Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Wadau wa Haki Jinai wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wamepeana jukumu la kufanya utafiti kuhusu Sheria ya Ushahidi ya Kieletroniki kwa Mahakama za Mwanzo kwakuwa kumekua na sintofahamu wakati mashauri yenye ushahidi wa kielekroniki yanapofikishwa katika Mahakama za Mwanzo kujua kama sheria imekataza ama iko kimya.
Hayo yaliazimiwa katika kikao cha kusukuma mashauri cha Mahakama ya Wilaya Kibaha kilichofanyika tarehe 28 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo.
Wadau hao wamekuwa na sintofahamu wakati mashauri yenye ushahidi wa kielekroniki yanapofikishwa katika Mahakama za Mwanzo na kupitia maamuzi ya mashauri mbalimbali wamegundua kuwa, sheria haijakataza Mahakama za Mwanzo kutopokea mashauri yenye ushahidi wa kielekroniki, na ndipo kufikia maazimio kwamba kila mdau afanye utafiti kusoma sheria na kuitafsiri vizuri na pia kupitia mashauri yaliyoamriwa na Mahakama za juu kuhusiana na sheria hiyo.
Akizungumza wakati wa majadiliano hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa
Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fredrick Shayo alisema Sheria ya Ushahidi wa Kielektroniki
imetokana na shauri ambalo Jaji Massam alizungumzia wakati wa uamuzi wa shauri la
rufaa kutoka Mahakama ya Mwanzo yenye ubishani kuhusu Ushahidi wa Kielekroniki
rufaa namba 3076 ya mwaka 2025 kati ya Hussein Haji Miraji na Isack Elias Kiganga
katika Mahakama Kuu masjala ndogo ya Shinyanga.
Mhe. Massam alisema, “hata hivyo hakuna kifungu katika Sheria ya Ushahidi ya Kielekroniki au Tangazo la Serikali na. 22/1964 inakataza ushahidi wa kielekroniki Mahakama za Mwanzo.”
Katika kikao hicho hoja mbalimbali zilijadiliwa lengo likiwa ni kupata namna bora ya kumaliza mashauri pasipo kuwa na mashauri ya mlundikano.
Akitoa mchango wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Amos Sura alisema kuwa, ni bora mashauri yakasikilizwa siku moja ili kuepuka kubaki na majalada ya washtakiwa walioruka dhamana kwa kuzingatia mwongozo wa Jaji Mkuu wa kuzuia Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo.
Akijibu lalamiko la Mawakili kuchelewesha mashauri kwa kigezo cha kuwa na mashauri Mahakama za juu Wakili Sura amemuomba Hakimu Mkazi Mfawidhi Kibaha na Mahakimu wengine wa Wilaya kutumia Mahakama Mtandao (Virtual Court) ili kuepuka kuchelewesha mashauri na Mawakili ambao wamekuwa wakitumia kisingizio cha kuwa na mashauri Mahakama za juu.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai alisema anatamani ifike kipindi katika vikao hivyo wafike na kupongeza tu, kwakuwa hakuna shida katika usikilizaji mashauri.
Mhe. Lukumai amewataka upande wa Polisi kuwa, wakati wanapopeleka mashauri
ya Mahakama za Mwanzo wanatakiwa wawe na uhakika kuwa mlalamikaji yupo na siku
hiyo hiyo shauri lisikilizwe kwakuwa mashauri ya Mahakama za Mwanzo hayana
ufundi hivyo yanaweza kusikilizwa na kumalizika siku hiyo na kusema kuwa, hatua
hiyo litaepuka washtakiwa kuruka dhamana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Kusukuma Mashauri Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai (kulia) akiwa na Wakili wa Serikali Said Seif Katibu wa kikao hicho kwa pamoja wakiongoza Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wazi uliopo katika Mahakama hiyo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kusukuma Mashauri cha
Mahakama ya Wilaya Kibaha wakiwa katika kikao hicho.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni