Jumanne, 1 Oktoba 2024

MAHAKAMA YA TANZANIA YAJA NA MAHAKAMA TENTI

  • Inaweza kuweka kambi na kutoa huduma kwa muda mrefu

Na JEREMIA LUBANGO, Mahakama-Dodoma

Mahakama ya Tanzania imetambulisha Mahakama Tenti (Justice Tent) yenye huduma zote za kiofisi ambazo Hakimu anazihitaji wakati wa kutekeleza wajibu wake wa kusikiliza mashauri na kutoa huduma. 

Mahakama Inayotembea (Mobile Court) ndio linaibeba Mahakama Tenti ambayo ina uwezo wa kukita kambi kwenye maeneo tofauti tofauti ambayo yako mbali na huduma za kimahakama. 

Akizungumza wakati wa utambulisho wa huduma hiyo jana tarehe 30 Septemba, 2024 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Naibu Msajili ambaye pia ni Mratibu wa Huduma za Mahakama Zinazotembea ‘Mobile Court Services’, Mhe. Moses Ndelwa alisema Mahakama hiyo tenti imetengenezwa kwa ajili ya kupiga kambi kusikiliza mashauri ya eneo hilo kwa kipindi cha muda mrefu.

“Mfano tunaenda Wilaya ya Chemba, Mkalama pale, tutafanya ‘session’ kwa miezi mitatu na hii ndio kazi yake tofauti na ‘mobile court’ ambazo leo inafanya eneo hili kesho eneo tofauti,” alisema Mhe. Ndelwa.

Alisema pia, uwepo wa Mahakama Tenti itasaidia kwa maeneo ambayo Mahakama bado hazijaanza kujengwa ili iweze kutumika kama mbadala.

Naye, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa alisema ni ngumu kujenga Mahakama 200 kwa wakati mmoja na pia ni ngumu kujenga Mahakama sehemu mmoja na kuweza kuihamisha lakini uwepo wa Mahakama Tenti ina uwezo wa kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

“Badala ya kuwa na Mahakama 200 katika maeneo 200 tunaweza kuwa na Mahakama Tenti mbili ambazo zinaweza kuhudumia wananchi katika maeneo hayo,” alisema Mhe. Tengwa.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kufanya maboresho mbalimbali na kufurahiswa na kile ambacho walijadili kipindi cha nyuma kuweza kutekelezwa.

Muonekano wa Nje wa Mahakama Tenti iliyowekwa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

 
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mratibu wa Huduma za Mahakama Zinazotembea (Mobile Court Services), Mhe. Moses Ndelwa akizungumza na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania (hawapo katika picha) kuhusu Mahakama Tenti inavyofanya kazi.

Sehemu ya watumishi wa  Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mratibu wa Mahakama Zinazotembea (Mobile Court Services), Mhe. Moses Ndelwa (aliyesimama) alipokuwa anatoa maelezo namna Mahakama Tenti inavyofanya kazi.

 
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Mashauri Tengwa akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika utambulisho wa Mahakama Tenti jana tarehe 30 Septemba, 2024 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Chiganga Mashauri Mahakama ya Tanzania Tengwa (wa tatu kutoka kulia) akizungumza na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania walipokuwa wakikagua Mahakama Tenti (Justice Tent). Kutoka kushoto ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo, wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Elimo Massawe, wa pili kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Bw. Ginaweda Nashon.
 
Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo akichangia mada alipokuwa katika utambulisho wa Mahakama Tenti jana tarehe 30 Septemba, 2024 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania waliofika kwenye utambulisho wa Mahakama Tenti jana tarehe 30 Septemba, 2024 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa ndani ya Mahakama Tenti.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni