Jumanne, 3 Februari 2026

MAHAKAMA KUU KANDA YA SONGEA YASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA SHERIA NCHINI

Na NOEL SYLIVESTER- Mahakama, Songea

Mahakama ya Tanzania ni muhimili pekee wenye wajibu wa mwisho katika utoaji haki na katika kutekeleza wajibu huo, Mahakama imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ustawi wa maendeleo ya taifa.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe.  James Karayemaha, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kikanda jana tarehe 2 Februari, 2026 kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Songea.

Maendeleo ya Taifa ni mchakato wa kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote wa nchi husika kwa njia endelevu. Yanahusisha maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kuleta ustawi wa Taifa kwa ujumla,’ alisema.

Mhe. Karayemaha alieleza kuwa maendeleo yanaweza kuonekana katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kiuchumi kwenye ongezeko la kipato, ajira, uzalishaji na kuimarika kwa uchumi wa nchi; kijamii katika upatikanaji wa elimu bora, afya, usawa na haki na teknolojia katika matumizi ya sayansi na teknolojia ili kurahisisha maisha.

Maeneo mengine ni kwenye siasa katika uawala bora, amani, usalama, demokrasia na ushiriki wa wananchi; miundombinu kwenye uwepo wa miundombinu mizuri (barabara, umeme, maji) na kiutamaduni katika kuheshimu na kuendeleza mila na tamaduni chanya.

‘Mahakama ya Tanzania imekuwa ikitoa maamuzi ya migogoro mbalimbali kama vile ya uhifadhi wa maliasili, masuala ya kodi, ardhi na mikataba. Katika utatuzi wa migogoro hiyo, Mahakama imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ustawi wa maendeleo ya Taifa letu,’ Jaji Mfawidhi alisema.

Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ikitoa elimu kwa jamii juu ya sheria mbalimbali kupitia maamuzi, vyombo vya habari na kwa njia ya mitandao, hivyo kuleta uelewa wa pamoja katika masuala yote ya kisheria.

Mhe. Mhe. Karayemaha alibainisha kuwa hatua hiyo huchangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria na haki zao, hivyo kujenga jamii inayoheshimu sheria na kusaidia kuleta usawa katika jamii na kila mmoja kutambua wajibu wake katika kukuza ustawi wa maendeleo ya taifa.

‘Katika kutoa haki, Mahakama kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi, imekuwa ikiimarisha amani na utulivu katika jamii, hivyo kusababisha wananchi kujihusisha na shughuli za kiuchumi na za kijamii na kusaidia kukua kwa ustawi wa maendeleo ya Taifa,’ alisema.

Aidha, Jaji Mfawidhi alisema kuwa Mahakama inaendelea kuboresha upatikanaji wa haki kwa kuongeza huduma za Mahakama za Mwanzo karibu na wananchi ili kupunguza umbali, kuhakikisha upatikanaji kwa gharama nafuu na kwa wakati muafaka.

‘Mathalani, katika Kanda yetu ya Songea, Mahakama ipo katika hatua za mwisho za ujenzi wa Mahakama mpya za Mwanzo katika maeneo ya Msamala na Lilondo katika Wilaya ya Songea. Hapo awali wananchi wa maeneo hayo walipaswa kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma za Mahakama. Ujenzi na uanzishaji wa Mahakama za Mwanzo umefanyika katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo kusongeza huduma karibu na wananchi. Lakini pia vituo kama Namasakata, Lukumbule, Magazini, Ligera, Wabaki vilivyokuwa vimefungwa vimefunguliwa na wananchi wa maeneo hayo hawasafiri umbali mrefu kutafuta haki kama ilivyokuwa zamani,’ alisema.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa Viongozi mbalimbali wa Mahakama, Serikali na kidini, akiwepo Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. DKt Emmanuel Kawishe, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bregedia Ahmed Abbas Ahmed, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Sirilius Matupa, Naibu Msajili, Mtendaji, Mahakimu, Wadau na watumishi wa Mahakama kwa ujumla.

Sambamba na maadhimisho hayo, kulikuwepo na burudani iliyotolewa na kwaya ya Mahakama Kuu Kanda ya Songea pamoja na ngoma za asili.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Sirilius Matupa (wa kwanza kushoto), Mhe. DKt. Emmanuel Ludovick Kawishe (wa pili kutoka kushoto), Mhe. James Karayemaha (katikati), Bregedia Ahmed Abbas Ahmed (wa pili kutoka kulia) pamoja na Wakili Mary Makondo, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma (wa kwanza kutoka kulia).

Mhe. Elizabeth Nyembele.

Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Ruvuma Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Egidy Mkolwe.

Mwenyekiti wa TLS Songea, Bw. Eliseus Ndunguru.

Mahakimu na Mawakili.

Wadau wa Mahakama,

Viongozi wa dini (waliosimama).

Kwaya ya Mahakama (waliosimama).


 Wafanyakazi wa Mahakama.Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni