidhi kalenda ya matukio ya ujenzi wa jengo hilo unakamilika kama lilivyokusudiwa.
Moja ya nguzo katika Mpango Mkakati wa Mahakama ni utoaji haki kwa wakati. Mahakama ya Tanzania inatekeleza mpango huu kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki kwa wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hii.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyeketi kushoto) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kutoka kulia) akipokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi kutoka kwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Lt,d Mhandisi Shaban Kapinga (wa tatu kutoka kulia).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akipitia mchoro wa ramani ya ujenzi pamoja na Wahandisi na Viongozi Waandamizi wa Mahakama Mkoa wa Katavi waliombatana naye katika ziara hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akishuka katika moja ya ngazi za jengo hilo akiendelea na ukaguzi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzani,a Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na wahandisi wengine akiendelea na shughuli za ukaguzi kwenye mradi huo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyeketi kushoto) akiwa katika kikao cha majumuisho pamoja wa wajumbe wengine katika chumba cha mikutano katika eneo la mradi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni