Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Singida
Tume ya Utumishi wa Mahakama imedhamiria kuwafikia
wananchi na kuwaelimisha kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama
za Mikoa na Wilaya zinazopokea
malalamiko ya Wananchi yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama.
Akifungua mafunzo maalum ya siku mbili kwa Maafisa
Tarafa wa Mkoa wa Singida leo mkoani humo, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Alex Mbuya alisema mafunzo hayo
yatawawezesha wananchi kufahamu uwepo wa Kamati hizo na kuwasilisha malalamiko
yao.
Alisema Tume imeona ni muhimu kuwatumia Maafisa Tarafa
kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yake ikiwemo namna ya kuwasilisha
malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili kwa Maafisa Mahakama kwa kuwa
Maafisa Taarafa ni kiungo kati ya Serikali na Wananchi katika Tarafa na ni wawakilishi
wa Wakuu wa Wilaya katika shughuli za kijamii, miradi ya maendeleo na katika
kutatua migogoro ya wananchi.
”Moja ya mikakati ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na
kuwaelimisha ni kwa kuwatumia ninyi Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida lengo
likiwa ni kuwaelimisha ninyi ili nanyi mkawaelimishe wananchi hasa mnapokutana
nao kupitia fursa mlizonazo mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku kwa
wananchi”, alisema.
Naibu
Katibu alisema kuwa mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa misingi ya utawala bora
ya Tume unaozingatia Sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi na utekelezaji
wa majukumu ya Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa na Wilaya.
Alisema, ni matarajio ya Tume kuwa, kupitia mafunzo
hayo Maafisa Tarafa wataisaidia Tume kuwaelimisha wananchi namna ya kuwasilisha
malalamiko yao kwa njia sahihi ili waweze kupata haki kwa wakati.
Alizitaja
Mada zitakazotolewa kwenye mafunzo hayo kuwa ni Tume ya Utumishi wa Mahakama,
Muundo na Majukumu yake, Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa
Mahakama za Mikoa na Wilaya na uwasilishaji wa malalamiko pamoja na Mgawanyo wa
majukumu kati ya Mihimili ya Dola.
Aidha,
aliwasisitiza Maafisa hao kuzingatia maadili ya Uongozi katika Utumishi wa Umma
na kujiepusha na vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano mwema na wananchi wanaofika kupata
huduma kwenye maeneo yao.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ilitoa mafunzo kama haya
mwezi Juni mwaka huu kwa kwa Maafisa Tarafa 23 wa Mkoa wa Arusha.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia
uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia
Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza
jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia
Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa
katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu
cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni