Ijumaa, 13 Desemba 2024

TAWJA KIGOMA YAKEMEA VIKALI VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa Kigoma Mhe. Aristida Tarimo, ambaye ni Kiongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) mkoani Kigoma ameongoza wanachama wake kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mkoani humo tangu tarehe 04 Desemba 2024 hadi tarehe 10 Desemba, 2024.

Akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari, Mhe. Tarimo alisisitiza kuwa ukatili kwa Mkoa wa Kigoma unakuwa kwa kasi ambapo jamii inapaswa kuungana na kupaza sauti ya kupinga na kutokomeza ukatili kwa watoto na wanawake  katika ngazi ya familia.

Hata hivyo,  Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo alisema yapo mambo mengi yanayochangia ukatili ikiwemo ushirikina, tamaa ya mali na mmomonyoko wa maadili unaoanzia katika ngazi ya familia huku akisisitiza kuwa, ukatili  unakwamisha ndoto za watoto na Taifa kupoteza nguvu kazi na hatimaye kuwa Taifa lenye maadili yasiyompendeza Mungu na wanadamu.

“Naomba jamii isikie sauti hii ya wanawake Majaji na Mahakimu tunaopaza sauti kukemea sana vitendo hivi vya ukatili katika familia na jamii yetu kwa ujumla inayoleta sitofahamu ya maisha ya watoto wetu,” alisema Mhe. Tarimo.

Aidha, aliongeza kwa kutoa rai kwa wanafunzi hao wa Shule za Sekondari na Msingi kupenda kusomea tasnia ya Sheria ili wawe Mahakimu na Majaji wa baadaye watakaokemea ukatili unaofanywa na ndugu na jamaa katika familia.

Kwa upande wake Afisa wa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma, Bi. Epheta Msiga, alisema kuwa jamii ya watu wa Kigoma wanafanya ukatili kwa kasi maana matukio ya ukatili yanaongezeka kwa kasi kubwa na ya kutisha hivyo ni vyema jamii ikaliona hilo kuwa ni janga ambalo lazima kuungana kukemea na kutoa taarifa sahihi kwa mamlaka zilizopo ili kuwashughulikia kisheria wahusika wote wa ukatili ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa mjibu wa sheria ili kukomesha vitendo vya kikatili katika jamii.

Aidha, Afisa wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Tanzania, Bi. Ashura Hamis, alisema jamii inao wajibu wa kutoa taarifa sahihi za ukatili wa aina yoyote katika jamii na familia zetu kwa ujumla maana kufanya hivyo ni kusaidia Jeshi la Polisi kukusanya taarifa sahihi za tukio na mhanga kuweza kupata matibabu akiwa tayari amefanyiwa uchunguzi wa kipolisi kupitia daktari pamoja watu wa ustawi wa jamii. 

“Aidha Jeshi la Polisi linawataka wanafamilia kuwa makini na watu wanaobaki na watoto pamoja na kuchunguza nyendo zao kwani hao watu wa karibu wanachangia sana kufanya ukatili kwa watoto wetu,” alisema Bi. Ashura.

Aliongeza kuwa, dawati la jinsia na watoto mkoani Kigoma lipo wazi kupokea mtu yoyote aliefanyiwa ukatili wa aina yoyote na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mhusika wa ukatili huo na kwamba dawati linaomba ushirikiano wa wadau pamoja na wahanga pamoja na familia zao ili mhusika aweze kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania zinazozuia uakatili katika jamii yetu.

Elimu ilitolewa katika shule za Msingi na Sekondari zipatazo nne zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma hata hivyo walitoa elimu kwa njia ya Redio ya TBC na Redio Joy Kigoma ili kuufikia umma mkubwa wa watanzania.

Aidha, katika kutimiza jukumu hilo la kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili katika maendeleo ya jamii zetu na Nchi kwa ujumla wake Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), walishirikiana na wadau wa kupinga ukatili ambao ni pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Mhe. Eva Mushi, Mhe. Anna Kahungu, Mhe. Vestina Nombo na Florence Ikorongo  pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma, Afisa Dawati la Jinsia na Watoto na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akisisitiza jambo wakati wa kutoa elimu kwa umma juu ya ukatili wa kijinsia na watoto kupitia Redio Joy mkoani Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wa Afisa wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Bi. Ashura Hassan (wa pili kushoto), Mwakilishi wa Kitengo cha Habari wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Aidan W. Robert na wakwanza (wa kwanza kushoto), wawili kulia ni Waandishi wa Habari wa Redio Joy ya mkoani Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Eva B. Mushi (wa kwanza kushoto), Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma Mhe. Anna Kahungu (wa kwanza kulia) na Mtangazaji wa TBC Taifa Redio Kigoma, Bw. Abdulatif (wa pili kushoto).

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Eva Mushi (kushoto) na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Ujiji, Mhe. Vestina Nombo, wakiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu wa Shule ya Sekondari Mwananchi Kigoma mara baada ya kumaliza kutoa elimu ya ukatili.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Anna Kahungu (aliyesimama wa pili kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Mwandiga, Mhe. Florence Ikolongo (wa tatu kushoto) ambao pia ni Wanachama wa TAWJA wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kigoma Mpya mara baada ya kutoa elimu ya ukatili.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni