Jumapili, 21 Juni 2026

'MAENDELEO YA TEKNOLOJIA YAMEWEZESHA SHUGHULI NYINGI ZA KIJAMII, KIUCHUMI NA KISHERIA'

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Lumuli Mbuya amesema maendeleo ya Teknolojia yamesababisha shughuli  nyingi za kijamii, kiuchumi na kisheria kufanyika kwa njia kielektroniki.

Mhe. Mbuya aliyasema hayo tarehe 19 Juni, 2026 alipokuwa akitoa mafunzo ya Namna ya Kupokea Ushahidi wa kielekroniki kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya Ilala na Mahakama za Mwanzo za Wilaya hiyo.

Mhe. Mbuya, alisema  mawasiliano ya WhatsApp, sms, baruapepe (email), mitandao ya kijamii, miamala ya fedha kwa simu, picha za kidijitali, video na sauti za kurekodiwa sasa ni sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi na kutokana na hali hiyo, sheria imefanyiwa marekebisho kwa kuongeza kifungu cha 8A katika kanuni za Ushahidi za Mahakama za Mwanzo.

Amesema marekebisho hayo yameondoa shaka iliyokuwepo hapo awali kuhusu uwezo wa Mahakama ya Mwanzo kupokea ushahidi wa kieletroniki na kwamba Mahakama za Mwanzo sasa zina mamlaka kamili ya kupokea, kuchunguza na kutathmini ushahidi huo kwa kuongozwa na kifungu cha 19 cha Sheria ya Miamala ya Kieletroniki na kifungu cha 70 cha Sheria ya Ushahidi.

Akieleza misingi minne ya Sheria ya chini ya Kifungu cha 19(2), Mhe. Mbuya alisema, Sheria ya Miamala ya Kieletroniki inaelekeza Mahakama kuzingatia mambo manne muhimu wakati wa kutathmini ushahidi wa kieletroniki kwamba uaminifu wa namna ya taarifa iliyotengenezwa, kuhifadhiwa au kutumwa.

Ameongeza kuwa, msingi wa pili ni uaminifu wa namna uhalisia wa taarifa iliyohifadhiwa na namna aliyetoa au kuanzisha taarifa (originator) aliyetambulika na nne jambo lolote lingine linaloweza kusaidia Mahakama kuamua uzito wa ushahidi huo.

Amesema kuwa, mambo hayo manne ndiyo msingi mkuu wa kazi ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo katika kutathmini ushahidi wa kielektroniki.

Kadhalika, Naibu Msajili huyo amesema ataandaa mwongozo huo vizuri ili kuwawezesha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kufanya kazi kwa ufanisi na uhakika wa kile wanachokifanya katika kupima na uzito wa ushahidi na kupokea ushahidi wa kieletroniki.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Herrieth Mwailolo aliwashukuru Mahakimu hao kwa kuhudhuria mafunzo hayo.

Akieleza madhumuni ya mafunzo hayo, Mhe. Mwailolo amesema kutokana na Sheria ya Miamala ya kielektoniki kwa Mahakama za Mwanzo wameona vema wapate mafunzo mafupi ili kuongeza ujuzi na pia kwa Mahakama ya Wilaya wamekuwa wakitumia sheria hiyo lakini wameona vema kuwa na uelewa wa pamoja katika mashauri yanayohusu Sheria za Miamala ya Kieletroniki.

“Kwahiyo tumeona umuhimu wa kukaa pamoja na kwamba Mahakama ya Wilaya tumekuwa tukifanya kesi za aina hiyo, lakini kwa namna moja ama nyingine  wakikaa wawili au watatu  huwa jambo linakuwa jema zaidi pengine hata sisi tulikuwa tunakosea kwa majadiliano hayo tutafika mahali wote tutakuwa na uelewa mmoja,” alisema Mhe. Mwailolo.

Naye Ofisa Upelelezi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakili Emmanuel  Cheneko amesema kodi ni sheria, kodi ni madai na kodi ni jinai na kwamba kodi ikiwa madai lazima ianzie kwa Kamshina Mkuu  na pale unapoona hujaridhishwa na maamuzi ya Kamishna Mkuu kwa muktadha wa madai, hatua ya kwanza unatakiwa kwenda kwenye Bodi halafu Baraza la Rufaa la Kodi na mwisho Mahakama ya Rufani.

Bw. Cheneko amesema kuwa, wakati kodi inapokuwa jinai ndipo Mahakama za kawaida zinahusishwa. Amesema katika kesi hizo ushahidi mwingi ni wa kieletroniki.

Akifafanua zaidi amesema, kesi za madai za kodi zinaenda kwenye Mabaraza na Jinai zinaenda kwenye Mahakama za kawaida na malalamiko yanaenda kwenye Baraza la Uchunguzi (Ombudsman).

Wakati huohuo, kulikuwa na kikao kazi kilichofanyika kabla ya mafunzo kuanza ambapo Hakimu Mkazi Mfawidhi aliwapongeza Mahakimu hao kwa kufanya kazi kwa bidii na kusema kuwa, hakuna kesi za mlundikano pamoja na Mahakama za Mwanzo kusajili mashauri kwenye mfumo na kuyahuisha kwa wakati.

Katika kikao hicho waliweka mpango mkakati wa kukutana kila robo ya mwaka ili kutathmini utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kuweka maazimo, lakini pia katika vikao hivyo vinne kimojawapo kitahusisha watumishi wote na wale wasio Mahakimu maana ni sehemu ya uwezeshaji wa kufanisi utendaji kazi wa Mahakimu. 

Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika Kinyerezi na baada ya mafunzo na kikao waliweza kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.


 Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Lumuli Mbuya (kushoto) akitoa mafunzo ya Namna ya Kupokea Ushahidi wa kielekroniki kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya Ilala na Mahakama za Mwanzo za Wilaya hiyo tarehe 19 Juni, 2026. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Herrieth Mwailolo.

 Washiriki wa Mafumo ya Namna Bora ya Kupokea Ushahidi wa Kieletroniki wakiwa katika picha ya pamoja na Mwezeshaji wa mafunzo hayo Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Lumuli Mbuya (aliyekaa katikati). Kushoto ni Mhe. Herrieth Mwailolo na kulia Mhe. Mohamed Burhan.

Baadhi ya Washiriki ambao ni Mahakimu wakishiriki mafunzo ya namna ya kupokea Ushahidi wa Kieletroniki.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Mhe. Herrieth Mwailolo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Namna Bora ya Kupokea Ushahidi wa Kieletroniki.

Ofisa Upelelezi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakili Emmanuel Cheneko akifundisha Sheria za Kodi kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya Ilala na Mahakama za Mwanzo za Wilaya hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni