Jumanne, 10 Desemba 2024

KITUO JUMUISHI TEMEKE CHAADHIMISHA MIAKA MITATU TANGU KUANZISHWA

  • Jaji Mkuu aipongeza Serikali kwa uwezeshaji kuboresha mfumo utoaji haki

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali kuchukua mkopo Benki ya Dunia wa Dola za Kimarekani milioni 91 ili kuboresha mfumo wa utoaji haki, ikiwemo Vituo Jumuishi wa Utoaji Haki tisa vipya vinavyojengwa katika Mikoa mbalimbali nchini.

Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo leo tarehe 10 Desemba, 2024 kama Mgeni Rasmi katika sherehe ye maadhimisho ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke ambayo imefanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania ziliridhia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maboresho Baada ya Majengo Jumuishi sita kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Oktoba, 2021 na kuonyesha mafanikio makubwa katika utoaji haki. Kwa sasa, Vituo Jumuishi vinajengwa Simiyu, Geita, Katavi, Njombe, Songwe, Songea, Lindi, Singida na Pemba…

“Tunaweza kusema, mafanikio ya Kituo Jumuishi Temeke yamechangia kujenga hoja za kujengwa vituo jumuishi vingine tisa. Tusherehekee mafanikio ya miaka mitatu ya Kituo Jumuishi Temeke kama chachu ya ujenzi wa Vituo Jumuishi tisa zinazoendelea kujengwa nchini,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa sherehe hizo za Kituo Jumuishi Temeke ni miaka mitatu tangu Rais Samia alipozindua majengo sita Jumuishi ambayo ni fahari ya Tanzania yaliyojengwa Dodoma, Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Arusha, Mwanza na kukumbusha kuwa hatua hiyo ni matunda ya ushirikiano wa karibu baina ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.

Mhe. Prof. Juma ameeleza pia kuwa sherehe hizo ni kumbukumbu ya mbinu mpya iliyotumiwa na Serikali ya Tanzania kutatua changamoto ya muda mrefu ya uchakavu mkubwa na kutokuwepo na miundombinu ya Mahakama na kwamba Serikali ya Tanzania ilikopa kutoka Benki ya Dunia ili Mahakama ya Tanzania itekeleze Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kupitia Programu ya Maboresho.  

“Kwa mara ya kwanza Benki ya Dunia ilijitokeza katika maboresho ya huduma za utoaji haki kwa kiasi kikubwa. Tunasherehekea miaka mitatu ya Benki ya Dunia kujitokeza kufadhili ujenzi wa miundombinu ya Mahakama kwa kutambua kuwa utoaji wa haki kwa weledi, ufanisi na uwazi ni wezeshi kwa ukuaji wa uchumi, biashara na ustawi wa wananchi,” amesema.

Jaji Mkuu amefafanua kuwa kutokana na unyeti wa mashauri ya ndoa, talaka, watoto, matunzo ya watoto na mirathi, Mahakama ya Tanzania iliamua kati ya vituo sita jumuishi zilizokuwa zikitarajiwa kujengwa, angalau Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kimoja kitumike kushughulikia migogoro ya kifamilia.

“Maamuzi haya ya kutenga kituo Jumuishi Temeke yalisukumwa na tatizo la uwepo wa idadi kubwa ya mashauri ya mirathi pamoja na mashauri ya ndoa na talaka. Mfano, kati ya mwaka 2017-2019 kulikuwepo na mashauri 7,600 ya mirathi ambapo kati yake mashauri 3,765 yalikuwa katika ngazi ya Mahakama za mwanzo. Mashauri ya ndoa na talaka yalikuwa takribani 4,200 kati ya mwaka 2017-2019,” amesema.

Aidha, Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa msukumo na uhitaji wa kuwa na Kituo Jumuishi Mahsusi kwa mashauri ya watoto, ndoa, talaka, matunzo na mirathi ilitoka katika asasi za kiraia na wadau wengine wa haki za binadamu kama Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Chama Cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA).

“Katika nyakati tofauti tofauti, vyama hivi viliwasilisha hoja zao kwa uongozi wa Mahakama. Hivyo basi, leo hii tunasherehekea pia za miaka mitatu ya Mahakama ya Tanzania kuwasikiliza wadau walioomba kuanzishwa kwa Mahakama ya Masuala ya Familia Temeke Dar es Salaam,” amesema.

Jaji Mkuu ameeleza pia kuwa kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Programu ya Maboresho, Mahakama ya Tanzania ilijenga hoja kwa Serikali ya Tanzania, na Serikali ya Tanzania ilikubali kuwa, Mahakama ya Tanzania ni mtekelezaji muhimu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

“Mahakama ikisogeza huduma zake sehemu zote Tanzania na ikitekeleza majukumu yake ya utoaji haki kwa ufanisi, weledi na uwazi itaichangia Tanzania kuyafikia Malengo Makuu Matano yaliyotajwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025,” amesema.

Mhe. Prof. Juma ameyataja baadhi ya malengo hayo yanayotekelezwa na Mahakama ni pamoja na kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja; kujenga utawala bora; na kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani na nchi nyingine duniani.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kuzungumza na wananchi, Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Kituo kimefanikiwa kuhudumia idadi kubwa ya wananchi ambao wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa.

Amesema kuwa kitakwimu, ndani ya mwaka wa kwanza wa kutoa huduma, mwaka 2021 hadi 2022, Kituo kilipokea wastani wa wateja 700 kwa siku, mwaka wa 2022 hadi 2023, Kituo kilikuwa kinapokea wastani wa wateja 971 na kwa mwaka 2023 hadi 2024, Kituo kimekuwa kinapokea wastani wa wateja 890 kwa siku. Hivyo wanajivunia kwa idadi hiyo ambayo ni ishara kwamba wananchi wanaridhika na huduma zinazotolewa Kituoni.

“Kitakwimu, tangu kuanzishwa kwa Kituo hadi kufikia tarehe 26 Agosti, 2024, Kituo kimehudumia wateja wapatao 580,610; kati ya hao wanaume wakiwa 265,985, sawa na asilimia 45.8, wanawake 311,183, sawa na asilimia 53.6 na watoto waliohudumiwa ni 3,442, sawa na asilimia 0.6,” Mhe. Mawanabaraka amesema.

Kwa upande wa mashauri, amebainisha pia kuwa kipindi cha mitatu kuanzia tarehe 27 Agosti 2021 mpaka tarehe 26 Agosti 2024, Kituo kimesajili jumla ya mashauri 22,929, kati ya hayo yaliyoamuliwa ni 20,077, ambayo ni sawa na asilimia 88 ya mashauri yote yaliyofunguliwa na yale ambayo hayakusikilizwa ni 2,852, sawa na asilimia 12.

Viongozi mbalimbali wa Mahakama na wadau mbalimbali wamehudhuria sherehe hizo, wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Wasajili na Watendaji wa Mahakama, Mawakili wa Kujitegemea, Viongozi wa Dini, Wanafunzi wa Shule ya Sheria kwa Vitendo na Watumishi wa Kituo Jumuishi Temeke.

Wakati wa maadhimisho hayo, Jaji Mkuu wa Tanzania alizindua taarifa maalum ambayo imeandaliwa na Kituo hicho kuonesha kazi mbalimbali ambazo zimefanyika katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka mitatu tangu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kianzishwe.



Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akizungumza katika maadhimisho hayo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizundua taarifa maalum inayoonesha kazi mbalimbali zilizofanyika kwa kipindi cha miaka mitatu ya Kituo hicho.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) ikifuatilia kilichokuwa kinajiri kwenye maadhimisho hayo.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wastaafu, watumishi na wadau wengine wa Mahakama (juu na chini) ikiwa kwenye maadhimisho hayo.


Sehemu nyingine ya watumishi katika maadhimisho hayo (juu na chini).



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni