Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Kikao Kazi cha Wadau wa
Haki Jinai kwenye uhifadhi wa Wanyamapori kinachofanyika kwenye Hoteli ya Mount
Meru jijini hapa kimeinmgia siku ya pili huku washiriki wakipitishwa kwenye
mada mbalimbali zinazolenga kuimarisha mapambano dhidi ya uharifu wa
Wanyamapori.
Mada zilizowasilishwa
zinahusu Matumizi ya Sayansi katika upatikanaji wa Haki: Jukumu la Sayansi
Jinai ya Biolojia na Vinasaba vya Wanyamapori katika kesi za Uharifu Dhidi ya
Wanyamapori.
Mada hiyo iliwasilishwa
kwa pamoja na Mkemia kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bi. Leticia
Waitara na Wakili Mkuu wa Serikali, Bi Tarsila Gervas.
Katika wasilisho lao,
wawezeshaji hao wamesisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi katika mapambano ya
uharifu wa Wanyamapori hauepukiki kwa sasa, kwani utasaidia kufikia uamuzi
usiokuwa na mawaa.
Wameeleza pia kuwa
matumizi ya Vina Saba [DNA] kwenye matukio ya Wanyamapori yanaweza kuthibiti
changamoto wanazokabiliana nazo kwenye uhifadhi wa Wanyamapori.
Mada nyingine ilihusu Uendeshaji
Mashtaka Kiitelijensia
katika Uhalifu wa Wanyamapori; Kuimarisha Mkakati wa Uchunguzi na Mwitikio wa Kisheria
kwenye Uhalifu wa Wanyamapori, ambayo
iliwasilishwa na Bw. Elisifa Ngowi kutoka PAMS Foundation.
Katika wasilisho lake,
Mzee Ngowi, pamoja na mambo mengine, ameelezea jinsi ya kutumia intelijensia
kwenye upelelezi na umuhimu kwa wapelelezi kuweka kumbukumbu za kiupelelezi
kuanzia kukamatwa kwa mtuhumiwa, ukusanyaji wa vielelezo na ushahidi wote kabla
ya shauri kupelekwa mahakamani.
Mada nyingine ilihusu Wajibu
wa Mahakama katika Ulinzi na Matumizi Endelevu ya Maliasili, ambayo
imewasilishwa na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha.
Katika wasilisho hilo,
Mhe. Mugasha amesisitiza kuwa Mahakama kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ndiyo yenye mamlaka ya mwisho kwenye utoaji wa haki
nchini.
Amesema kuwa mchango wa
Mahakama katika masuala ya uhifadhi wa Wanyamapori ni kutafsiri ipasavyo sheria
zinazohusika ili kuhakikisha yale yote yanayoahidiwa na Serikali yanatekelezwa katika
kulinda maliasili zilizopo.
Mhe. Mugasha ameeleza pia
kuwa Mahakama ya Tanzania imeunda Mahakama maalum inayoshughulikia mashauri ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi, yakiwemo yale yanayohusu uhalifu wa Wanyamapori na
hivi karibuni Jaji Mkuu ametoa mamlaka katika kila Kanda kusikiliza mashauri
kama hayo.
‘Mahakama nchini Tanzania ina jukumu muhimu katika kulinda
na kuhakikisha matumizi endelevu ya maliasili kupitia utekelezaji wa sheria
husika ambayo ni muhimu kwa kulinda urithi wa asili wa nchi na hatimaye kupata
haki kwa asili na kukuza uchumi...
‘Jukumu chanya la Mahakama linaweza kuboreshwa zaidi ikiwa Wadau wengine
watachukua hatua chanya katika uchunguzi wa haraka na madhubuti wa makosa
ambayo ndiyo nguzo ya ufanisi wa mashtaka ya makosa yanayohusiana,’ amesema.
Mada nyingine zilihusu Mchango wa Utalii kwenye Uchumi wa Nchi; Faida na Changamoto, iliyowasilishwa na Kamishana Msaidizi, Bi. July Lyimo kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa [TANAPA]; Kutangaza Utalii kwa Njia ya Akili Unde nchini Tanzania iliyowaslishwa na Dkt. Hellen Maziku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkazo wa Mahali pa Kazi na Utumiaji wa Akili Unde katika ulinzi wa Wanyamapori iliyowasilishwa na Dkt. Garvin Kweka.
Bw. Elisifa Ngowi kutoka PAMS Foundation akiwasilisha mada.
Dkt. Hellen Maziku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwasilisha mada.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni