Jumamosi, 28 Septemba 2024

MAHAKAMA SPORTS ROBO FAINALI

•        Yatinga robo fainali kwenye mchezo wa Kamba, Mpira wa Miguu.

•        Haikamatiki kwenye riadha.

 

Na. EVELINA ODEMBA MAHAKAMA – Morogoro

 

 Baada kupata ubingwa mnono upande wa riadha, Mahakama Sports Club jana tarehe 27 Septemba, 2024 iliendelea kuonesha uwezo wake baada ya kufuzu kwenye hatua ya 16 bora, ushindi ambao unaiongoza moja kwa moja kuelekea hatua ya robo fainali kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea mjini Morogoro. 

 

Timu ya Kamba Wanawake (KE) iliwaburuza Mifugo wakati Kamba Wanaume (ME) ikiwavuta kama karatasi RAS Iringa katika mchezo uliofanyikia Uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro.

 

Upande wa Mpira wa Miguu, Mahakama imejipatia ubingwa dhidi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuwacharaza washika mtutu hao mabao mawili kwa sifuri. Magori yote yalifungwa katika kipindi cha kwanza ndani ya Uwanja wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA). 

 

Licha ya kuwa mashindano bado yanaendelea, upande wa Mahakama tayari imeshajitwalia ubingwa katika mchezo wa riadha ambapo upande wa wanawake mfukuza upepo Juster Tibendelana ameibuka kidedea  kwa kutwaa ubingwa mara mbili katika mbio za mita 3000 pamoja na mita 800.

 

Mbali na hilo, Mahakama kupitia wanariadha wake imechukua nafasi ya kwanza katika mbio za wazee wanaume, mshindi wa pili mbio za mita 100 wanaume na wanawake na mshindi wa pili wa mbio za kupokezana vijiti upande wa wanawake.

 

Pamoja na hatua kubwa waliyopiga, iBundi ametua upande wa timu ya mpira wa pete baada ya kuyaaga mashindano kwa kupoteza mchezo wake ambao walikuwa wanachuana na timu toka Wizara ya Elimu iliyopita kwa ushindi mwembamaba wa magori 22 kwa 20.

 

Matokeo hayo yanaiondoa Mahakama katika mchezo huo, huku kocha wa timu hiyo akiahidi kuwa wanaenda kujipanga kivingine na kuahidi kuwa katika mashindano yajayo watafanya vizuri zaidi.

 


Kikosi cha timu ya kamba wanaume (ME) toka Mahakama Sports kikiwa katika harakati za kuisaka nafasi ya kuingia robo fainali. 

Kikosi cha timu ya kamba wanaume (ME) toka Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja mara baara ya kufuzu hatua ya kuingia robo fainali.


Kikosi cha timu ya kamba wanawake (KE) toka Mahakama ya Sports wakifurahia ushindi dhidi ya Mifugo (hawapo pichani).


Kikosi cha timu ya mpira wa miguu toka Mahakama Sports wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mechi dhidi ya Mambo ya Ndani.


Mchezaji wa timu ya mpira wa miguu toka Mahakama Sports akipambana uwanjani dhidi ya washika mitutu toka Mambo ya Ndani.


Kikosi cha timu ya mpira wa miguu toka Mahakama Sports kikifanya dua ya pamoja kabla ya kuwavaa timu ya Mambo ya Ndani katika hatua ya pili.


Washangiliaji wa Mahakama Sports wakicheza kwa furaha baada ya Mahakama kuibamiza Mambo ya Ndani gori mbili kwa sifuri.


Kikosi cha mpira wa pete toka Mahakama Sports kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mchezo wake dhidi ya Elimu.


Mfukuza upepo toka Mahakama Juster Tibendelana akiinua mikono kwa ushindi wakati akielekea kuuvuka mstari wa ushindi wa nafasi ya kwanza katika mbio za mita 3000.


Baadhi ya wanariadha toka Mahakama Sports wakiwa katika picha ya pamoja na kocha na Katibu wao mara baada ya kuutwaa ushindi.


Timu ya mbio za vijiti toka Mahakama Sports wanawake wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki kabla ya kuanza mchezo huo ulioiweka Mahakama kuwa nafasi ya pili.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni