Jumanne, 21 Januari 2025

TAASISI 45 KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA MOROGORO MAADHIMISHO WIKI YA SHERIA

 Na EVELINA ODEMBA – Mahakama Morogoro

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Steven Magoiga amesema kuwa jumla ya wadau 45 kutoka Taasisi mbalimbali wamethibitisha kushirikiana na Mahakama kutoa elimu ya sheria katika kipindi cha Wiki ya Sheria mkoani Morogoro kwa mwaka 2025.

Mhe. Magoiga aliyasema hayo jana tarehe 20 Januari, 2025 alipokuwa anazungumza na Vyombo vya Habari na kutoa picha halisi ya namna ambavyo Mahakama imejiandaa kwenye maadhimisho hayo yanayotegemewa kufunguliwa tarehe 25 Januari, 2025.

‘Napenda kuwajulisha kwamba kwa mwaka huu tumeongeza kituo cha utoaji wa huduma za elimu ya sheria katika viwanja vya standi ya treni ya mwendo kasi ya Jakaya Mrisho Kikwete (SGR). Kituo hiki pia kitahusisha Wadau wetu wote na watoa huduma wa TRC. Hadi sasa Wadau 45 wamethibitisha kushiriki,” alisema.

Miongoni mwa Wadau watakaoshiriki ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Wakili Mkuu wa Serikali,TAWJA, Ustawi, Huduma za Uangalizi, RITA, Uhamiaji, TCB, NHIF, PSSF, NMB na CRDB.

Akizungumzia kuhusu ufunguzi, Mhe. Magoiga alisema Kanda ya Morogoro itazindua Wiki ya Sheria kwa maandamano yatakayoanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kuelekea stendi ya zamani ya daladala iliyoko mjini Morogoro.

Alieleza kuwa katika maandamano hayo kutakuwa na washiriki zaidi ya 1,000, wakiwemo Askali wa Jeshi la Wananchi toka Shule ya Mafunzo na Huduma Pangawe, Askari Polisi, Askari Magereza, Vikundi mbalimbali vya mchakamchaka (Jogging Clubs), pamoja na watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro.

Aidha, Mhe. Magoiga aliongeza kuwa Kanda ya Morogoro pamoja na Wilaya zake ambazo ni Mvomero, Gairo, Ulanga, Malinyi, Kilombero, wataadhimisha Wiki ya Sheria katika Wilaya zao, hivyo aliwaomba Viongozi wa Serikali katika Wilaya hizo kutoa ushirikiano kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa miaka mingine.

Wakati huo huo, Mdau kutoka Huduma za Uangalizi Mkoa wa Morogoro, Bw. Yusuph Ponela alisema kuwa tayari wamejipanga na wanasubiria uzinduzi ili waingie kuelimisha Wananchi waweze kujua masuala mbalimbali yanayohusu huduma za uangalizi na namna wanavyoshirikiana na Mahakama kuifikia dira ya Taifa ya Maendeleo kwa kusimamia adhabu mbadala na wafungwa wanapata muda wa kutumikia vifungo vyao, huku wakipata nafasi ya kushiriki shughuli zao za uzalishaji mali.

Naye Mdau kutoka Mamlama ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Chacha Gotora alisema kuwa katika maadhimisho hayo ya Wiki ya Sheria wamejipanga kutoa elimu ya sheria za kodi, kupokea changamoto wanazopata Wananchi kulingana na sheria za kodi na watapata wasaa wa kupatiwa ufafanuzi.

Wiki ya Sheria itahitimishwa tarehe 1 Februari, 2025 ikifuatiwa na maadhimisho ya Siku ya Sheria tarehe 3 Februari, 2025. Matukio hayo yanaafungua shughuli za Mahakama rasmi kwa mwaka 2025 kwa kutoa dira kamili. Maadhimisho hayo yanabebwa na Kauli Mbiu inayosema, “Tanzania ya Miaka 50: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga akizungumza Waandishi wa Habari (hawapo pichani).

Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni (kulia) pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo, wakifuatilia hotoba ya Mhe. Magoiga kwa Vyombo vya Habari.

Maafisa Utumishi toka Mahakama Kanda Morogoro wakifuatilia mkutano huo.

Waandishi wa Habari toka Vyombo mbalimbali (juu na chini) wakifuatilia hotuba ya Kaimu Jaji Mfawidhi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni