Na Mwaandishi Wetu-Tanga
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, kwa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga yameadhimishwa na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Siasa, Dini, Wadau wa haki na wananchi kwa ujumla kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga.
Kulikuwa na mfululizo wa simulizi za mafanikio, pale mhimili unaotafsiri sheria na kutenda haki, yaani Mahakama, unajiweka wazi namna matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanavyofuta rushwa na ukiritimba kwenye utendaji kazi.
Akizungumza kwenye Maadhimisho hayo jana tarehe 2 Februari, 2026, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule, alisema matumizi ya TEHAMA mahakamani, yanayoendelea kuboreshwa, yanaondoa ulazima wa mteja kuonana ‘uso kwa uso’ na mtoa huduma, hali inayodhibiti vitendo viovu vya baadhi ya watumishi, hasa katika rushwa na ukiritimba.
Alitoa mfano kuwa, kutokana na matumizi ya TEHAMA, muda wa juu wa kusikiliza shauri mkoani Tanga katika Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ni miezi sita, wakati Mahakama ya Mwanzo ni miezi mitatu, hali ambayo awali ilichukua takribani miaka minne.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, alirejea kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema, “mchango wa Mahakama katika Ustawi wa Maendeleo ya Taifa”, na kusema mhimili huo unachangia kustawisha maendeleo kwa kutatua migogoro kwa wakati.
Alisema, hali hiyo inawafanya waadawa kwenye mashauri yao kupata haki kwa wakati, na kuendelea kutekeleza majukumu yao kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Aliahidi kuratibu mpango wa kupata rasilimali zitakazoboresha huduma Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, ikiwemo usikilizaji mashauri kwa njia ya mtandao na kuratibu upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama na ofisi zake, ili kuwafikishia wananchi huduma za kimahakama kwa karibu zaidi.
Mhe. Balozi Dkt Batilda alisema kuwa kufanyika kwa maadhimisho hayo ni ishara ya wazi kwamba Tanzania inatambua na kuheshimu utawala wa sheria, kadri ulivyoakisiwa kwenye Katiba.
Akizungumza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Saidi Johari, Ofisi ya Wakili wa Mkoa wa Tanga, Wakili Rebecca Msalangi, alisema kauli mbiu ya mwaka 2026, inaakisi nafasi ya kipekee ya Mahakama katika kulinda haki, kudumisha amani na kuweka mazingira wezeshi ya kisheria, kimuundo na kitaasisi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Mkoa wa Tanga, Wakili Mary Swai, alisema maadhimisho hayo yanakumbusha kuwa, maendeleo ya Taifa yasingewezekana bila utawala wa sheria na Mahakama huru.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni