- Awataka kuzingatia nguzo tano za uweledi za uwakili
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama,
Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12 Desemba, 2024 amewapokea na
kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea 524 wapya na kuwataka kuzingatia nguzo tano
za uweledi za uwakili wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kuwa waaminifu na
kujisimamia.
Akizungumza katika sherehe
hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof.
Juma ametaja nguzo nyingine kama kuwa na uwezo, kupata heshima, kuwa na ujasiri
na kufanya kazi kwa uhuru bila shinikizo.
“Uweledi katika kazi ya
Uwakili ni kanuni, tamaduni, tabia, mazoea na taratibu ambazo zimekubaliwa kuwa
zinawaongoza Mawakili katika kazi na zinawatambulisha, kuwapambanua na
kuwatofautisha na taaluma zingine,” amesema.
Akizungumzia nguzo hizo,
Jaji Mkuu amesema kuwa lazima kila Wakili anatakiwa kutambua kuwa uaminifu na
kuaminika itampambanua kuwa ni Mawakili mwenye uweledi au la.
“Vipimo na vigezo vya
uaminifu na kuaminika kwenu vimetajwa katika Kanuni za Kimaadili, Kiweledi,
Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili. Kanuni ya 6 ya Kanuni hizi imeainisha
mifano ya Mawakili wasio na uaminifu na kukosa uaminifu ni kukosa Uweledi na
ukimuona wakili huyo, muepuke,” amesema.
Kuhusu nguzo ya uwezo, Mhe.
Prof. Juma amebainisha kuwa kwa vitendo, kwa kauli na kwa viwango vya huduma, lazima
Wakili aonyeshe kuwa kweli umesoma Sheria na Shahada ya Sheria na kwamba maandishi
na fikra zake zijionyeshe kuwa yeye ni mwanasheria na ni Wakili.
Ameeleza kuwa Kanuni za
Kimaadili, Kiweledi, Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili za mwaka 2018 zinataka huduma
za Wakili zionyeshe uwezo na ujuzi unaotarajiwa kutoka kwa Wakililinganifu na
mwanasheria aliyesoma chuo kikuu na kuiva.
“Kanuni za 8 hadi 14 za Kanuni
za Kimaadili, Kiweledi, Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili, 2018 zinasisitiza
wateja wenu, Mahakama na wananchi wanayo haki ya kutarajia kuwa mnao uwezo kufanya
kazi ya uwakili itakayokuwa inawakabili,” Jaji Mkuu amesema.
Mhe. Prof. Juma
amebainisha pia kuwa kupitia Chama cha Mawakili, Mawakili wanatakiwa kujisimamia,
kujiendesha na kujiangalia kiuweledi, kimaadili na kitaaluma bila kuingiliwa na
Taasisi za Dola kama Serikali, Bunge na Mahakama.
“Kila Wakili, anao wajibu
wa kujisimamia na kuwasimamia Mawakili wenzake ili watekeleze kanuni
zinazosimamia Uweledi na Uadilifu wa Mawakili. Kudharau au kutokutekeleza
Kanuni zenu wenyewe, ni kuhujumu Uhuru wa Taaluma ya Uwakili na pia manufaa ya
umma ambayo Kanuni zenu za Uweledi na Uadilifu zinalenga,” amesema.
Jaji Mkuu amewaambia Mawakili
hao pia kuwa katika safari yao ya kufikia uweledi, watatafuta nguzo muhimu ya
kupewa “Heshima” bila ya kuiomba au kuidai.
“Heshima hapa ni kwa
tabia na mwenendo wa Wakili, kila siku na kila wakati. Jamii inampa heshima,
anaheshimika, anawaheshimu Mawakili wenzake, anawaheshimu wateja wake,
anawaheshimu Majaji, Mahakimu na anawaheshimu watumishi wote katika mfumo mzima
wa utoaji wa haki,” amesema.
Mhe. Prof. Juma amebainisha
pia kuwa Wakili mwenye Uweledi au Ubobezi ni kama jengo imara lisilo na nyufa
na wananchi watakaofuata huduma za Wakili, hawatakuwa na sababu za kuhofia
madhara yoyote. Amesema kuwa zifa zake humtangaza Wakili aliyetimiza safari na
kufikia nguzo zote za uweledi na uadilifu.
Akizungumza katika sherehe
hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari amewaambia Mawakili hao kuwa
wanayo nafasi kubwa katika kuhakikisha jukumu la utoaji haki linatekelezwa kwa
ufanisi na Mahakama.
Amesema kuwa kama Maafisa
wa Mahakama Mawakili wanapaswa kuhakikisha wanaisadia Mahakama kutekeleza
jukumu la utoaji haki nchini kwa kutoa tafsiri sahihi za sheria ili kutenda
haki na kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki zao wanapokwenda mahakamani au
kwenye vyombo vingine vya kisheria.
Katika harakati zenu za
kusimamia haki, ni muhimu kujua kuwa jukumu lenu ni kubwa zaidi ya
kuwawakilisha wateja. Ninyi ni walinzi wa haki, wawakilishi wa uadilifu, na
watetezi wa sheria katika jamii yetu. Malalamiko ya wananchi kuhusu kutotendewa
haki yatapungua kwa kiasi kikubwa mkitimiza wajibu wenu kikamilifu,” Mhe.
Johari amesema.
Naye Rais wa Chama cha
Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Msomi Boniface Mwambukuzi amewaeleza Mawakili
hao kujenga tabia ya kuheshimu maamuzi yanayotolewa na Mahakama katika ngazi
mbalimbali.
“Ukiona haujaridhika, kata
rufaa,” amesema na kuwasisitizia Mawakili hao wapya kuwa lazima watambue kuwa
kazi yao inatokea ndani ya mfumo wa Mahakama, ambayo ni nguzo muhimu katika
utawala wa sharia na utoaji wa haki.
“Kama wawakilishi wa sharia,
mnajukumu la kuheshimu Mahakama kama Taasisi. Mahakama siyo tu nisehemu ya
kutoa hukumu, bali pia ni chombo cha kuhifadhi na kutetea haki za kila mtu.
Kupokelewa kwa Mawakili hao
wapya 524 kunafanya idadi ya Mawakili wa Kujitegemea nchini kufikia 12,995.
Kati ya Mawakilinhao wapya 524, wa kiume ni 296 na wa kike ni 228. Mawakili 214
wamepata msamaha wa kutohudhuria Shule ya Sheria Tanzania, 16 walifaulu Mtihani
wa Uwani na 294 wamemaliza masomo yao katika Shule ya Sheria.
Miongoni mwa Mawakili
wapya waliokubaliwa na kupokelewa leo na Jaji Mkuu ni Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Wilfred Dyansobera, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Eva Nkya, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Katibu wa
Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Naibu Wasajili na Mahakimu mbalimbali pamoja na
wananchi wengine.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wastaafu nao walihudhuria sherehe hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni