Na Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa
juzi tarehe 05 Disemba 2024 alifungua mafunzo kwa watumishi wapya wa Mahakama
Kanda hiyo ya kuwajengea uwezo ili kuzifahamu vema kanuni za kiutumishi na kuwakumbusha
misingi ya maadili ya utumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao.
Akizungumza
katika hafla fupi ya ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Nongwa aliwasisitiza watumishi hao kujenga
utamaduni wa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kutanguliza weledi unaoleta
ufanisi kazini.
“Mnapaswa
siku zote kama watumishi kufanya kazi kwa bidii na kutumia maarifa mliyonayo
kwa weledi mkubwa ili kuleta ufanisi kazini na pia kujiepuka na vitendo vya
rushwa kwani ni kinyume na sheria za nchi na ni kitendo kinacho chafua taswira
ya Mahakama ambacho ni chombo cha umma cha utoaji haki,” aliongeza Mhe. Nongwa.
Aidha,
mafunzo hayo yalitolewa kwa kuzingatia taaribu na kanuni za utendaji wa
shughuli za Mahakama. Hivyo watumishi hao walijengewa uwezov katika maeneo
mbalimbali na kutambua namna bora Mahakama inavyoendesha shughuli zake kwa
kufuata utaratibu na miongozo iliyowekwa katika kutekeleza shughuli hizo, mfano;
kuitambua mifumo mbalimbali ya ndani ya TEHAMA inayotumika kuendeshea mashauri mahakamani
na ile inayotumika kiutawala na kifedha.
Vilevile,
mafunzo hayo yalilenga kuelekeza watumishi hao taratibu mbalimbali za kitumishi
hususani eneo la shughuli za kiutawala hasa kufahamu taratibu za kuomba likizo,
uombaji wa ruhusa, ujazaji wa taarifa katika mfumo wa watumishi na namna ya
upandishwaji wa madaraja kwa watumishi.
Watumishi
hao pia, walipata elimu ya namna ukaguzi wa ndani wa masurufi unavyofanyika kwa
watumishi wa Mahakama. Mathalani nani anayekaguliwa na kwa nini anakaguliwa, na
pia majukumu ya msingi mkaguzi wa ndani wa fedha.
Akifunga
mafunzo hayo Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bi. Mavis Miti kwa niaba ya
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa aliwasihi
watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, kufuata sharia, miongozo na
kanuni za utumishi wa umma ili kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kuichafua
Mahakama.
“Mnaenda
katika maeneo tofauti kufanya kazi katika Mahakama za mkoa wa Mbeya na wengine
pengine mnabaki hapa Mahakama Kuu, nawaomba mjiupesha na vitendo vya rushwa na
kufanya kazi kwa uaminifu kwa kuwa mtumishi atayekutwa kafanya vitendo kinyume
na miongozo na kanuni za utumishi wa umma anaweza kuchukuliwa hatua na akafutwa
kazi,” alisema Bi. Miti.
Nao
watumishi hao kwa kwa nyakati tofauti waliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Mbeya kwa kuwezesha mafunzo hayo kwani yamewajengea uwezo na
kukumbushwa wajibu wao katika ufanyaji kazi kwa kuzingatia maadili, kanuni na
misingi inayoiongoza Mahakama Tanzania katika kutimiza wajibu wake wa kikatiba.
“Tunashukuru
tumejifunza vitu vingi na kutambua sheria na kanuni za mtumishi wa umma na
tunaomba mafunzo haya yafanyike mara kwa mara ilikuweza kukumbushana, na
tunaahidi hatuta vunja heshima ya Mahakama Tanzania” alisema mmoja wa mtumishi
hao.
Aidha,
mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalum wa ndani wakiwemo Mtendaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti, Mkaguzi wa Ndani Bw. Bakari Msangi, Mkuu wa
Kitengo cha TEHAMA Injinia Sadati Kalungwana, Mwasibu Mwandamizi Bw. Nasir
Upete na Afisa Utumishi Mwandamizi Mahakama Kuu Mbeya Bw. Alintula Ngalile.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa (kulia) akiwa anafuatilia mafunzo mara baada ya kuyafungua, kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni