Na Lydia Churi na Evelyne Odemba- Morogoro
Tume ya Utumishi wa Mahakama inakusudia kuanzisha mfumo
wa kielekitroniki utakaoratibu masuala ya Ajira, Maadili na nidhamu kwa
watumishi wa Mahakama.
Katika mchakato wa kuanzishwa kwa Mfumo huo, leo Agosti
6, 2024 Tume imekutana na wadau wake muhimu katika kikao kazi kilichoanza mjini
Morogoro kwa lengo la kupokea maoni na mapendekezo kwa lengo la kuanzisha mfumo
huo utakaorahisisha utendaji kazi na kuleta uwazi zaidi.
Akifungua rasmi kikao kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor alisema kuanzishwa kwa
mfumo wa Kielekitroniki wa Ajira, Maadili na nidhamu ndani ya Tume ya Utumishi
wa Mahakama ni muendelezo wa safari mageuzi
ya mfumo ya Mahakama ya Tanzania ili kuboresha shughuli za utoaji haki nchini.
”Katika dunia ya sasa teknolojia inakua kwa kasi na
shughuli nyingi za Serikali inafanywa kwa mfumo huo, kwa kutambua hili, Tume imeona
ni vema kuwa na mfumo wa kielekitroniki utakaoratibu masuala ya Ajira, Maadili
na Nidhamu kwa watumishi wa Mahakama”, alisema.
Aidha, Jaji Mansoor alitoa rai kwa wadau kutoa michango
ya mawazo itakayozaa matunda yatakayowezesha kujengwa kwa mfumo bora zaidi wa
ajira ambao utafungamanishwa na mfumo wa kielekitroniki wa uendeshajiwa Kamati
za maadili ambazo Wenyeviti wake ni wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.
Awali akitoia neno la utangulizi, Katibu wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa
lengo la kikao hicho ni kupata maoni ya wadau kuhusu uanzishwaji wa mfumo ambao
utaleta mabadiliko ya Utendaji kazi wa Tume.
“Nia yetu ni kuona kwamba Tume ya Utumishi wa Mahakama ya
Tanzania inaenda kuwa kitovu cha mageuzi ndani ya Afrika na duniani kote katika
matumizi ya TEHAMA”, alisema.
Alitaja baadhi ya mada zilizowasilishwa katika kikao kazi
hicho kuwa ni pamoja na rasimu ya mafunzo kuhusu mfumo huo, rasimu ya masuala
ya ajira, kushirikishana uzoefu wa masuala ya TEHAMA na kujadiliana namna ya
kuboresha mfumo huo ulioanza kujengwa.
Alisema kuwa ujio wa mfumo huo utasaidia katika kusimamia
rasilimali watu, ajira, maadili na nidhamu na utakuwa na manufaa kwa Tume ya Utumishi
wa Mahakama na watanzania kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama Bw. Jocktan Bikombo alisema kuwa Tume imedhamiria kuanzisha kuanzisha Mfumo
ambao utasaidia kupanua wigo wa kiutendaji kazi wake.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo
cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya
Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzaniua Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa Kikao Kazi Maalum kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mfumo wa kuratibu Ajira, Maadili na Nidhamu wa Tume leo tarehe 6 Agosti, 2024 mjini Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni