Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Kikao Kazi kilichowaleta
pamoja Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Wadau wa Haki Jinai kwenye
uhifadhi wa Wanyamapori kilichokuwa kinafanyika jijini hapa kimehitimishwa leo
tarehe 11 Septemba, 2025 kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire.
Washiriki wa Kikao Kazi
hicho waliwasili katika lango kuu la kuingilia kwenye Hifadhi hiyo majira ya
saa 4.30 asubuhi na kupokelewa na Naibu Kamishna kutoka Shirika la Hifadhi ya
Taifa (TANAPA), Afande Steria Ndaga kwa kushirikiana na Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi, Afande Beatrice Kessy.
Baada ya kupata maelezo
mafupi kuhusu Hifadhi hiyo, ambayo ni ya tatu kati ya 21 kuingiza fedha nyingi
za Watalii katika pato la Taifa, Majaji na Wadau wa Haki Jinai hao walianza
safari kuzungukia maeneo mbalimbali ya Hifadhi hiyo.
Wakiwa katika Hifadhi
hiyo, washiriki wa Kikao Kazi hicho wamejionea maajabu ya Dunia na utajiri
ambao Tanzania inajivunia ikiwemo wanyama pori, ndege, misitu ya kupendeza
pamoja na urithi wa maliasili iliyopo nchini kwenye Hifadhihiyo.
Wajumbe hao wamefanikiwa
kuwaona baadhi ya wanyama maarufu duniani wanaofahamika kama Big-5
wanaopatikana kwa urahisi katika Hifadhi hiyo kama Tembo na Nyati na wanyama
wengine kama Twiga, swala, pundamilia, mbuni na ndege wa aina mablimbali
wakiwemo Korongo.
Wadau hao wameonesha
kufurahishwa na utalii huo na wamefarijika kujionea kwa macho wanyama
wanaowaona kwa picha kwenye vitabu na runinga.
Utalii huo wa ndani kwenye Hifadhi hiyo umeandaliwa na TANAPA kama sehemu ya Kikao Kazi hicho kilichokuwa kinafanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru ambacho Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi ilikuwa Mratibu Mkuu.
Kundi la Nyati likisaka malisho.
Pundamilia, mnyama anayevutia kwa macho kuliko wote.
Kundi la Nyumbu.
Swala haoo, njoo Tarangire wapo wa kutosha.
Wenyeji katika Hifadhi hiyo wakitoa maelezo mafupi kabla ya kuwakaribisha wageni kuanza utalii huo wa ndani.
Picha ya pamoja baada ya kupata ukaribisho kabla ya kuanza kutalii kwenye Hifadhi ya Tarangire.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni