Ijumaa, 12 Desemba 2025

MCHANGO WA MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA BIASHARA KWENYE UKUAJI UCHUMI, UFANISI KIBIASHARA

  • Yarejesha kwenye mzunguko wa fedha bilioni 11 za Kitanzania kila mwezi

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, imefanikiwa kurejesha kwenye mzunguko wa fedha wastani wa kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 11 kila mwezi kwa mwaka wa 2025.

Hayo yamebainishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, kwenye hotuba iliyowasilishwa kwa niaba yake na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud, kwenye uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Biashara uliofanyika leo tarehe 12 Desemba, 2025 jijini Dar es Salaam.

‘Hizi fedha zinatokana na mashauri ambayo uamuzi wake umekamilika hadi utekelezaji. Ninaposema Mahakama ya Biashara ipo kwa ajili ya kuwezesha miamala ya kibiashara, itekelezwe kwa ufanisi ninamaanisha hiyo. Taarifa za Mahakama hii zinathibitisha eneo la ukuaji wa uchumi na ufanisi wa biashara nchini,’ Mhe. Dkt. Siyani ameeleza kwenye hotuba yake.

Jaji Kiongozi ameeleza kuwa urejeshaji wa kiasi kikibwa cha fedha hizo kwenye mzunguko wa fedha ni tafsiri kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imechangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2025-2050 inayolenga kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kuongeza imani ya wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kwa Mahakama ya Tanzania.

 Ameeleza kuwa anafahamu pia kuwa kuanzia katikati ya mwezi Octoba hadi Novemba, 2025, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ilikuwa na vikao maalum vya usikilizaji mashauri, ambapo jumla ya mashauri ya kibishara yaliyoamuliwa  ni 96 yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania 65,964,979,029/04, Dola za Kimarekani 10,195,592,01 na Euro 172,892.

‘Taarifa nilizozipokea kutoka kwa Jaji Mfawidhi ni kwamba mashauri haya yalisikilizwa kama yalivyopangwa kwa  zaidi ya asilimia 90,’ sehemu ya hotuba ya Jaji Kiongozi inaeleza.

Ameeleza kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imeamua kutoa mwongozo huo kwa kutambua kuwa mashauri ya kibiashara yanapaswa kusikilizwa na kuamriwa mapema ipasavyo na kuzingatia weledi unaoakisi kwa usahihi ujuzi kwenye eneo husika la mgogoro na kwa kutambua kuwa si wengi walio na maarifa sahihi kwenye ushughulikiaji wa mashauri ya kibiashara.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, licha ya mwongozo huo kushughulika na mashauri ya kibiashara, ni imani yake kuwa utanufaisha Wadau wengi, hata kwenye mashauri mengine ya madai kwa kuwa mashauri ya kibiashara ni mashauri ya madai pia.

‘Kwa sababu hiyo, taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kibiashara zinashabihiana na taratibu za uendeshaji wa mashauri mengine ya madai, ingawa kuna tofauti za hapa na pale,’ Mhe. Dkt. Siyani amesema.

Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi amesema kuwa Mwongozo huo utakuwa rejea nzuri kwa vijana waliopo kwenye Shule ya Sheria kwa Vitendo na Vyuo Vikuu kwa mambo mbalimbali wanayojifunza. Kadhalika, Wahadhiri na Watafiti mbalimbali wa ndani na nje ya nchi pia watanufaika na maarifa yaliyomo ndani ya Mwongozo huo.

Akizungumzia chimbuko la Mwongozo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha, ameeleza kuwa pamoja na uboreshaji ambao umefanyika kwenye maeneo mbalimbali, nyenzo na vitendea kazi vilivyopo kwa sasa katika eneo la haki madai haviwezeshi Maofisa Mahakama, Mawakili na Wadau wenye mashauri mahakamani hapo kufanya mambo kwa wepesi.

Amesema kuwa hali hiyo inatokana na upekee wa migogoro ya kibiashara ambao utatuzi wake wakati mwingine unaweza kuhitaji maarifa ya ziada yasiyopatikana kwenye vitendea kazi vilivyopo. Mhe. Mkeha ametaja sababu nyingine ni mabadiliko ya namna njia za ufanyaji biashara zinavyobadilika kwa kasi kutokana na kukua kwa teknolojia ulimwenguni.

Hivyo, Mhe. Mkeha ameishukuru Benki Kuu ya Tanzania, hususan Gavana wa Benki Kuu Emmanuel Tutuba kwa kufanikisha kwa kiasi kikubwa uandishi, uhariri na uzalishaji wan akala 100 za Mwongozo huo.

 Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na kasi itakayowezesha kurudi kwa fedha zinazoshikiliwa, kwa sababu ya uwepo wa mashauri katika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, kwenye mzunguko wa uchumi.

‘Tutafanya hivyo kwa kuharakisha ukazaji wa tuzo tunazozitoa, eneo ambalo Benki imeliwekea pia mkazo katika fedha ambazo imezitoa kwa Divisheni ya Biashara katika mwaka huu wa fedha wa 2025/2026. Kwa kufanya hivyo, Mahakama itakuwa imechangia ukuaji wa uchumi na kuwa kivutio cha uwekezaji nchini,’ amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto [IJA] na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, akiwasilisha neno lake wakati wa uzinduzi huo, amepongeza ushirikiano kati ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara na Benki Kuu, ambao umefanikisha kupatikana kwa Mwongozo huo.

Ameeleza kuwa wao kama Chuo, ambao kazi yao ni kufundisha na kuwajengea weledi na uwezo Majaji na Majaji katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, watautumia Mwongozo huo kama nyenzo ya kufundishia na ameahidi kuenedeleza ushirikiano uliopo kati ya IJA na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwenye eneo la mafunzo.

Uzinduzi wa Mwongozo huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama, Wahadhiri wa Vyuo, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea, Wadau na watumishi wa Divisheni ya Biashara.

Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud, akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, kwenye uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Biashara uliofanyika leo tarehe 12 Desemba, 2025 jijini Dar es Salaam.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha, akieleza kwa kifupi chimbuko la Mwongozo huo.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto [IJA] na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo huo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Joyce Minde akitambulisha wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo.

Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani. Picha chini ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria uzinduzi huo.


Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji na Viongozi Waandamizi wa Mahakama Kuu Divisnehi ya Biashara. Picha chini ni wajumbe wa kamati iliyofanikisha utayarishaji wa Mwongozo huo.


Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama kutoka Makao Makuu Dodoma. Picha chini Wadau waliohudhuria hafla hiyo.


Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama Kuu. Picha chini ni Mawakili na Wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo.


Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara [juu na chini] waliohudhuria uzinduzi huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni