Ijumaa, 13 Desemba 2024

MAJAJI, MAHAKIMU KUTOKA UGANDA, KENYA NA RWANDA WAVUTIWA NA MFUMO WA UNUKUZI NA TAFSIRI

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Majaji, Wasajili na Mahakimu wa Nchi za Uganda, Kenya na Rwanda hivi karibuni kwa nyakati tofauti walitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa namna shughuli za Mahakama zinavyofanyika ndani ya Mahakama za Tanzania sanjari na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya pamoja na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa walishiriki pamoja na wageni hao katika ziara hiyo ya kutembelea IJC Arusha.

 Wakati wageni hao wakiwa katika Mahakama hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha pamoja na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. James Mniko walieleza na kuonesha kwa kwa vitendo namna mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) unavyofanya kazi na jinsi unavyomrahisishia kazi Jaji au Hakimu wakati wa kusikiliza mashauri na kutoa mwenendo wa mashauri kwa muda mfupi. 

Majaji na Mahakimu hao kutoka Kenya, Rwanda na Uganda walionesha nia na shauku ya kuwa na mfumo wa TTS katika nchi zao ili kurahisisha utendaji wao wa kazi na hatimaye kuweza kuwahudumia wananchi wao kwa wakati.

Akiwakaribisha mahakamani hapo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Elia Mrema aliwaeleza Majaji na Mahakimu hao kuwa Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kiasi kwamba mashauri yote kuanzia Mahakama ya Wilaya hadi Mahakama ya Rufani yanapokelewa, kusajiliwa na kusikilizwa kwa njia ya mtandao (e-CMS)

“Kwa sasa Mahakama ya Tanzania imeanza mkakati wa kuacha kutumia muda mwingi kuandika mazungumzo kwa mkono wakati mashauri yanasikilizwa, mchakato ambao ni mrefu na ni gharama, hivyo Mahakama inatumia Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) kwa lengo la kurahisisha uandaaji wa mienendo ya mashauri katika muda mfupi na kwa wakati,” alisema Mhe. Mrema.

Vile vile, Majaji na Mahakimu hao walitembelea ofisi mbalimbali zilizopo ndani ya jengo la IJC Arusha ikiwemo Mahakama ya Watoto (Juvenile Court) ambayo iliwavutia sana na kukiri kuwa nchi ya Tanzania inajali na kuthamini Haki za Watoto, kadhalika, walitembelea chumba maalum cha kunyonyeshea kwa ajili ya akina Mama wenye Watoto wadogo wanaokuja kupata huduma mahakamani.

Majaji na Mahakimu hao kutoka Kenya, Rwanda na Uganda walikuja nchini Tanzania hivi karibuni kushiriki Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) uliofanyika katika Hoteli ya Gran Melia` jijini Arusha.

Hivyo, walitumia fursa hiyo kutembelea Mahakama ya Kituo Jumuishi (IJC) Arusha kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kimahakama katika nchi zao.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eva Nkya (wa pili kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Wasajili kutoka Kenya na Uganda walipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha hivi karibuni. Wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winfrida Mokaya (Katikati), Msajili wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Isaac Wamaasa (wa kwanza kushoto), wa pili kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Mhe. Sarah Langa Siu na Msajili Mkaguzi wa Mahakama Uganda, Mhe. Pamela Lamunu Ocaya ( wa kwanza kulia). Waliosimama nyuma wa pili kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa,  wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha, katikati ni Mwanasheria wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Kenya, Mhe. Robert Kibor, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya na wa kwanza kulia ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji Kanda ya Arusha, Mhe. James Mniko.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa kwanza kushoto) na wageni kutoka Kenya na Uganda wakifuatilia kwa makini maelezo kuhusu Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) unavyofanya kazi wakati wa ziara ya Wasajili wa Nchi hizo walipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha hivi karibuni.

Rais wa Majaji na Maafisa wa Mahakama wa nchi ya Rwanda, Mhe. Harrison Mutabazi akiwa pamoja na Jaji wa Mahakama za Mwanzo wa Rwanda, Mhe. Grace Uwanyirigira (katikati) wakimpatia zawadi ya picha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta walipotembelea Kituo hicho hivi karibuni.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta (kulia) akiwasalimia na kuwashukuru Majaji, Wasajili na Mahakimu kutoka nchi ya Rwanda walipotembelea Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu. Aliyesimama kushoto kwa Mhe. Mugeta ni Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya Arusha, Mhe. Elia Mrema.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri -Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha (aliyesimama) akielezea namna Mfumo wa TTS unavyofanya kazi kwa Wasajili kutoka Kenya na Uganda walipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Sehemu ya Majaji, Wasajili na Mahakimu kutoka Rwanda wakiwa katika picha ya pamoja walipotembelea Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni