Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa
Chama cha Waajiri Tanzania, Bi. Suzanne
Ndomba-Doran ameziomba nchi za Afrika Mashariki kuangalia uwezekano wa
kuoanisha sheria zinazohusu sekta ya ajira na kazi ili kuwa na uelewa wa
pamoja katika utatuzi wa migogoro ya kazi katika ukanda huo.
Bi. Ndomba-Doran ametoa
wito huo leo tarehe 4 Desemba, 2024 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu
Uoanishaji Sheria za Kazi Afrika Mashariki ili Kuboresha Utatuzi wa Migogoro
kwenye siku ya nne ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu
kutoka Nchi za Afrika Mashariki unaofanyika jijini hapa.
“Kama nchi zote
tunajadiliana suala zima la Umoja wa Afrika Mashariki na maeneo mengine
machache ambayo tayari yanajadiliwa, nafikiri hata hili linawezekana. Jinsi
gani litafanyika ni suala la majadiliano zaidi namna ya kuangalia. Tunaweza
tusikubaliane katika maeneo yote kwa sababu nchi hizi zinatofautiana, lakini
pia kuna maeneo ambayo tunaweza kukubaliana,” amesema.
Amebainisha kuwa
ukiangalia katika sheria za kazi zilizopo unaweza kuona kuna maeneo ambayo
hakuna utofauti kubwa, mfano vipengele vinavyohusu likizo za uzazi na hiyo
inatokana na nchi hizo kuridhia mikataba fulani ya Shilika la Kazi Duniani.
“Zoezi hili la uoanishaji
wa sheria za kazi lina faida. Kama tunazungumzia ulinganifu na kama watu
wanatoka sehemu moja kwenda nyingine, mfano suala la uhamishaji wa mafao, kila
nchi ina utaratibu wake wa kulipa mafao. Sheria za Tanzania zinaruhusu raia wa
nje akimaliza muda wake anaweza kutoa yale mafao…
“Lakini labda tunaweza
kuwa na mikataba ambayo inaruhusu kwamba yale mafao yake yanaweza kusomeka
katika nchi yake, lakini sheria za nchi zote lazima ziangalie jinsi gani mafao
yale yanaweza kusomeka ili kuhakikisha ule mustakabali mzima wa pensheni uweze
kuwa na uhalisia,” Mkurugenzi huyo amesema.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Majaji tayari wameshaanza kuangalia sheria za nchi zingine zinafanyaje na wamezitumia katikakuamua mashauri. Ametoa mfano wa mashauri kadhaa yaliyoshughulikiwa na Mahakama ya Rufani Tanzania, ikiwemo ya CCBRT Hospital dhidi ya Daniel Celestine Kivumbi na ile ya Standard Chartered Bank Ltd dhidi ya Justin Teneishemo.
Kadhalika, Bi.
Ndomba-Doran amemnukuu Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Kenya, Mhe. Mhe. Dkt.
Priscah Wamucii Nyotah, ambaye alizungumzia kuhusu umri wa mtoto wa kufanya
kazi. “Kwenye hili kulioanisha ni ngumu? Kwa sababu kuoanisha inaweza ikawa
siyo kuwa na sheria moja, lakini mkakubaliana kwenye kifungu kinachohusiana na
masuala hayo,” amesema.
Kabla ya kuhitimisha mada
yake, aliwaeleza washiriki namna utendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
inavyosaidia na pia jukwaa la utatu linalofanywa na Mahakama kuwaalika waajiri
na wafanyakazi kwa pamoja kujadili masuala mbalimbali, changamoto na kuangalia
maeneo ya kuboresha zaidi.
Baada ya uwasilishaji wa
mada hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kenya, Mhe. Jemimah Keli aliongoza mjadala
uliochangiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Linda Lilian Tumusiime
Mugisha na Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Mahakama ya Kenya, Mhe. Dkt. Priscah
Wamucii Nyotah kabla ya kuruhusu washiriki wa Mkutano huo kuuliza maswali.
Mkutano huo unahudhuriwa
na washiriki zaidi ya 380 kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar, Burundi na
Sudani ya Kusini na mada mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa zikilenga kuboresha
huduma ya utoaji haki katika nchi za Ukanda huo.
Kaulimbiu ya Mkutano huo
inasema; ‘Uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa ajili ya kuimarisha
utengamano na Ukuzaji Uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.’
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni