Jumanne, 17 Septemba 2024

JAJI MFAWIDHI KIGOMA AONGOZA MAZISHI YA ALIYEKUWA HAKIMU MKAZI MFAWIDHI MASASI

Azikwa Kigoma kitaaluma na Majaji/Mahakimu
Asindikizwa na mamia ya Wananchi

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, ameongoza watumishi wa Kanda hiyo na mamia ya wananchi katika mazishi ya aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Masasi marehemu Batista Kindaga Kashusha aliyefariki dunia tarehe 13 Septemba, 2024.

Marehemu Kashusha alizikwa jana tarehe 16 Septemba, 2024 katika kitongoji cha Katombo katika kijiji cha Mgaraganza Kata ya Kagongo Wilaya ya Kigoma vijijini. 

Safari ya kumsindikiza Marehemu Kashusha ilianza na misa takatifu iliyoambatana na sala ya wafu ili kumuombea marehemu iliyoongozwa na Padri Flavian Rutakangwa, ambapo aliwataka waombolezaji kumuombea marehemu kwani yeye ameumaliza mwendo na imani ameilinda na kuwataka kuiga mfano wa Mhe. Kashusha ambaye aliishi maisha ya imani katoliki katika maisha yake yote na kujitolea zaidi katika shughuli za Kanisa.

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza alisema kuwa, Jaji Mkuu alipokea taarifa za kifo cha Mhe. Kashusha kwa masikitiko, hivyo anawapa pole familia yake, wananchi, ndugu na jamaa walioguswa na msiba huo.

Kadhalika Mhe. Kahyoza alitoa salaam za rambirambi kwa wafiwa kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. Projestus Kahyoza alisema, “Mhe. Kashusha nimemfahamu kwa kufanya naye kazi hivyo familia ya Mahakama na familia yake tumepoteza jembe kwelikweli, hivyo hatuna budi kukubali kuwa kazi ya Mungu haina makosa.”

Mhe. Kahyoza alisema, kama isingekuwa kifo Mhe. Kashusha alitegemea kupata likizo ya kustaafu Utumishi wa Umma mwaka huu ili apate kupumzika lakini Mungu amempenda zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa msafara wa kumsindikiza marehemu Kashusha kutoka Mkoani Mtwara alipokuwa akihudumu Marehemu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mzava, alisema kuwa anamshukuru Mungu maana wamesafiri kwa umbali mrefu kutoka Mtwara mpaka mkoani Kigoma bila tatizo lolote.

Hata hivyo, Mhe. Mzava aliwashukuru Majaji Wafawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda za Mtwara na Kigoma kwa kushirikiana kufanikisha mazishi ya marehemu Mhe. Baptista Kindaga Kashusha.

Akisoma historia fupi ya chanzo cha kifo cha marehemu Mhe. Kashusha, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Bw. Julius Irembe Christopher, alisema kuwa marehemu alifariki ghafla huku chanzo chake kikiwa ni shinikizo la damu lililomtokea ghafla na kufikishwa hospitali kupata matibabu na hatimaye kupoteza uhai wake tarehe 13 Septemba, 2024.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili (TLS) Mkoa wa Kigoma, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Wilaya na Mkoa wa Kigoma, Viongozi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Buronge, Viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mgaraganza pamoja na mamia ya wananchi walioguswa na msiba huo kutoka maeneo mbalimbali.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile  (katikati) akiwa na Mahakimu Wakazi wakimsindikiza marehemu Baptista Kindaga Kashusha katika nyumba yake ya milele jana tarehe 16 Septemba, 2024.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Projestus Kahyoza akitoa salamu  kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara,  Mhe. Charles Mzava akitoa neno la shukrani kwa Mwajiri (Mahakama ya Tanzania) kwa kuwezesha kusafirisha mwili kutoka Masasi- Mtwara mpaka mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.
Mahakimu Wakazi wakiwa wamenyanyua sanduku lenye mwili wa marehemu Baptista Kindaga Kashusha kumpeleka katika nyumba yake ya milele.

 Mhe. Eva Mushi akiwa ameshika picha ya marehemu Baptista Kindaga Kashusha. Pamoja naye ni Mahakimu Wakazi mara baada ya kufika malaloni kwa ajili ya mazishi ya Hakimu mwenzao.
Sehemu ya watoto pamoja na wananchi wengine wakiwa katika mazishi ya aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Masasa, marehemu 
Baptista Kindaga Kashusha

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni