Alhamisi, 29 Agosti 2024

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA AWATAKA WATUMISHI KUTHAMINIANA

  Na MAGRETH   KINABO -Mahakama, Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa rai kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa kuthaminiana,licha kuwa elimu na ngazi tofauti za utendaji kazi, kwa kuwa wanafanya kazi  ya  kuiwezesha Mahakama kutimiza jukumu lake la msingi la utoaji haki.

Akizungumza leo tarehe 29 Agosti, 2024 wakati alipotembelea Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kigamboni na kuzungumza na watumishi wa mahakama hizo, wakiwemo wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mtendaji huyo, alisema kila kazi ina changamoto yake, hivyo wategemeane katika utendaji wao wa kazi.

“Jambo la muhimu ninalotaka kuwaambia ni mthaminiane katika nafasi zote za kiutumishi, kwa kuwa kila mtu ana thamani yake katika kazi anayoifanya, awe ni mlinzi, mhudumu au ofisa. Hivyo kila mtumishi anapaswa kuendelea kufanya kazi vizuri ili watu wafurahie kazi anayoifanya,” amesema Mtendaji huyo Prof. Ole Gabriel.

Prof. Ole Gabriel aliwashauri watumishi hao, wasiridhike na elimu au vyeo walivonavyo, bali wajiendeleze kielimu, hali itakayofanya kupanda vyeo mbalimbali katika Utumishi wa Umma, huku akitolea mfano kuwa yeye alianza na kazi ya uhudumu lakini sasa amekuwa ni profesa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Amesema pia watumishi hao, wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wasibaguane kwa  kuwa wote wanafanya kazi ya kumsaidia Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kwenye jukumu lake la  utoaji haki kwa wananchi.

Mtendaji huyo amewapongeza watumishi hao, kwa kufanya kazi kwa kujituma licha kuwa upungufu wa watumishi 4,000, kwani kwa sasa mahitaji ya watumishi kwenye Mahakama  ya Tanzania ni 10,351, lakini kuna watumishi 5,800.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Vicky Mwaikambo amesema Mahakama hiyo ilianzishwa kupitia tangazo la Serikali namba 36 la tarehe 02Februari, 2018, na ilianza rasmi kufanya kazi tarehe 22 Juni,2018.Kufikia Novemba, 2020 Mahakama hiyo ilichaguliwa kuwa Mahakama ya mfano katika kusajili mashauri na kuandika mienendo ya mashauri bila kutumia makaratasi (paper less court).

 Zoezi hili pia lilihusisha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (virtual court). Hivyo, kuanzia Novemba, 2020 hadi tarehe 5 Novemba, 2023 jumla ya mashauri ambayo yamesikilizwa bila kufunguliwa kwa njia ya kawaida (nyaraka ngumu) ni mashauri 1,265,” amesema Mhe. Mwaikambo.   

Mhe. Mwaikambo ameongeza kuwa katika kipindi cha Desemba 2023 mashauri yaliyo lala ni 96, funguliwa kuanzia Januari 2024 ni 160 na yaliyobaki ni 105, amuliwa ni 150, yakiwemo ya Mlundikano tisa.  Alisema mashauri yaliyolala Desemba 2023 katika Mahakama ya Mwanzo ni 152, funguliwa Januari mpaka Agosti 28, 2024 ni 933, yaliyoamuliwa ni 917 na yaliyobakia ni 168.

Aidha amefafanua kuwa ili kujenga na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau, shughuli mbalimbali zimefanyika  kufikia lengo hilo, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kila siku ya Jumatatu na Jumatano, uwepo wa Mahakama Klabu katika Shule ya Sekondari Makonda, ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa wakati pamoja na kufanya vikao vya kusukuma mashauri ya jinai na madai.

 

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka amesema  katika kipindi  cha Januari, 2024 Kanda hiyo ilivuka mwaka 2023na mashauri8,146 na kati ya Januari hadi Juni 2024 jumla ya mashauri yaliyofunguliwa ni 12,056 na yaliyosikilizwa na kuisha ni 10,697 na yaliyobaki ni 9,646.

“Takwimu hizi zinaonesha kwamba kiwango cha uondoshaji wa mashauri kwa Kanda ni asilimia 89 na wastani wa umaliziaji wa mashauri ni asilimia 53, Aidha kwa kipindi hicho Kanda ilikuwa na mzigo wa mashauri 20202 na wastani wa mzigo kwa majaji ni 124 na mahakimu ni 130,” amesema Bw. Mashaka.

Mashaka ameongeza kwamba kwa upande wa mashauri ya mlundikano hadi Juni, 2024 Kanda ilikuwa na jumla ya mashauri ya mlundikano 537 sawa na asilimia sita ya mashauri yote yaliyobaki 2023, hivyo takwimu za Agosti 28, 2024 zinaonesha kuwa mashauri ya mlundikano yaliyopo katika Kanda ni 330. Mahakama Kuu mashauri ya Mlundikano ni 37, Mahakama za Hakimu Mkazi 165, Mahakama za Wilaya 128, huku Mahakama za Mwanzo zikiwa hakuna mlundikano. 

Akizungumzia kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) amesema mfumo wa e-CMS, umeendelea kutumika katika ushughulikiaji wa mashauri yote kwa Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya, ambapo mashauri 5,099 yalisajiliwa katika mfumo huo. Pia usikilizwaji kwa njia ya mtandao jumla mashauri 727 yalisikilizwa kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2024 na maamuzi 478 yalipandishwa kwenye TANZILII. 

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kigamboni, Mhe.Geuza Rashid Mbeyu na Mtunza Kumbukumbu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Bi.Anjelina Msagati wakizungumza kwa niaba ya wenzao walimshukuru Mtendaji huyo kwa kuwatembelea na kuendelea kuboresha utendaji  wa mahakama hizo.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel(kushoto) akisaini katika kitabu cha wageni mara baada kuwasili katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Vicky Mwaikambo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Vicky Mwaikambo, akitoa taarifa ya utekelezaji ya mahakama hiyo na Mahakama ya Mwanza Kigamboni.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel(kushoto) akisalimiana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Franco Sebastian Kiswaga.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel(kushoto) akisalimiana Mhasibu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Bi. Anna Clement.
Baadhi ya watumishi wa mahakama mbalimbali  za Kanda ya Dares Salaam, wakimsikiliza. Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Picha namba 4528 ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Bw. Beatus Mlando Benedictus na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Bi. Athanasia Kabuyanja wakimsikiliza Mtendaji huyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Vicky Mwaikambo(katikati) akimkabidhi Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel(kulia) ‘flash’ yenye taarifa utekelezaji wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kigamboni.

 Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka (aliyesimama)akitoa taarifa ya  utendaji kazi wa Kanda hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka(kulia) akimkabidhi taarifa hiyo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel(kushoto).

Mtendaji Mkuu Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo baada ya kupata taarifa ya mahakama hizo.

Picha ya juni na chini ni Mahakimu na watumishi mbalimbali wa mahakama za Kanda ya Dar es Salaam wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, alipokuwa akizungumza não.


Mtendaji Mkuu Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akipata maelezo kuhusu mifumo ya TEHAMA inavyofanyakazi katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kigamboni kutoka kwa Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima(kushoto).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akizungumza na mahakimu na watumishi mbalimbali wa mahakama za Kanda ya Dar es Salaam. Wengine ni Watendaji na Mahakimu wa Mahakama mbalimbali za Kanda hiyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kigamboni, Mhe.Geuza Rashid Mbeyu akitoa neno la shukurani.

Mtunza Kumbukumbu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Bi.Anjelina Msagati akitoa neno la shukurani.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akiwa katika picha ya pamoja na wahudumu.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,(mstari wa mbele katikati )akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa mahakama za Kanda ya Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,(mstari wa mbele katikati akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa mahakama za Kanda ya Dar es Salaam wanawake.

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,akiagana na watumishi hao.

(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni