Alhamisi, 11 Septemba 2025

MAJENGO MATATU YA MAHAKAMA ZA MWANZO LINDI YAKABIDHIWA

Na. Hilary Lorry – Mahakama, Lindi

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Godfrey Mbeyela amekabidhiwa majengo matatu ya Mahakama za Mwanzo ambazo ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Ndomoni iliyopo Wilaya ya Nachingwea, Mahakama ya Mwanzo Mipingo iliyopo Wilaya ya Lindi na Mahakama ya Mwanzo Mtandi iliyopo Wilaya ya Kilwa zote zikiwa Mkoa wa Lindi.

Makabidhiano hayo yalifanyika kwa siku mbili kati ya tarehe 8 na 9 Septemba 2025 ambapo tarehe 08 Septemba 2025 Mtendaji huyo alikabidhiwa Mahakama ya Mwanzo Ndomoni iliyopo wilaya ya Nachingwea na tarehe 9 Septemba 2025 alikabidhiwa Mahakama za mwanzo Mipingo iliyopo Wilaya ya Lindi na  Mahakama ya  Mwanzo Mtandi iliyopo wilaya ya Kilwa.

Aidha, zoezi la makabadhiano ya majengo hayo matutu ya Mahakama za Mwanzo yamefanyika kati ya kampuni ya Uandisi ya Engineering Plus ambao ni wajenzi wa majengo hayo chini ya Mhandisi mshauri kutoka kampuni ya Norman na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.

Akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano hayo Mtendaji Mbeyela aliipongeza kampuni ya Engineering Plus kwa kufanya kazi hiyo ya ujenzi kwa weledi na ufanisi mkubwa.

“Nimpongeza Mhandisi Mshauri na jopo lake kutoka kampuni ya Norman kwa usimamizi mzuri wa mradi huku akiwasisitiza kuendelea kufuatilia majengo hayo kwa ukaribu wakati wote ambapo majengo hayo yapo katika muda wa uangalizi (probation period),” aliongeza Mtendaji huyo.

Kwa upande, Mkadiriaji Majenzi Bw. Abdallah Nalicho kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania aliwataka kampuni ya Engineering plus kutoa mafunzo juu ya mifumo mbalimbali ikiwemo mifumo ya umeme, mifumo ya TEHAMA, Mifumo ya kuzuia na kudhibiti moto na mifumo mingine yote ndani ya siku kumi na nne (14) tangia kukabidhiwa miradi hiyo.lengo ni kuwafanya watumiaji wawe na uelewa mzuri wa namna bora ya matumizi ya mifumo hiyo.

“Niwashauri watuamiaji kuripoti dosari zozote zitakazojitokeza kwa haraka hasa wakati huu ambapo majengo haya yapo chini ya uangalizi ili mkandarasi ajuzwe na kuweza kurekebisha kasoro zozote zitakazojitokeza na akimtaka mhandisi mshauri kushiriki katika kusimamia marekebisho yoyote yatakayojitokeza kwani bado ni jukumu lako kwa kipindi hiki cha uangalizi,” alisema Bw. Nalicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mhandisi kutoka kampuni ya Engineering plus Bw. Silas Paul na Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Norman Bw. Beno Batinamani waliupongeza Uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote jambo ambalo limefanya majengo hayo matatu ya mahakama za Mwanzo kukamilika katika ubora uliokusudiwa.

“Jambo moja la kutilia mkazo kwa watumiaji ni kuongeza umakini katika kutunza vifaa vyote vilivyowekwa kwenya Mahakama hizo ili viweze kuleta tija iliyokusudiwa na kutomuingiza yeye katika hasara ya manunuzi ya vifaa vingine hasa wakati huu ambapo majengo yapo chini ya uangalizi,” alisisitiza Mhandisi huyo.

Jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Mipingo iliyopo Wilaya ya Lindi linavyoonekana kwa sasa.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Mbeyela akipokea hati ya makabidhiano ya majengo ya Mahakama za Mwanzo kutoka kwa Mkandarasi Mhandisi Silas Paul.

Jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Ndomoni iliyopo Wilaya ya Nachingwea linavyoonekana kwa sasa.




Wajumbe wa kamati ya Makabidhiano wakiangalia jinsi kamera za ulinzi(CCTV CAMERA) zinavyofanya kazi wakati wa ukaguzi wa Mahakama ya Mwanzo Mipingo.




Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Nachingwea  Mhe.Neema Mhelela akiangalia kangavuke lililopo katika Mahakama ya Mwanzo Ndomoni.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni