Jumamosi, 18 Januari 2025

JAJI KIONGOZI ASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA KUZUIA NA KUPAMBANA NA UHALIFU

 Na Salum Tawani - Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani jana tarehe 17 Januari, 2025 alishiriki katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini na kusisitiza ushirikiano katika kuzuia na kupambana na uhalifu wa aina hiyo kwa Taasisi zote zinazohusika.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Bandari jijini Dar es Salaam, Mhe Dkt. Siyani alisema anaishukuru Tume hiyo kwa kuishirikisha Mahakama katika kila hatua ya kuandaa mkakati huo kuanzia hatua za mwanzo na sasa katika utekelezaji wake, kwani Mahakama imekuwa sehemu ya maboresho ambayo Serikali inaendelea kuchukua hatua.

“Ifahamike kuwa wajibu mkubwa wa Mahakama na jukumu lake kikatiba ni kutoa haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 A ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara 107 B inasema katika kutimimiza majukumu yake Mahakama itapaswa kuwa huru,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.

Mhe. Dkt. Siyani alisema, Mahakama huwa inapata kazi baada ya matukio ya aina hiyo kuwa yamefanyika ama kutokea, maana kazi ya Mahakama ni kutoa haki kwa hiyo, makosa yakifanyika na wanaodhaniwa au kushukiwa kufanya makosa wanapo bainika na kufikishwa mahakamani. Hivyo Mahakama inakuwa na wajibu wa kupima ikiwa waliofikishwa mbele ya Mahakama wamefanya makosa hayo kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.

Wajibu huo wa Mahakama unaweza usionekane moja kwa moja wakati wa kazi ya kupambana na kuzuia uhalifu huo, kwahiyo unaweza kuiona picha ya jinsi gani kazi za Mahakama zinaweza kusaidia kuzuia uhalifu wakati tukio limeshatokea.

Vilevile, Mhe. Dkt. Siyani alisema,  kwa sasa ili Mahakama isaidie kuzuia uhalifu kuna mambo kadhaa yanapaswa yafanyike kwa mfano, imani kwa umma juu ya Mahakama ni lazima iwe kubwa, umma ungependa kuona waliyofanaya makosa na kupatikana na hatia wanahukumiwa kwa haraka kwa mujibu wa sheria, mambo haya mawili yakitokea umma utakuwa na imani na Mahakama.

“Mashauri ya aina hiyo yanapochukua muda mrefu mpaka umma ukasahau matukio yaliyotokea umma unaweza poteza imani na Mahakama, sasa ili wahalifu waliopatikana na makosa hayo wahukumiwe kwa haraka na kwa mujibu wa sheria. Mahakama inapaswa kushirikiana na vyombo vingine vinavyohusika kuharakisha mchakato wa uendeshaji wa mashauri hayo ili Mahakama yenyewe iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo”, amesema Jaji Siyani.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani alisema kuwa, ili Mahakama iweze kuzuia uhalifu ni lazima pia ilinde haki za binadamu katika kutimiza majukumu yake bila kuathiri imani ya wananchi kwa Mahakama. Lakini pia ili Mahakama itoe mchango wake ni lazima iwe na mifumo ya kuratibu mashauri hayo, uzalishaji wa taarifa muhimu na ubadilishanaji wa taarifa za waalifu na uhalifu wenyewe kati yake na Taasisi nyingine za haki jinai.

“Makosa sita yaliyoonekana kuwasilishwa kwa wingi mahakamani kwa mwaka 2023 na 2024 ni usalama barabarani, ubakaji, madawa ya kulevya, mauaji, uhamiaji haramu pamoja na ukatli wa kijinsia na pia kuna matukio ya uhalifu mpya wa wizi wa kimtandao ambao umeibua mbinu mpya za kosa la wizi, hata hivyo makosa ya zamani yanatumia mbinu mpya ni kama usafirishaji haramu wa binadamu’’, aliongeza Mhe. Dkt. Siyani.

Kwa upande wa madawa ya kulevya na ujangili Mhe. Dkt. Siyani alisema, wahalifu wamekuwa wakibuni njia mpya tofauti na zamani wahalifu walikuwa wakisafirisha pembe za ndovu kama zilivyo lakini kwa sasa wahalifu hao wana mashine za kusaga, wanasaga zile pembe vizuri na ukikutana nao utafikiri wamebeba unga wa sembe kumbe wanasafirisha unga wa pembe za ndovu, vilevile hata madawa ya kulevya wahalifu hawamezi kete tumboni kama ilivyozoeleka hilo linavyoonyesha mbinu mpya zinazobuniwa kila wakati na wahalifu.

“Mahakama inatoa mafunzo katika maeneo mapya ya kiuhalifu mfano, makosa ya kimtandao, utakatishaji wa fedha na kwenye maeneo mengine ya uhalifu wa kijinai. Vilevile Mahakama imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau, Taasisi za Serikali na Taasisi za kimataifa kwa ajili kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Majaji na Mahakimu na kubadilishana uzoefu, tunatengeneza miongozo mbalimabli ili kukabiliana na mahitaji mapya kwa mfano muongozo wa utoaji wa adhabu wa mwaka 2023 na pia Mahakama inakamilisha miongozo mingine ya adhabu ipatayo 59 na ndani yake ikuhusisha makosa ya wizi, kugushi na uharibifu wa miundombinu ya reli,” alisema Jaji Siyani.

Naye, Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho,  Prof. Sifune Ernest Mchome alisema kuwa, ni wakati sasa wa kushirikiana na kupeana taarifa zinazoashiria dalili za uhalifu ili kuweza kuzizuia zisitokee, kwa upande wa Mahakama kuna taarifa nyingi ambazo tukipeana mapema zinaweza kusaidia kuzuia uhalifu usiweze tokea na kwasababu baadhi ya mifumo inasomana ni wakati sahihi kupata tarifa hizi mapema ili kuweka mikakati iliyo bora ili kuzuia makoa ya kiuhalifu yasitokee na hivyo kupelekea jamii kuishi kwa utulivu na amani.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiwasilisha mada kwenye kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika jana  tarehe 17 Januari, 2025 Jijini Dar es Salaam.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya (kushoto) wakisikiliza kwa makini hoja zilizokuwa ziktolewa katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika  Jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya Wadau mbalimbali walishiriki katika  kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam wakimsikiliza kwa makini Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani hayupo pichani wakati akitoa wasilisho lake wakati wa kikao hicho.

Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho  Profesa Sifune Ernest Mchome (wa kwanza kushoto) akielezea jambo akiwa na wadau wengine katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini kilichofanyika  Jijini Dar es Salaam.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania Mhe. Desderi Kamugisha akisikiliza kwa makini hoja zilizokuwa zikiwakilishwa katika kikao Kazi cha Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kutambua na Kuzuia Uhalifu nchini na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Dkt. Jovine Bishanga.

(Picha na Tawani Salum - Mahakama.)

Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni