Na AHMED MBILINYI, Mahakama-Bukoba
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Bukoba, Mhe. Immakulata Banzi hivi karibuni aliongoza Kikao cha Baraza la
Wafanyakazi la Kanda kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji na utumishi.
Akiwakaribisha wajumbe katika kikao hicho, Mhe. Banzi aliwaomba kuwa huru kuchangia na kutoa maoni mazuri yatakayolisaidia Baraza hilo kufikia maazimio yenye tija siyo tu watumishi wa Kanda hiyo bali pia wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
“Niwashukuru wajumbe kwa kuhudhuria kwenye Kikao cha Baraza hili, ushiriki wenu ni muhimu sana kwani michango ya mawazo mtakayotoa itasaidia kufikia maazimio yenye tija yatakayopelekwa kwenye Baraza Kuu siyo kwa manufaa yetu sisi bali pia watumishi wa Mahakama kwa ujumla,” alisema Mhe. Banzi.
Wakati wa Baraza hilo, wajumbe walijadili masuala mbalimbali yakiwemo mapitio ya bajeti, ukomo wa bajeti, utekelezaji wa bajeti, changamoto za utekelezaji wa bajeti, kupokea na kujadili hoja za watumishi na pia majibu na ufafanuzi ulitolewa na viongozi mbalimbali.
Kadhalika Mhe. Banzi alisisitiza kwa watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, ushirikiano kwa watumishi na wadau wa mahakama, na kuwakumbusha kujiendeleza kielimu katika taaluma zao pamoja na matumizi ya TEHAMA.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi Waandamizi wa Mahakama hiyo akiwemo, Naibu
Msajili Mahakama Kanda ya Bukoba, Mhe. Saidi Mkasiwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko, wajumbe kutoka wilaya zote za Mkoa wa
Kagera.
Wajumbe wengine ni Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Kagera, Bw. Edward Mwashitanda aliyeelezea faida za kutumia Mabaraza ya Wafanyakazi katika kutatua changamoto za watumishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni