Alhamisi, 5 Desemba 2024

PROF. OLE GABRIEL ATAKA UJENZI WA MAHAKAMA YA MWANZO HAUBI KUKAMILIKA MAPEMA

Na ARAPHA RUSHEKE- Mahakama Kondoa 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.Elisante Ole Gabriel jana tarehe 4 Desemba, 2024 amekagua shughuli zinazoendelea katika mradi wa ujenzi  wa Mahakama ya Mwanzo Haubi na kutoa maelekezo mahsusi ya kukamilisha mradi huo kwa wakati, viwango na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba.

 

Mradi huo ambao unajengwa katika Wilaya ya Kondoa, iliyoko jijini Dodoma unatekelezwa na kampuni ya Moladi Construction, ambapo katika ukaguzi huo Mtendaji huyo, alionesha kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa na kukamilisha ujenzi kwa kuzingatia matakwa ya mkataba na maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa.

“Najua mradi huu unatakiwa kuisha Machi 2025 lakini nitashukuru sana kama mtaweza kumaliza mwishoni mwa Januari 2025, lengo ni moja bila kuharibu ubora, ubora ubaki vilevile lakini likiisha mapema nitashukuru sana lazima tukiri tuna changamoto kubwa na wakandarasi wengi, sasa imetokea kwamba miradi mingi ambayo tumempa Moradi ndiyo ambayo inafanya vizuri, sasa ningetamani tukisimama mbele ya watu tukasema kampuni ya Moradi inafanya vizuri tuwe na mifano halisi…

“Sasa mkiweza kukazana likaisha 31 Januari, 2025 itakuwa na faida nyingi kwani wananchi wa Haubi wamesubiri hili jengo kwa muda mrefu sana,”alisema Prof.Ole Gabriel.

 

Aidha Mtendaji Mkuu  huyo  aliwahimiza wakandarasi kuzingatia kalenda ya shughuli zilizopangwa kufanyika kwa kipindi cha utekelezaji wa mkataba huo wa ujenzi.

Aliongeza pia anatamani tutume ujumbe kwa wengine kwamba inawezekana kumaliza mapema jengo letu hilo na lazima tujivunie pale ambapo panawezekana ili tunaposhindwa ijulikane pia imeshindikana kwa sababu ambazo  ni za msingi. Hivyo pale panapo wezekana tuweze kujivunia na wakandarasi wetu kama inavyosisitizwa na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kila wakati kwamba wapeni kipaumbele wazawa. 

Alisisitiza kwamba vifaa vyote viwepo tayari na muda wowote katika eneo la mradi ikiwa ni pamoja na mpangilio wa nguvu kazi iliyopo ili kukidhi kalenda ya matukio ya ujenzi wa jengo hilo unakamilika kama ambavyo ilivyokusudiwa.

Kwa upande wao wakandarasi hao kutoka Ogm na Moladi walimshukuru Mtendaji  huyo  kwa kuwatembelea na kushukuru kwa kupewa fursa ya kufanya hiyo kazi na wanaahidi kuifanya kadri ya uwezo wao usiku na mchana ili kuweza kutimiza lengo ambalo lililokubaliwa.

 

 

1.    

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.Elisante  Ole Gabriel (aliyevaa miwani kulia) akisalimiana na wajumbe mbalimbali wanaosimamia mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Haubi mara baada ya kuwasili katika eneo hilo la ujenzi Wilayani Kondoa, jijini Dodoma.

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel (aliyeshika kitabu) akisaini kitabu cha wageni katika eneo la mradi huo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel (alievaa kofia na miwani) akipokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi kutoka kwa Mhandisi wa kampuni ya Moladi. (ambaye hayupo pichani).

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel akipanda moja ya  ngazi za jengo hilo akiendelea na ukaguzi.

  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel (katikati) na Naibu Msajili  wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Upendo. Ngitiri(kulia) pamoja na wahandisi wengine wakiendelea na shughuli za ukaguzi kwenye mradi huo.

  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Mahakama aliombatana nao pamoja na wahandisi wa mradi huo. katika eneo la mradi huo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni