Jumatano, 18 Septemba 2024

‘BILA MAAD'ILI HAKUNA HUDUMA BORA’

Na EVELINA ODEMBA – Mahakama, Morogoro

 

Mkurugenzi wa Utawala na Raslimaliwatuwa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewataka washiriki wa mafunzo ya maadili na huduma kwa mteja kuzingatia maadili ya kazi wakati wa utoaji huduma.

 

Bi Beatrice alitoa wito huo tarehe 17 Septemba, 2024 mjini hapa wakati anafungua mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa watumishi wa Kada ya Wasaidizi wa Ofisi na Walinzi. 

 

Alieleza kuwa mafunzo hayo ni nguzo iliyopo katika mpango mkakati wa Mahakama ili kuwajengea uwezo na kuongeza ujuzi na maarifa kwa watumishi wa Mahakama.

 

Aliongeza kuwa mada zitakuwa wezeshi kwa watumishi hao ikiwemo kuwa na maadili mema mahala pa kazi, kuwa namna ya kuwapokea na kuwahudumia wananchi wanaofika mahakamani na madhara ya rushwa ambayo ni chanzo cha uvunjifu wa maadili.

 

“Ndugu washiriki, maadili ni msingi wa utendaji kazi bora na wenye ufanisi, bila maadili hakuna huduma bora itakayoweza kutolewa kwa wananchi ambao ndio wateja wetu. Ni matarajio yangu kuwa mara baada ya mafunzo haya kila mmoja ataelewa wajibu na majukumu aliyonayo kama Mtumishi wa Mahakama na atakuwa mtenda kazi mzuri katika kutoa haki sawa na kwa wakati,” alisisitiza Bi. Beatrice.

 

Bi. Beatrice alisema kuwa anaamini kuwa washiriki hao wataimarishiwa mara dufu uwezo wao katika kutekeleza majukumu yao kupitia mada mbalimbali zitakazotolewa na wawezeshaji.

 

“Mtakuwa wapya wenye maarifa mapya, motisha na dhamira thabiti huku mkitambua kuwa mafanikio ya Mahakama yetu yanategemea juhudi na utayari wa kila mmoja wetu katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi, maarifa na uadilifu” alisema.

 

Awali, wakati akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patrice Ngungulu alisema kuwa jumla ya washiriki 130 watapatiwa mafunzo.

 

Aliongeza kuwa mada zitakazofundishwa ni pamoja na majukumu ya wasaidizi wa ofisi na walinzi na maadili ambayo anapaswa kuwa nayo, huduma kwa mteja, na mkataba wa huduma kwa mteja, uelewa kuhusu masuala ya jinsi na jinsia, umuhimu wa kutunza afya, huduma ya kwanza na zimamoto, na kujiandaa kustaafu, ambazo zinabeba sehemu kubwa ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku mahali pa kazi.

 

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni aliwataka washiriki kuzingatia na kufanyia kazi yale yote watakayofundishwa katika mafunzo hayo, hiyo ndio shukurani pekee wanayopaswa kuitoa kwa waandaaaji.

 

“Hongereni kwa kubahatika kupata mafunzo haya, rai yangu ni wote mliopo hapa mzingatie yale mtakayoelekezwa kwani mafunzo haya yameandaliwa kwa gharama kubwa, hivyo tusiwaangushe waandaaji,” alisema.

 


 Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akifuatilia utambulisho wa washiriki (hawapo pichani) wakati wa kufungua mafunzo ya maadili na huduma kwa mateja.


 

Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu akizungumza wakati akitoa neno la utangulizi kabla ya kufunguliwa kwa mafunzo.



Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni akizungumza wakati akiwakaribisha washiriki katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro wakati wa zoezi la ufunguzi wa mafunzo.



 Sehemu ya washiriki wa mafunzo (juu na chini) wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa ufunguzi.


 


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick (aliyesimama mbele) akiwasilisha mada kwa washiriki.


 

Meza kuu ikiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick (aliyekaa wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo.


 


  


Meza kuu ikiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick (aliyekaa wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya mafunzo.


Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha akifuatilia matukio wakati wa ufunguaji wa mafunzo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni