Na Innocent Kansha, Arapha Rusheke –Mahakama, Dodoma
Jaji
kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani leo
tarehe 6 Disemba, 2024 ametunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Dodoma
maarufu kama (UDOM) ambapo
mahafali hayo yamefanyika kwenye Ukumbi wa mikutano Chimwaga jijini Dodoma.
Akizungumza
mara baada ya kutunukiwa Shahada hiyo ya Uzamivu Mhe. Dkt. Siyani amesema kama
Muhitimu wa shahada ya Uzamivu ya chuo Kikuu cha Dodoma alijiunga Chuoni hapo miaka
mitatu iliyopita na amefanikiwa kuhitimu safari yake ya Shahada ya Uzamivu
(PhD) kwa miaka mitatu ambacho ni kipindi cha chini kabisa kama ambavyo
taratibu za chuo zilivyowekwa.
“Ni siku ya
furaha kwangu kuona kwamba nimefikia tamati ya safari ya shahada yangu ya
uzamivu kwa mafanikio pamoja na furaha hii niliyonayo ningependa kuzungumza
mambo machache kwa watanzania na wengine ambao wanafutailia. Safari ya masomo
ya shahada ya uzamivu ni safari ambayo mimi ningetamani kila mtanzania mwenye
nafasi aifanye kwa maana inatoa fursa ya kujikita na kuwa mbobevu katika maeneo
mbalimbali ambayo mtu atachagua na kwa hivyo kumpa mtu nafasi ya kuweza
kuchangia Maendeleo ya Taifa letu,” amesema Dkt. Siyani.
Mhe. Dkt. Siyani ameongeza kuwa, Chuo hicho
kinatoa fursa ya idadi kubwa ya wanafunzi wa uzamivu mathalani wahitimu wa
uzamivu walikuwa takribani 54 ambao wamehitimu shahada zao za uzamivu.
“Safari ya
masomo ya shahada ya uzamivu inataka mtu kutenga muda wa kutosha lakini pia
kuwa na nidhamu ya huo muda kwa maana
kwamba kwa mimi binafsi ambaye
nilikuwa naendelea na majukumu ya kazi na huku nikisoma ilikuwa inanihitaji
kuwa na nidhamu ya muda kuhakikisha kwamba ninapata nafasi ya kuendelea kuwahudumia
watanzania lakini pia ninatimiza majukumu yangu…
kama
mwanafunzi, na kwa kupitia fursa hii napenda kuwaamasisha wafanyakazi wenzangu
ambao wapo Mahakama ya Tanzania lakini wafanyakazi na watumishi wa Serikali na
watanzania kwa ujumla kuendelea kujiendeleza ni jambo la muhimu kwasababu bila
elimu hatuwezi kupiga hatua za haraka za kuliletea maendeleo Taifa letu,”
amesema Jaji Kiongozi huyo.
Aidha, Mhe.
Dkt. Siyani amesema mwisho wa safari ya masomo imemuhamasisha kufanya kitu
kingine kama mhitimu tayari ameanza kufikiria kitu kingine cha kufanya pamoja
na kutumia taaluma hiyo aliyoipata kwenye safari hiyo ya masomo, tayari amefikiria
kufanya maandiko mengine mengi ili watuwengi zaidi waweze kupata elimu ambayo
ameimepata na kupitia utaalam ambao ameupata.
“Shahada yangu ya uzamivu imejikita katika
eneo la utoaji haki ningependa watu wengi zaidi wafahamu utafiti na tasnifu
yangu, ilikuwa inaangalia changamoto ambazo Mahakama inakumbana nazo katika
kuhakikisha kwamba inatimiza jukumu la kikatiba la kutoa haki kwa wakati. Kwa hiyo tasnifu iyo imesheheni mambo
mbalimbali ambayo ni changamoto za kisheria lakini pia za kiutendaji na
mapendekezo ya nini kifanyike ili kuhakikisha kiu ya watanzania ya kupata haki
kwa wakati inatimia. Ninatazama namna ambavyo nita andika zaidi ili watanzania
watakao pata fursa ya kusoma nao waweze kufahamu wanapokuwa na shauri Mahakamani
watarajie nini wafanye ilikuhakikisha kwamba tunatimiza takwa la katiba la
kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wakati,” amesema Jaji Kiongozi.
Naye, Mwenyekiti
wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Dodoma Profesa Rwekaza Mkandara amewapongeza kwa
dhati wahitimu wote walioweza kumaliza masomo yao kwa mwaka 2024 katika fani
zote ambazo wanatunukiwa vyeti vyao.
“Vilevile
nawapongeza wanataaluma na wafanyakazi wengine kwa kazi kubwa waliyoifanya na
kufanikisha waitimu hawa kumaliza masomo yao. Napenda kuwaasa wahitimu wetu
kuwa baada ya kupata tuzo zenu muweke mbele dhamira ya kujiendeleza kielimu na
maono ya baadae kwa sababu tupo katika dunia yenye ushindani mkubwa wa maarifa kwa
hiyo lazima kuendana na wakati. Sote kwa pamoja tumeungana kuhakikisha kuwa
wahitimu wanaandaliwa vizuri na kukomaa kitaaluma kwa viwango vya kimataifa,”
amesema Profesa Mkandara.
Jaji kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akitunukiwa Shahada ya Uzamivu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Dkt Stergomena .L.Tax katika Chuo Kikuu cha Dodoma maarufu kama (UDOM) leo tarehe 6 Disemba, 2024 ambapo mahafali hayo yamefanyika kwenye Ukumbi wa mikutano Chimwaga jijini Dodoma.
Jaji
kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa
kwanza kushoto) akipongezwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania
Prof.Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia )
mara baada ya kuhitimu shahada yake ya uzamivu.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) akiwa sehemu
ya mahafali hayo.
Jaji
kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa nne
kutoka kulia ) akisoma kiapo cha maadili ya taaluma mara baada ya kutunukiwa shahada ya uzamivu wakati wa
mahafali hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Chimwaga jijini
Dodoma.
Jaji
kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa
kwanza kushoto) akiwa na sehemu ya wahitimu wa shahada ya uzamivu wakati wa
mahafali hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Chimwaga jijini
Dodoma.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni