Jumamosi, 6 Septemba 2025

MWAJABU BWIRE WA MAHAKAMA SPORTS ANG'ARA MBIO ZA BAISKELI SHIMIWI MWANZA

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Mwanza

Mwendesha baiskeli machachali wa Timu ya Mahakama ya Tanzania-Mahakama Sports, Bi Mwajabu Bwire ameibuka kidedea kwenye mchezo wa mbio za baiskeli wanawake  katika mashindao ya Michezo ya 39 ya Shirikisho la Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) yanayofanyika jijini Mwanza.

Akizungumza baada ya mashindano hayo leo tarehe 06 Septemba, 2025, Bi. Mwajabu amesema alianza kushiriki mashindano hayo SHIMIWI mwaka jana Morogoro na kushika nafasi ya nne kutokana na kutokuwa na vifaa vya mchezo huo lakini mwaka huu Mahakama imemuwezesha vitendea kazi na mazoezi mazuri ndio yamechangia kuleta matokeo hayo.

"Nasikia furaha sana kwa kupata nafasi ya kwanza na kumshinda bingwa mtetezi wa mchezo huu mwaka jana vifaa vilikuwa hakuna ndio maana sikuweza kufanikiwa," amesema Mwanamichezo huyo.

Bi. Mwajabu Bwire ameshinda mbio hizo za Kilometa 30 akitumia saa moja na dakika nane, kwa upande wa wanaume Mahakama imeshika nafasi ya nne baada ya Mwakilishi Gerald Robert kufanikiwa kupata nafasi hiyo. 

Amesema pia, alianzia namba nne akaja mbili na leo hii amekuwa mshindi namba moja. Amechukua fursa hiyo kuwashukuru Wana Mahakama Sports kwa kumtia moyo katika mbio hizo na hatimaye kufika katika nafasi hiyo.

Aidha, hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama kutoa mwakilishi upande wa wanaume katika mbio hizo za Baiskeli. Akizungumza na Mwandishi wa Habari hii, Mwakilishi huyo amesema amepata matokeo hayo kutokana na maandalizi hafifu ya mchezo huo na kifaa cha mashindano hayo kutokuwa na viwango bora.

"Ukiangalia mshindi namba moja, mbili na tatu baiskeli zao zilikuwa na viwango tofauti na ya kwangu," amesema Bw. Robert akiongeza kuwa, anajiandaa kwa mwakani akipata vifaa vizuri na mazoezi mazuri atafika nafasi nzuri zaidi.

Naye Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Wilson Dede amesema kwa upande wa wanaume, imekuwa mara ya kwanza kushiriki na mshiriki aliyefanya mazoezi ya mbio hizo alipata ajali akiwa mazoezini na kusababisha majeraha na Daktari kushauri kutoshiriki kutokana na hali yake kutoimarika kiasi cha kuingia katika mashindano hayo kwakuwa Mahakama ina watu wana vipaji vingi, Mwanariadha Gerald Robert aliomba kuingia katika mashindano hayo na kushika nafasi ya nne, ambapo amekiri kuwa ameshika nafasi hiyo kwakuwa hakuwa na maandalizi mazuri na kutokuwa na vifaa vya mchezo huo.

Kadhalika, amesema hii ni mara ya pili kwa Mahakama Sports kutoa washiriki katika mbio za baiskeli katika mashindano hayo na mara ya kwanza mshiriki Bi. Mwajabu Bwire alishika nafasi ya nne.

Mashindano hayo ya mbio za baiskeli yalianzia makaburi ya Mv Bukoba Igoma mpaka Isangijo na kurudi wakati mbio za baiskeli wanaume kilometa 50 yameanzia makaburi ya Mv Bukoba mpaka Nyangune na kurudi.

Mwanamichezo kutoka Timu ya Mahakama ya Tanzania- Mahakama Sports, Bi. Mwajabu Bwire akijiandaa kuanza mashindano ya mbio za baiskeli katika eneo la  Makaburi ya Mv Bukoba Igoma jijini Mwanza leo tarehe 06 Septemba, 2025.

Mwendesha Baiskeli wa Mahakama Sports, Bw. Gerald Robert akiwa katika kinyanganyiro cha ushindi wakati wa mashindano ya mchezo wa mbio za baiskeli.

 

 Mshindi namba moja wa Mbio za Baiskeli -Mashindano ya 39 ya SHIMIWI, Bi. Mwajabu Bwire (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Bw. Nkrumah Katagira na na kulia ni Bw. Peter Machalo.

Upozaji koo baada ya ushindi ukiendelea.....

Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Wilson Dede (kulia) katika picha ya pamoja na Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Peter Machalo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni