Alhamisi, 11 Septemba 2025

MAJAJI, WADAU HAKI JINAI UHIFADHI WANYAMAPORI WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha

Kikao Kazi kilichowaleta pamoja Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Wadau wa Haki Jinai kwenye uhifadhi wa Wanyamapori kilichokuwa kinafanyika jijini hapa kimehitimishwa leo tarehe 11 Septemba, 2025 kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire.

Washiriki wa Kikao Kazi hicho waliwasili katika lango kuu la kuingilia kwenye Hifadhi hiyo majira ya saa 4.30 asubuhi na kupokelewa na Naibu Kamishna kutoka Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA), Afande Steria Ndaga kwa kushirikiana na Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Afande Beatrice Kessy.

Baada ya kupata maelezo mafupi kuhusu Hifadhi hiyo, ambayo ni ya tatu kati ya 21 kuingiza fedha nyingi za Watalii katika pato la Taifa, Majaji na Wadau wa Haki Jinai hao walianza safari kuzungukia maeneo mbalimbali ya Hifadhi hiyo.

Wakiwa katika Hifadhi hiyo, washiriki wa Kikao Kazi hicho wamejionea maajabu ya Dunia na utajiri ambao Tanzania inajivunia ikiwemo wanyama pori, ndege, misitu ya kupendeza pamoja na urithi wa maliasili iliyopo nchini kwenye Hifadhihiyo.

Wajumbe hao wamefanikiwa kuwaona baadhi ya wanyama maarufu duniani wanaofahamika kama Big-5 wanaopatikana kwa urahisi katika Hifadhi hiyo kama Tembo na Nyati na wanyama wengine kama Twiga, swala, pundamilia, mbuni na ndege wa aina mablimbali wakiwemo Korongo.

Wadau hao wameonesha kufurahishwa na utalii huo na wamefarijika kujionea kwa macho wanyama wanaowaona kwa picha kwenye vitabu na runinga.

Utalii huo wa ndani kwenye Hifadhi hiyo umeandaliwa na TANAPA kama sehemu ya Kikao Kazi hicho kilichokuwa kinafanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru ambacho Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi ilikuwa Mratibu Mkuu.

Tembo akinyonyesha mtoto wake, huku wengine wakishuhudia. Picha chini ni Tembo wengine wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire. Picha ya tatu kwa mbali tembo wanaonekana wakinywa maji kwenye Mto Tarangire.


Mfalme wa nyika, Simba akiwa amejipumzisha baada ya kushiba kupitiliza.

Twiga mnyama anayejua kunesa wakati anakatisha mitaa.

Kundi la Nyati likisaka malisho.

Pundamilia, mnyama anayevutia kwa macho kuliko wote.

Kundi la Nyumbu.

Swala haoo, njoo Tarangire wapo wa kutosha.

Wenyeji katika Hifadhi hiyo wakitoa maelezo mafupi kabla ya kuwakaribisha wageni kuanza utalii huo wa ndani.

Picha ya pamoja baada ya kupata ukaribisho kabla ya kuanza kutalii kwenye Hifadhi ya Tarangire.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni