Ijumaa, 26 Septemba 2025

MUSOMA YAFANYA UKAGUZI WA GEREZA LA WILAYA TARIME

   .Asisitiza utekelezaji wa Maelekezo ya Mhe. Jaji Mkuu kuhusu Mahakama za  Mwanzo kutokuwa na Mahabusu gerezani

Na. Kandana Lucas- Mahakama, Musoma

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu H. Mtulya hivi karibuni, amefanya ukaguzi wa Gereza la Wilaya ya Tarime ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa robo ya tatu ya mwaka 2025.

Akiongea na Mahabusu na Wafungwa wa Gereza hilo Mhe. Mtulya alieleza lengo la ziara hiyo ni kuwapa fursa wafungwa na mahabusu kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi na viongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na wadau wake ambao ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, Uhamiaji na Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea.

“Lengo la kutembelea gereza hili ni kusikiliza changamoto za Mahabusu na Wafungwa wote ili sisi Mahakama ya Tanzania kanda ya Musoma, tuweze kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wetu ambao tumeambatana nao,” alisema Jaji Mtulya.

Pamoja na kusikiliza kero mbalimbali na kuzitolea majibu, Jaji Mtulya pia aliwasisitiza Mahakimu wote kuendelea kutekeleza maagizo ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju kuhusu kutokuwa na Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo Magerezani.

Vilevile ukaguzi wa Gereza la Wilaya Tarime, ulitanguliwa na Ukaguzi wa Mahakama za Wilaya Butiama, Bunda, Serengeti na Tarime pamoja na Mahakama za Mwanzo Robanda Serengeti, Nyamwaga Tarime.

Vilevile Magereza ya Wilaya Bunda, Gereza la Kilimo na Mifugo Tabora B Serengeti na Mugumu Serengeti ambapo Jaji Mfawidhi aliwakilishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Mhe. Salome Abbubakar Mshasha, aliyeambatana na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Leonard John Maufi.

Akimwakilisha Jaji Mfawidhi katika Mahakama alizotembelea, Mhe Mshasha aliwahimiza watumishi kufanya kazi kwa nidhamu, kuzingatia maadili, kusimamia vyema utaratibu wa upokeaji na ushughulikiwaji wa malalamiko, kutokuwa na mashauri ya mlundikano, kudumisha ushirikiano na umoja katika vituo vya kazi.

Ukaguzi huo ulianza tarehe 17 Septemba 2025 hadi 23 Septemba 2025 ambapo Mahakama nyingine zaidi zilizokaguliwa ni Mahakama ya Wilaya Tarime, Mahakama ya Mwanzo Tarime, Mahakama ya Wilaya Rorya, Mahakama ya Mwanzo Ingri-Rorya, Mahakama ya Mwanzo Nyaburongo- Rorya, Mahakama ya Wilaya Musoma, Mahakama ya Mwanzo Mukendo, Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Gereza la Wilaya Musoma.

Jaji Mfawidhi Mhe. Fahamu H. Mtulya (Katikati) akiwa na Mahakimu na wadau mbalimbali wa Mahakama baada ya ukaguzi wa Gereza la Wilaya Tarime.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma Mhe. Salome A. Mshasha (Katikati) akiwa na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Leonard J. Maufi (kulia), Mkuu wa Gereza la Wilaya Bunda Fredrick Mpokwa (kushoto) pamoja na watumishi wa Mahakama na wadau wengine wa Mahakama (mstari wa nyuma).

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Leonard John Maufi akisikiliza maelezo ya Mhandisi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama na Magereza iliyofanyika hivi karibuni.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Mhe. Salome A. Mshasha (Katikati) akiwa na Mtendaji Mahakimu na wadau wa Mahakama baada ya ukaguzi wa Gereza la Mahabusu na Wafungwa Bunda

Uzio wa Mahakama ya Mwanzo Robanda- Serengeti ambao ni miongoni mwa miradi iliyokaguliwa na Naibu Msajili na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma wakimwakilisha Jaji Mfawidhi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu H. Mtulya (kulia), akiwa na Kaimu Mkuu wa Gereza la Wilaya Tarime SSP Sebastian A. Dioniz (kushoto) nje ya Gereza hilo wakati wa ukaguzi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni