Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Twaha Mpembenwe amesema kuwa, maboresho
ya Mahakama ya Tanzania yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika yana mchango
mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Mhe. Mpembenwe ameyasema hayo
leo tarehe 23 Mei, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati wa Semina iliyotolewa kwa wajumbe
(Wabunge) wa Kamati hiyo ya kujifunza kuhusu maboresho mbalimbali ya Mahakama nchini.
“Wakati
mwingine mtu anaweza akafikiria kuwa, unaamua kesi mambo yanaisha hapana sisi
kama Bunge Kamati ya Bajeti tunaangalia sana ni jinsi gani kwa namna moja au
nyingine Mahakama kama Mhimili unaojitegemea mbali ya kutoa haki kwa wananchi
lakini vilevile unakwenda kuchochea katika suala zima la ukuaji wa uchumi na
hiki ndicho kitu ambacho tumekuja kukiona kwa ukubwa zaidi,” amesema Mhe. Mpembenwe.
Amesema kwamba, Kamati
hiyo inaelewa kwamba mashauri yanaposikilizwa kwa wakati na haki inapokuwa
imetendeka ina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuokoa muda ambapo amesema kuwa,
muda ni sehemu muhimu katika kukuza uchumi wa nchi.
Amesema kwamba, ana imani kuwa
mbeleni zaidi, mashauri yatakavyoendelea kusikilizwa na kutolewa uamuzi kwa
muda mfupi itaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ameongeza kwa kupongeza uongozi
wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu kwa maboresho ya miundombinu ya
majengo ambayo Mahakama imejenga na inaendelea kujenga, huku akitoa mfano wa
Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania kutumika kama kivutio cha utalii.
Amesema kuwa, Jengo la Makao
makuu ya Mahakama ni utajiri katika nchi katika kuchochea uchumi kwa kuwa watu
mbalimbali wanaokuja kujifunza wanachangia kukuza uchumi kupitia hoteli
wanazofikia, chakula wanachokula na kadhalika.
“Napenda nikupongeze
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Ole na uongozi mzima kwa maboresho
ambayo yanaendelea kufanyika ndani ya Mahakama, ni matarajio ya Kamati yetu na
Bunge kwa ujumla kuona mambo makubwa na mazuri zaidi kuendelea kupatikana ndani
ya Mhimili huu,” amesisitiza Mhe. Mpembenwe.
Amebainisha kuwa, kufuatia
matunda mazuri ya Mahakama, waliona ni vema kuongeza bajeti ya Mhimili huo kwa
mwaka ujao wa fedha 2025/2026 kiasi cha Tshs. 321 bilioni.
Akiwasilisha mada kuhusu Maboresho
ya Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameishukuru Kamati ya Bajeti na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano wa karibu ulioiwezesha Mahakama kupata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli za Mahakama kutokana na matumizi
ya teknolojia.
Prof. Ole Gabriel
amewaeleza Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuwa, Mahakama
imefanikiwa kuanzisha mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa
Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (JoT e-CMS); Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri
Mwenendo wa Mashauri (TTS); Mfumo wa Takwimu (Data Hub); Mfumo wa taarifa za
Hukumu na Sheria Tanzania (TAnzLII); na mingine.
“Kadhalika Mahakama
imefanikiwa kuendelea kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani kutoka asilimia
10 mwaka 2020 hadi asilimia 4 mwaka 2025,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Ameongeza kuwa, Mhimili
huo umefanikiwa pia kusogeza huduma karibu na wananachi kupitia ujenzi wa
majengo na Mahakama zinazotembea sambamba na kuongezeka kwa imani ya wananchi
kwa Mahakama asilimia 88 kulingana na utafiti uliofanywa na REPOA.
Aidha, Mtendaji Mkuu amewaeleza
wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, kwa siku za mbeleni Mhimili huo umejipanga kuanzisha
utoaji huduma ya usikilizaji mashauri katika maji kupitia maboti, Mahakama
zinazotembea na hata kwenye helikopta (Floating, Mobile & Flying Court).
Kadhalika amesema kuwa, Mahakam imejipanga kuharakisha utatuzi wa mashauri ya kawaida na mkakati wa kumaliza mashauri ya muda mrefu (Backlog); kuimarisha Ukaguzi na Usimamizi wa shughuli za Mahakama, kuendelea na ujenzi wa Mahakama.
“Tumejipanga pia kuendelea kutekeleza Mpango
wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Mahakama, kuboresha Mifumo na matumizi ya
TEHAMA, kuongeza ushirikiano na wadau wa haki jinai na kuimarisha maendeleo ya rasilimaliwatu,
mafunzo na nidhamu,” amesisitiza.
Kamati hiyo imetembelea na
kuelimishwa kuhusu Chumba cha Kusimamia na Kuratibu Huduma za Teknolojia ya
Habari na Mawasilisho (TEHAMA) cha Mahakama ya Tanzania, Ofisi za Huduma kwa Mteja
(Call Centre), Chumba cha Watoto na cha kunyonyeshea pamoja na ukumbi wa
Mahakama (Court room).
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Twaha Mpembenwe akizungumza jambo leo tarehe 23 Mei, 2025 wakati wa Semina ya kujifunza maboresho ya Mahakama kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilipotembelea Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada kuhusu Maboresho ya Mahakama kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati kamati ilipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 23 Mei, 2025.
Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja baadhi ya watumishi wa Mahakama wakifuatilia wasilisho lililokuwa likitolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 23 Mei, 2025 katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda, Bw. Leonard Magacha (kushoto) akimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti yeye pamoja na wenzake walipowasilisha katika viunga vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 23 Mei, 2025 kwa lengo la kujifunza maboresho ya Mahakama ya Tanzania.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakioneshwa sehemu mbalimbali za Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania walipotembelea leo tarehe 23 Mei, 2025 kwa lengo la kujifunza maboresho ya Mahakama ya Tanzania.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika Chumba cha Watoto na cha Kunyonyeshea walipotembelea Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania ili kujifunza kuhusu maboresho ya Mhimili huo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (kulia) akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti miundombinu ya TEHAMA iliyosimikwa katika moja ya chumba cha Mahakama kilichopo katika Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akizungumza jambo na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Dkt. Charles Kimei (kulia). Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.
Picha ya pamoja kati ya Viongozi wa Mahakama na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti leo tarehe 23 Mei, 2025.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni