Ijumaa, 26 Septemba 2025

BODI YA KITAIFA YA USHAURI NA MSAADA WA KISHERIA WAKUTANA HAKIMU MKAZI MFAWIDHI KIGOMA

  •  Hakimu Mkazi Mfawidhi Kigoma atoa maoni ya uboreshaji wa huduma za Bodi hiyo
  • Bodi yaahidi kuzingatia maoni na kuboresha huduma

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma Mhe Aristrida Tarimo amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria nchini ikiwa ni ziara maalum ya bodi hiyo kukutana na wadau wa haki na watoa huduma za msaada wa kisheria Mkoani Kigoma.

Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 24 Septemba 2025 ilikuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na kupata mrejesho wa masuala mbalimbali yanayohusu huduma za msaada wa kisheria.

Katika ziara hiyo wajumbe wa bodi walipokea maoni, mapendekezo na ushauri kutoka kwa Mhe. Tarimo kuhusu namna bora ya kuimarisha upatikanaji wa msaada wa kisheria, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa sera na sheria zitakazowezesha wananchi wengi zaidi kupata haki kwa urahisi, mapema na bila kujali hali zao za kiuchumi.

Aidha, Mhe. Tarimo alishauri pia kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria zinazokinzana, ambazo huleta utata katika utekelezaji wake katika mnyororo wa haki.

Sambamba na hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Bodi hiyo kupitia kwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kwa namna ilivyoshirikiana na Mahakama kutoa huduma za kisheria wakati Wiki ya Sheria nchini 2025 mkoani Kigoma.

Hata hivyo, aliisitiza kuwa, “kampeni hiyo iendelee na kushirikiana na wadau wote wa haki, aidha  ianzishwe Ofisi ya Msaada wa Sheria katika Wilaya na Mkoa na waajiriwe Wanasheria wenye uwezo wa kumwakilisha mwananchi asiye na uwezo wa kifedha kupata uwakilishi wa Wakili Mahakamani  ili  kupunguza migogoro na kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi na kuleta tija katika mnyororo wa haki.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria nchini, Bw. Saulo Malauri alishukuru kupata maoni hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma Mhe Aristrida Tarimo (aliyeketi mbele) akipokea ujumbe kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria Bi. Ester Msambazi wa Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria (kulia), wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Saulo Malauri pamoja na wajumbe wengine kutoka Bodi hiyo.

Sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Kisheria wakitambulishwa walipomtembelea Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristrida Tarimo (hayupo katika picha) tarehe 24 Septemba, 2025.

Wajumbe wa bodi ya msaada wa kisheria wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristrida Tarimo walipomtembelea tarehe 24 Septemba, 2025. 

Picha ya pamoja kati ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Aristrida Tarimo (katikati) pamoja na wajumbe wa Bodi ya Kitaifa ya Ushauri na Msaada wa Kisheria. (wa pili kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Saulo Malauri na kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Bi. Ester Msambazi na wajumbe wengine wa Bodi hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni