Alhamisi, 11 Septemba 2025

WATUMISHI WA MAHAKAMA KANDA YA TABORA WAFANYA UTALII WA NDANI SERENGETI

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora wamefanya ziara ya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara kwa lengo la kujifunza, kuhamasisha utalii wa ndani na kuongeza mshikamano baina ya watumishi wa kada mbalimbali ndani ya Mahakama.

Ziara hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania Tawi la Tabora (TMJA) ilifanyika kuanzia tarehe 04 hadi 07 Septemba, 2025 na ilihusisha ushiriki wa Mahakimu, Maafisa wa Mahakama pamoja na watumishi wengine wa kada mbalimbali kutoka Mahakama Kuu na Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya.

Katika ziara hiyo, watumishi walitembelea Kambi maarufu ya Seronera iliyopo katikati ya Mbuga ya Serengeti, ambapo walipata fursa ya kujionea moja kwa moja wanyamapori kama Simba, Tembo, Twiga, Pundamilia, Nyumbu, Fisi, Viboko na aina mbalimbali za ndege kama Korongo, Tai na ndege wa rangi tofauti tofauti.

 Aidha, walishuhudia mandhari ya kuvutia ya mbuga hiyo pamoja na kuelezwa mchakato wa uhamaji maarufu wa nyumbu (wildebeest migration) ambapo wanyama hao huenda Kenya huvutia watalii wengi kutoka kona mbalimbali za dunia.

Uhamaji wa Nyumbu ni moja ya matukio makubwa, ya kipekee na ya kuvutia sana duniani yanayohusisha uhamaji wa mamilioni ya wanyama hususan Nyumbu, Pundamilia na Swala wakihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa msimu, wakitafuta malisho mabichi na maji.

Imebainishwa kuwa, safari hiyo ya kipekee huanza mwishoni mwa mwaka hadi mapema mwaka mpya (Desemba–Machi) katika Kusini mwa Serengeti ambapo Nyumbu huzalia kwa wingi, kisha huendelea kuelekea Kaskazini kupitia maeneo ya kati na Magharibi ya Serengeti (Aprili–Mei) na kufikia Maasai Mara (Juni–Oktoba) ambapo hushuhudiwa tukio maarufu la kuvuka Mto Mara huku wakikumbana na hatari za Mamba na wanyama wakali.

Aidha, mvua zinapoanza Novemba, hurejea Serengeti na kuanza mzunguko upya. Tukio hili ni moja ya maajabu ya asili ya Afrika na huchangia kwa kiasi kikubwa katika utalii wa ndani na wa kimataifa.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Mhe. Gabriel Ngaeje alisema, "ziara hii imetupa nafasi si tu ya kujifunza kuhusu rasilimali za Taifa letu, bali pia imeimarisha mahusiano baina ya watumishi na kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii. Huu ni mfano bora wa kujumuika katika shughuli za kitaifa na kijamii nje ya ofisi.”

Watumishi walioshiriki katika utalii huo walikiri kufurahishwa na safari hiyo, huku wakisema kuwa, uzoefu walioupata umewapa muamko mpya kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kuhifadhi wanyamapori.

Kadhalika, walieleza kwamba, utalii wa ndani unapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa ni njia mojawapo ya kusaidia kukuza uchumi wa Taifa na kuhamasisha uzalendo.

Tembo akiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, inaelezwa kuwa mnyama huyu mkubwa zaidi wa nchi kavu na anaweza kufikia uzito wa kilo 6,000 hadi 7,000 ni urithi wa asili wa Tanzania. Watumishi wa Mahakama Kanda ya Tabora wamejionea ukubwa wake mubashara wakiwa katika hifadhi hiyo.

Simba ni mojawapo ya wanyama waliovuta hisia za wengi akiwa anatembea huku akitazamwa kwa tahadhari na mshangao na washiriki kutoka Mahakama Kanda ya Tabora.

Muundo wa mistari ya pundamilia si tu wa kuvutia, bali hufanya kazi ya kipekee ya kujikinga na wadudu na joto. Uzuri na mvuto wake ni hadithi ya isioelezeka mojawapo ya fahari za Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo Watumishi kutoka Mahakama Kanda ya Tabora wamebahatika kutembelea.

Nyumbu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni miongoni mwa wanyama wachache wanaoshiriki katika uhamaji mkubwa zaidi duniani,  wakisafiri zaidi ya kilomita 1,000 kila mwaka kwa kutafuta malisho bora. 

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja katika Daraja la Igongo-Busisi lililopo jijini Mwanza. Daraja hilo sio tu njia ya kuvuka bali pia ni sehemu ya utalii na kujivunia kuhusu Tanzania.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni