Ijumaa, 26 Septemba 2025

JAJI MFAWIDHI KANDA YA MUSOMA AFANYA UKAGUZI WA GEREZA LA WILAYA TARIME

  • Asisitiza utekelezaji maelekezo ya Jaji Mkuu Mahakama za Mwanzo kuhusu Mahabusu gerezani

NA KANDANA LUCAS- MAHAKAMA KUU MUSOMA.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya hivi karibuni, amefanya ukaguzi wa Gereza la Wilaya ya Tarime ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa robo ya III mwaka 2025.

Akiongea na Mahabusu na Wafungwa wa Gereza hilo, Jaji Mtulya alieleza lengo la ziara hiyo ni kuwapa fursa kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi na Viongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Wadau wake ambao ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, Uhamiaji na Mawakili wa Kujitegemea.

‘Lengo la kutembelea Gereza hili ni kusikiliza changamoto za Mahabusu na Wafungwa wote ili sisi Mahakama ya Tanzania Kanda ya Musoma tuweze kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wetu ambao tumeambatana nao,” Jaji Mtulya alieleza.

Pamoja na kusikiliza kero mbalimbali na kuzitolea majibu, Jaji Mtulya pia aliwasisitiza Mahakimu wote kuendelea kutekeleza maagizo ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kuhusu kutokuwa na Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo magerezani.

Ukaguzi wa Gereza la Wilaya Tarime ulitanguliwa na Ukaguzi wa Mahakama za Wilaya Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime Mahakama za Mwanzo Robanda- Serengeti, Nyamwaga-Tarime pamoja na Magereza ya Wilaya Bunda, Gereza la Kilimo na Mifugo Tabora B- Serengeti na Mugumu Serengeti.

Jaji Mfawidhi aliwakilishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Mshasha kwenye ukaguzi wa maeneo hayo na aliambatana na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi.

Akiwa kwenye ukaguzi huo, Mhe Mshasha aliwahimiza watumishi kufanya kazi kwa nidhamu, kuzingatia maadili, kusimamia vyema utaratibu wa upokeaji na ushughulikiaji wa malalamiko, kutokuwa na mashauri ya mlundikano, kudumisha ushirikiano na umoja katika vituo vya kazi.

Ukaguzi huo ulianza tarehe 17 Septemba 2025 hadi 23 Septemba 2025 ambapo Mahakama nyingine zaidi zilizokaguliwa ni Mahakama ya Wilaya Tarime, Mahakama ya Mwanzo Tarime, Mahakama ya Wilaya Rorya, Mahakama ya Mwanzo Ingri-Rorya, Mahakama ya Mwanzo Nyaburongo- Rorya, Mahakama ya Wilaya Musoma, Mahakama ya Mwanzo Mukendo, Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Gereza la Wilaya Musoma.

 









Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kulia) akiwa na Kaimu Mkuu wa Gereza la Wilaya Tarime, SSP Sebastian Dioniz (kushoto) nje ya Gereza hilo wakati wa ukaguzi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa na Mahakimu na wadau mbalimbali wa Mahakama baada ya ukaguzi wa Gereza la Wilaya Tarime.

Naibu Msajili Mhe. Salome Mshasha (katikati) akiwa na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi (kulia), Mkuu wa Gereza la Wilaya Bunda Fredrick Mpokwa (kushoto) pamoja na watumishi wa Mahakama na wadau wengine wa Mahakama (mstari wa nyuma).

Uzio wa Mahakama ya Mwanzo Robanda- Serengeti ambao ni miongoni mwa miradi iliyokaguliwa na Naibu Msajili na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma wakimwakilisha Jaji Mfawidhi.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi akisikiliza maelezo ya Mhandisi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama na Magereza iliyofanyika hivi karibuni.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Mshasha (katikati) akiwa na Mtendaji, Mahakimu na wadau wa Mahakama baada ya ukaguzi wa Gereza la Mahabusu na Wafungwa Mugumu-Serengeti.

Naibu Msajili Mhe. Salome Msasha (mwenye ushungi) akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Rorya wakati wa ziara ya ukaguzi uliofanyika hivi karibuni.

Habari hii imehaririwa  na  FAUSTINE KPM-Mahaka, Dodoma

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni