- Hakimu Mkazi Mfawidhi Kigoma atoa maoni ya uboreshaji wa huduma za Bodi hiyo
- Bodi yaahidi kuzingatia maoni na kuboresha huduma
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma Mhe Aristrida Tarimo amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria nchini ikiwa ni ziara maalum ya bodi hiyo kukutana na wadau wa haki na watoa huduma za msaada wa kisheria Mkoani Kigoma.
Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 24 Septemba 2025 ilikuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na kupata mrejesho wa masuala mbalimbali yanayohusu huduma za msaada wa kisheria.
Katika ziara hiyo wajumbe wa bodi walipokea maoni, mapendekezo na
ushauri kutoka kwa Mhe. Tarimo kuhusu namna bora ya kuimarisha upatikanaji wa
msaada wa kisheria, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa sera na sheria
zitakazowezesha wananchi wengi zaidi kupata haki kwa urahisi, mapema na bila
kujali hali zao za kiuchumi.
Aidha, Mhe. Tarimo alishauri pia kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya
sheria zinazokinzana, ambazo huleta utata katika utekelezaji wake katika
mnyororo wa haki.
Sambamba na hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru
Bodi hiyo kupitia kwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kwa namna
ilivyoshirikiana na Mahakama kutoa huduma za kisheria wakati Wiki ya Sheria
nchini 2025 mkoani Kigoma.
Hata hivyo, aliisitiza kuwa, “kampeni hiyo iendelee na kushirikiana na
wadau wote wa haki, aidha ianzishwe Ofisi
ya Msaada wa Sheria katika Wilaya na Mkoa na waajiriwe Wanasheria wenye uwezo
wa kumwakilisha mwananchi asiye na uwezo wa kifedha kupata uwakilishi wa Wakili
Mahakamani ili kupunguza migogoro na kuongeza uelewa wa
sheria kwa wananchi na kuleta tija katika mnyororo wa haki.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria
nchini, Bw. Saulo Malauri alishukuru kupata maoni hayo
na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha huduma ya msaada wa kisheria kwa
wananchi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma Mhe Aristrida Tarimo (aliyeketi mbele) akipokea ujumbe kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria Bi. Ester Msambazi wa Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria (kulia), wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Saulo Malauri pamoja na wajumbe wengine kutoka Bodi hiyo.
Sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria wakitambulishwa walipomtembelea Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristrida Tarimo (hayupo katika picha) tarehe 24 Septemba, 2025.
Wajumbe wa bodi ya msaada wa kisheria wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristrida Tarimo walipomtembelea tarehe 24 Septemba, 2025. 
Picha ya pamoja kati ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristrida Tarimo (katikati) pamoja na wajumbe wa Bodi ya Kitaifa ya Ushauri na Msaada wa Kisheria. (wa pili kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Saulo Malauri na kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Bi. Ester Msambazi na wajumbe wengine wa Bodi hiyo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni