Jumatano, 10 Septemba 2025

MAPATO YA UTALII TANZANIA YAPAA

  • Yafika zaidi ya bilioni 400
  • Watalii waongezeka mwaka hadi mwaka

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha

Idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali Tanzania imeongezeka kutoka 786,710 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia 1,493,135 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuchangia zaidi ya 499bn/- kwenye pato la Taifa.

Hayo yamebainishwa na Kamishna Msaidi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa [TANAPA], Bi. July Lyimo alipokuwa anawasilsha mada kwenye Kikao Kazi cha Wadau wa Haki Jinai kwenye uhifadhi wa Wanyamapori kinachofanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru jijini hapa.

Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017, watalii hao 786,710 waliingizia Taifa jumla ya Shilingi za Kitanzania milioni 187,889,184,373, huku mapato hayo yakiongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia Shilingi za Kitanzania milioni 499,895,848,371/95 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

‘Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ukusanyaji wa mapato ulikuwa 410,665,187,391/96 na makadirio ya mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yalikuwa 430,556,220,982/99, lakini mapato yaliyopatikana yalikuwa 499,075,308,953/63. Makadirio ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni 600,181,999,994,’ amesema.

Bi Lyimo amebainisha pia kuwa mapato hayo yamepatikana kutokana na vivutio mbalimbali, huku Mbuga ya Serengeti ikiongoza kwa asilimia 53.47, ikifuatiwa na Mlima Kilimanjaro wenye asilimia 20.80 na mbuga ya Tarangire ikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 11.90.

Vivutio vingine na namna vilivyochangia mapato kwa asilimia kwenye mabano ni Lake Manyara [4.10], Nyerere [2.79], Arusha [2.10], Mikumi [1.97], Ruaha [1.10], Saadani [0.50], Mkomazi [0.27] na hifadhi nyingine [1].

Bi Lyimo amesema TANAPA wanamikakati mbalimbali ambayo itasaidia kuvutia watalii na kuongeza mapato, ikiwemo kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara za utalii na viwanja vya ndege, malazi, malango madaraja na kuboresha malazi ya bei nafuu kwa ajili ya soko la ndani na nje.

Mikakati mingine ni kuvutia wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii ndani ya Hifadhi za Taifa ili kukidhi mahitaji ya watalii wa hadhi zote (malazi, mazao ya utalii) na kutangaza vivutio vya utalii katika masoko ya ndani na nje ya nchi kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwemo maonesho, matamasha, kampeni maalum, mikutano mikubwa, mashuleni, Taasisi mbalimbali, watu maarufu na michezo (Marathon).

Bi Lyimo ametaja mikakati mingine kama kuendelea kubuni mazao mapya ya utalii ili kuweza kuongeza mapato, kuongeza idadi na aina ya Wanyamapori na kufanya upembuzi yakinifu na kubaini hifadhi za kuongeza idadi na aina ya wanyamapori ili kuvutia watalii zaidi katika Hifadhi zenye upungufu.

Kuna aina mbalimbali za vivutio vya utalii Tanzania, ikiwemo aina mbalimbali za Wanyama, Wingi wa Wanyama, upekee wa Wanyama katika eneo, Wanyama wakubwa watano [5], Uhamaji wa Nyumbu kwa kuvuka mto Mara na Grumet) na kuzaa kwa wakati mmoja (Zebra, Thomson Gazell Eland).

Vivutio vingine ni Milima kama Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru, Fukwe za Bahari na Maziwa-Saadani na Maziwa (Tanganyika, Manyara, Momela, Burigi, Victoria], Wanyama adimu na hatarini kutoweka (Mkomazi na Serengeti) na Uwanda wa kuvutia Ndege mbalimbali na Maua.

Kamishna Msaidi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa [TANAPA], Bi. July Lyimo akiwasilisha mada kuhusu mchango wa utalii kwenye uchumi wa nchi katika Kikao Kazi cha Wadau wa Uhifadhi wa Wanyamapori kilichokuwa kinafanyika jijini Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akitoa majumuisho ya mada zilizowasilishwa.

Sehemu ya washiriki kwenye Kikao Kazi [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri


Sehemu nyingine ya washiriki kwenye Kikao Kazi [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.


Sehemu nyingine ya tatu ya washiriki kwenye Kikao Kazi [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.


Sehemu nyingine ya nne ya washiriki kwenye Kikao Kazi [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.




Sehemu nyingine ya tano ya washiriki kwenye Kikao Kazi [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.




Dkt. Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye ubora wake wakati akiwasilisha mada kwenye Kikao Kazi hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akiongoza jopo jingine la majadiliano ya mada mbalimbali.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu Kikao Kazi hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni