Ijumaa, 26 Septemba 2025

JAJI KIREKIANO AFANYA ZIARA MAHAKAMA KIBAHA, AWAPONGEZA WATUMISHI KWA UTENDAJI KAZI MZURI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Anorld Kirekiano amewapongeza watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha kwa kazi nzuri wanazozifanya  katika kutekeleza wajibu wao. 

Mhe. Kirekiano alitoa pongezi hizo tarehe 24 Septemba, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha alipokuwa  akizungumza na watumishi hao baada ya ziara ya ukaguzi wa robo ya mwaka aliyofanya katika Mahakama hiyo. 

Wakati wa ziara hiyo Jaji Kirekiano alipokea taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha, ambayo pamoja na mambo mengine iliainisha changamoto zinazowakabili watumishi wa Mahakama hizo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kirekiano alisema kupitia ukaguzi wake amepata kujua kinachoendelea kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya pamoja na taarifa zilizopo Kanda ya Dar es Salaam, alisema kuwa, ameridhika na huduma zinazotolewa licha ya kuwa na changamoto bado watumishi wa Mahakama hizo hawajaacha kutoa huduma bora kwa wateja wa Mahakama.

Aidha, Jaji huyo alieleza kwamba, kumekuwa na jitihada za kila wakati za kuboresha mifumo ya utendaji kazi ili kurahisisha utendaji kazi na si kuwasumbua watumishi, hivyo basi aliwataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi na kuwatia  moyo wafanye kazi kwa weledi.

“Kazi zinafanyika vizuri, tunajua pia zinaweza kufanywa kwa uzuri zaidi ila ukaguzi ni kwa ajili ya kupata picha halisi,” alisisitiza Mhe. Kirekiano.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo aliwapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri pia kwenye mapungufu wameelekeza na kutoa rai yafanyiwe kazi.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe Joyce Mkhoi aliwashukuru viongozi hao na kusema ukaguzi huo unawasaidia kwa kuwa unawatoa sehemu moja na kwenda sehemu nyingine na kuahidi kuwa hoja zilizoibuka watazifanyia kazi.

Nao Viongozi pamoja na watumishi walitoa shukrani kwa uongozi wa Mahakama kwa kuzidi kuzingatia maslahi ya watumishi na kuzidi kuboresha mazingira katika sehemu ya kazi.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Mhe. Kirekiano aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo, Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Sheyla Biletwa pamoja na Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Farida Sufiani.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Anorld Kirekiano (katikati) akiwa katika picha ya pamoja baada ya ziara ya ziara ya ukaguzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya na Kibaha Pwani. Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha- Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama wa Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai, wa kwanza kulia ni  Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani,  Bw. Nestory Mujunangoma. Waliosimama nyuma kushoto ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Sheyla Biletwa na kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Farida Sufiani. 


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo (aliyesimama) akimkaribisha Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Anord Kirekiano (katikati) ili azungumze na watumishi na wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani alipofanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama hizo tarehe 24 Septemba, 2025. Aliyeketi kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha Kibaha Pwani wakimsikiliza Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Anorld Kirekiano (hayupo katika picha) alipofanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama hizo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni