Ijumaa, 28 Machi 2025

WATUMISHI KANDA YA SUMBAWANGA WAPEWA ELIMU KUHUSU UGONJWA WA MPOX

Na Fredrick Mahava- Mahakama, Sumbawanga

Watumishi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga wamepata mafunzo juu  ugonjwa wa  Mpox  ili kuwajengea uwezo na njia sahihi za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo baada ya Serikali kutoa taarifa juu ya uwepo wa ugongwa huo nchini.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Manyanda jana tarehe 27 Machi, 2025 na yalifanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mhe. Manyanda alisema kwa kuwa taarifa ya Serikali kuhusu uwepo wa ugonjwa huo nchini haikusema wagonjwa wamegundulika sehemu gani kama watumishi wa Mahakama shughuli za utoaji haki zimekuwa na mwingiliano mkubwa sana na watu hivyo ni lazima tahadhali ichukuliwe na kuwaita wataalamu wa afya waje kutoa elimu namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Aidha, Mtaalum wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Maingu Matoke alitoa elimu kwa watumishi wa Mahakama kuhusu historia ya ugonjwa huo wa mpox tangu umegunduliwa, jinsi ugonjwa huo unavyonea, dalili zake, matibabu yake, watu gani wapo hatarini kuambukizwa, namna ya kujikinga na ugonjwa huo na pia alitoa takwimu za ugonjwa huo kwa Mkoa wa Rukwa.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba aliwaomba watumishi kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia elimu iliyotolewa na mtaalamu wa afya hasa namna ya kujikinga na ugonjwa huo wa Mpox.

Wakati wa mafunzo hayo, watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga walipata wasaa wa kuuliza maswali kwa mtaalamu wa afya na kupewa majibu ambayo yaliwasidia kuelewa zaidi kuhusu ugonjwa wa Mpox.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Manyanda akifungua Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama Kanda hiyo kuhusu Ugonjwa wa Mpox.

Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa ya Rukwa Dkt. Maingu Matoke akitoa Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama, Kanda ya Sumbawanga.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba akizungumza wakati wa Mafunzo hayo.

(Habari Hii Imehariri na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni