Na EVA LESHANGE, Mahakama-Singida
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt. Juliana Masabo
jana tarehe 01 Aprili, 2026 alikabidhi rasmi eneo jipya la kiutawala la
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Singida Kwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe.
Ayoub Mwenda.
Mhe. Dkt. Masabo amempongeza Mhe. Ayoub Mwenda kwa kuaminiwa na Viongozi na kuteuliwa kuwa Jaji wa kwanza kuanzisha Masjala Ndogo ya Singida ambapo alisema kuwa, “ni heshima kubwa na nina imani itakuwa Kanda ya mfano.”
Aidha
ameushukuru uongozi mzima wa Mahakama wa Tanzania kwa mageuzi na uboreshaji wa
miundombinu ya Mahakam ana kusema kuwa, “ujenzi huu wa Mahakama Kuu Masjala
ndogo ya Singida utatatua changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kuja
Singida kwani kutokana na umbali sio watu wote walifanikiwa kuifuata haki
Dodoma.”
Vilevile,
Mhe. Dkt. Masabo aliwashukuru watumishi na viongozi wa Mahakama Mkoa wa Singida
hasa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa
kwa uongozi thabiti muda wote waliofanya kazi kwa kutekeleza majukumu
mbalimbali kwa weledi.”
“Mhe
Allu Nzowa alikuwa kinara katika kuwaelekeza wenzie tulipoanza matumizi ya
mfumo mpya wa Kielektroni wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) na uongozi wake
thabiti katika usikilizwaji wa mashauri, Mkoa wa Singida upo kumi (10) bora
kitaifa,” alisema.
Aidha,
aliwasisitiza watumishi wa Kanda hiyo kwamba, ushirikiano uliopo uendelee hata
kwa viongozi wapya na kusisitiza kuiishi salamu ya Mahakama.
Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda amempongeza sana Mhe. Dkt Juliana Masabo kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chote alichosimamia Mkoa wa Singida kwani ameona mambo mengi mazuri yamefanyika kupitia taarifa alizosomewa siku alipowasili Singida na ameshukuru kwa nyenzo zote za kazi alizokabidhiwa na kuahidi kuendelea kuwa na ushirikiano mzuri na Kanda ya Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (kulia ) akimkabidhi nyaraka na taarifa za utekelezaji Mhe Ayoub Mwenda, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Singida wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Kituo cha Singida iliyofanyika jana tarehe 01 Aprili, 2026.
Viongozi wa Mahakama Kanda ya Dodoma na Singida wakiwa katika picha ya pamoja. Aliyeketi kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda. Waliosimama katikati ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri, wa pili kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Mhe.Evodia Kyaruzi, aliyesimama wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Bw. Filbert Matotay, wa pili kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka na wa kwanza kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu Dodoma, Bw.Bedson Mariba.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt
Juliana Masabo akisisitiza jambo mbele ya
watumishi (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya makabidhiano ya Kituo cha Mahakama Kuu Kanda ya Singida jana tarehe 01 Aprili, 2026.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Singida na watumishi wengine waliohudhuria hafla hiyo kutoka.Wa kwanza kulia Mhe. Fadhili Luvinga, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Singida, akifuatiwa na Mhe. Alisile Mwankejela, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni na Mhe Luzango Khamsini, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Iramba.
Sehemu ya Watumishi waliohunduria hafla hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni