Na Innocent Kansha- Mahakama
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Rose Ally Ebrahim
amewakumbusha Majaji na Mahakimu waliopata mafunzo ya Wakufunzi ya namna bora
ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi ‘Election Dispute Resolution’ kutoa elimu
hiyo kwa Maafisa wengine kwa kuzingatia ujuzi na weledi walioupata ili kupata mwongozo
na maarifa ya pamoja wakati wa utatuzi wa migogoro hiyo.
Mhe. Ebrahim ametoa wito huo leo tarehe 19 Septemba, 2024 jijini Dar es salaam alipokuwa anafunga mafunzo hayo ya siku tatu yenye lengo la kuwaandaa Majaji na
Mahakimu kuongeza weledi wa namna bora ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi yaliyoendeshwa
jijini Dar es salaam kwa ufadhili wa Taasisi ya Kimataifa Inayoshughulika na
Mifumo ya Uchaguzi (IFES) na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama –
Lushoto (IJA).
Mhe.
Ebrahim amesema mafunzo hayo siyo tu yametoa fursa ya elimu ya namna bora ya
kutatua migogoro ya uchaguzi bali yamewawezesha kujenga uwezo wa namna bora ya
kuwaelimisha Maafisa Mahakama wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki
mafunzo hayo.
“Mafunzo
haya ya Wakufunzi yameongeza chachu ya kuhakikisha ujuzi huu unawafikia wengine
kwa usahihi na ufanisi mkubwa ili kila Afisa Mahakama atende yale yanayopaswa
kutimizwa wakati wa utatuzi wa migogoro ya uchaguzi kwa weledi mkubwa. Hivyo
basi wale wote tuliopata mafunzo haya tuna jukumu la kuhakikisha tunawafundisha
wenzetu ambao hawakushiriki mafunzo hayo moja kwa moja,” amesema Jaji Ebrahim.
Aidha,
Mhe. Ebrahim amesema mafunzo hayo yamejenga msingi wa uelewa wa pamoja wa namna
bora ya kuendesha na kutatua migogoro ya uchaguzi katika viwango
vinavyokubalika kisheria kwa kuzingatia msingi wa haki, ufanisi na uwazi katika
kila mamlaka za kimahakama wakati wa kutatua migogoro hiyo.
“Mashauri
yatokanayo na migogoro ya uchaguzi yana changamoto nyingi na ni nyeti huku
yakivuta hisia za watu wengi hasa katika nchi zinazozingatia mifumo ya
kidemokrasia. Kupitia mafunzo haya ya Wakufunzi wa utatuzi wa migogoro ya uchaguzi
yametuongeza ujuzi na shime ya uelewa wa namna bora ya utatuzi wa migogoro
ikiwa ni sehemu pia ya namna ya kuelimisha maafisa Mahakama wenzetu mbinu hizi
za kiufundi tulizofundishwa,” amesisitiza Mhe. Jaji Ebrahim
Mhe.
Ebrahim ameongeza kuwa, kupita mafunzo yamewakumbusha mambo ya msingi ikiwemo
kusimamia uhuru wa Mahakama, kufanya maamuzi bila upendelelo ikizingatiwa
kwamba haki wakati wote ndiyo itasimamia utatuzi wa migogoro ya uchaguzi.
Kwa
upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam
Mhe. Salma Mussa Maghimbi akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa
mafunzo ya wakufunzi ya namna bora ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi amesema
kipindi cha siku tatu za mafunzo hayo ni muhimu sana kwa Mahakama katika
jitihada za kustawisha maendeleo ya utoaji haki nchini.
“Tunatambua
kwamba ili nchi yoyote iweze kuendelea inahitaji serikali imara inayotokana na
uchaguzi huru na wa haki, kwa kipindi cha mafunzo haya tumejifunza mambo mengi
ya muhimu yatayokuwa ya msingi kwa Mahakama kama chombo huru kisichokuwa na
upande wakati wa utatuzi wa migogoro ya uchaguzi,” amesema Jaji Maghimbi.
Mhe.
Maghimbi amesema mafunzo hayo yameibua mambo ya msingi ya kuyazingatia wakati
wa utatauzi wa migogoro ya uchaguzi ikiwemo suala la muda, kutambua sheria
zinazohusika na namna bora ya kuzitumia kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi
na baada ya uchaguzi, pia kutambua aina ya migogoro ya uchaguzi kama ina asili
ya jinai ama madai.
Mafunzo
hayo ya wakufunzi wa utatuzi wa migogoro ya uchaguzi yaliwajumuisha jumla ya washiriki
32 wakiwemo Majaji, Naibu wasajili, Mahakimu Wakazi wa mikoa na Wilaya nchini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Rose Ally Ebrahim akitoa nasaha kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa kufunga rasmi Mafunzo ya siku tatu kwa Wakufunzi wa utatuzi wa migogoro ya uchaguzi leo tarehe 19 Septemba, 2024 jijini Dar es salaam.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam Mhe. Salma Mussa Maghimbi akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo ya wakufunzi ya namna bora ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa Inayoshughulika na Mifumo ya Uchaguzi (IFES) nchini Tanzania Bw. Lamin Lighe akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo hayo yaliyohitimishwa leo jijini Dar es salaam.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya wakufunzi wa namna bora ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi wakifuatilia hotuba ya kufunga mafunzo hayo.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni