- Asisitiza utekelezaji maelekezo ya Jaji Mkuu Mahakama za Mwanzo kuhusu Mahabusu gerezani
NA KANDANA LUCAS- MAHAKAMA KUU MUSOMA.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya hivi karibuni, amefanya
ukaguzi wa Gereza la Wilaya ya Tarime ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa robo ya III
mwaka 2025.
Akiongea na Mahabusu na Wafungwa
wa Gereza hilo, Jaji Mtulya alieleza lengo la ziara hiyo ni kuwapa fursa kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi
na Viongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Wadau wake ambao ni Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka, Polisi, Uhamiaji na Mawakili wa Kujitegemea.
‘Lengo la kutembelea Gereza hili ni kusikiliza
changamoto za Mahabusu na Wafungwa wote ili sisi Mahakama ya Tanzania Kanda ya
Musoma tuweze kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wetu ambao tumeambatana
nao,” Jaji Mtulya alieleza.
Pamoja na kusikiliza kero mbalimbali na kuzitolea
majibu, Jaji Mtulya pia aliwasisitiza Mahakimu wote kuendelea kutekeleza
maagizo ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kuhusu
kutokuwa na Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo magerezani.
Ukaguzi wa Gereza la Wilaya Tarime ulitanguliwa na
Ukaguzi wa Mahakama za Wilaya Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime Mahakama za
Mwanzo Robanda- Serengeti, Nyamwaga-Tarime pamoja na Magereza ya Wilaya Bunda,
Gereza la Kilimo na Mifugo Tabora B- Serengeti na Mugumu Serengeti.
Jaji Mfawidhi aliwakilishwa na Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Mshasha kwenye ukaguzi wa maeneo hayo
na aliambatana na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi.
Akiwa kwenye ukaguzi huo, Mhe Mshasha aliwahimiza
watumishi kufanya kazi kwa nidhamu, kuzingatia maadili, kusimamia vyema
utaratibu wa upokeaji na ushughulikiaji wa malalamiko, kutokuwa na mashauri ya
mlundikano, kudumisha ushirikiano na umoja katika vituo vya kazi.
Ukaguzi huo ulianza tarehe 17 Septemba 2025 hadi 23
Septemba 2025 ambapo Mahakama nyingine zaidi zilizokaguliwa ni Mahakama ya Wilaya
Tarime, Mahakama ya Mwanzo Tarime, Mahakama ya Wilaya Rorya, Mahakama ya Mwanzo
Ingri-Rorya, Mahakama ya Mwanzo Nyaburongo- Rorya, Mahakama ya Wilaya Musoma,
Mahakama ya Mwanzo Mukendo, Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Hakimu
Mkazi Musoma na Gereza la Wilaya Musoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa na Mahakimu na wadau mbalimbali wa
Mahakama baada ya ukaguzi wa Gereza la Wilaya Tarime.
Naibu Msajili Mhe. Salome Mshasha (katikati) akiwa na
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi (kulia), Mkuu wa Gereza
la Wilaya Bunda Fredrick Mpokwa (kushoto) pamoja na watumishi wa Mahakama na
wadau wengine wa Mahakama (mstari wa nyuma).
Uzio wa Mahakama ya Mwanzo Robanda- Serengeti ambao ni
miongoni mwa miradi iliyokaguliwa na Naibu Msajili na Mtendaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Musoma wakimwakilisha Jaji Mfawidhi.
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi
akisikiliza maelezo ya Mhandisi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mugumu
Mjini wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama na Magereza iliyofanyika hivi
karibuni.Naibu Msajili Mhe. Salome Msasha (mwenye ushungi)
akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Rorya wakati wa ziara ya
ukaguzi uliofanyika hivi karibuni.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KPM-Mahakam , Dodoma



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni