Jumanne, 11 Agosti 2026

MAJAJI, MAHAKIMU MBEYA WANOLEWA JINSI YA KUKABILIANA NA MSONGO WA MAWAZO

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Majaji, Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama Masjala Ndogo ya Mbeya wametakiwa kutambua, kudhibiti na kukabiliana na msongo wa mawazo kwa wakati, wakizingatia kuwa afya njema ya akili ni msingi muhimu wa kufanya maamuzi yenye umakini, weledi na ya haki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Wito huo umetolewa katika mafunzo maalumu yaliyowakutanisha Majaji na Mahakimu wa Masjala Ndogo ya Mbeya, yaliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Lake Nyasa, iliyopo katika fukwe za Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela, ambapo washiriki walipata elimu kuhusu chanzo, madhara na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha na mazingira ya kazi.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Kilutheri ya Matema, Wilaya ya Kyela, Dkt. Ebenezer Richard Minja, ambaye aliwaeleza washiriki kuwa msongo wa mawazo ni hali inayoweza kumpata mtu kutokana na changamoto mbalimbali za maisha na mabadiliko ya mazingira au mtindo wa maisha na kwamba hali hiyo inapopuuzwa inaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya mtu.

Dkt. Minja alisisitiza umuhimu wa mtu kutambua mambo yanayoweza kumletea msongo wa mawazo na kuchukua hatua stahiki mapema, akiwataka washiriki kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara na kuepuka tabia ya kujilinganisha na watu wengine.

Aidha, alieleza kuwa kufanya ibada ni miongoni mwa njia zinazoweza kumsaidia mtu kupata utulivu wa akili, kwa kuwa humwezesha mtu kujenga imani na kumweleza Mungu changamoto anazokabiliana nazo.

Kwa mujibu wa Dkt. Minja, msongo wa mawazo unapokomaa unaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa afya ya mtu na kusababisha matatizo mbalimbali, yakiwemo shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo, kupoteza kumbukumbu, kupungua uzito na kushuka kwa kinga ya mwili, hali inayoweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa mengine kama kisukari.

“Ukihisi mambo yanaenda mrama, tafuta msaada mapema. Njiti moja ya kiberiti inaweza kuangamiza msitu mzima, hivyo chukua hatua mapema kupambana na msongo wa mawazo kabla matatizo makubwa hayajajitokeza,” alisema Dkt. Minja, huku akisisitiza umuhimu wa kutafuta msaada mapema pale mtu anapohisi kuzongwa na msongo wa Mawazo.

Akizungumzia suala hilo kwa mtazamo wa mazingira ya kazi za Mahakama, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya alisema kuwa, majukumu ya kimahakama yanaweza kuwa miongoni mwa vyanzo vya msongo wa mawazo kutokana na mlundikano wa mashauri, uzito wa maamuzi yanayofanywa pamoja na mazingira mbalimbali yanayowazunguka watendaji hao.

Bw. Chonya aliongeza kuwa, changamoto hizo zinahitaji usimamizi mzuri wa muda, kutenganisha majukumu ya kikazi na maisha ya nyumbani pamoja na kutafuta ushauri wa kitaalamu pale mtu anapohisi amelemewa.

“Akili iliyochoka inashindwa kuchuja ukweli na uwongo kwa wakati, hivyo tujitahidi kudhibiti msongo wa mawazo. Kwani afya ya watendaji wa Mahakama ina uhusiano wa moja kwa moja na uwezo wao wa kutekeleza wajibu wa kutoa haki kwa jamii,” alisema Bw. Chonya.

“Ili uweze kutoa haki kwa jamii ni lazima ujitendee haki mwenyewe kwa kulinda afya ya mwili na akili. Jamii inatuhitaji tukiwa na afya njema na akili timamu,” alisema Mtendaji Chonya

Katika mafunzo hayo pia washiriki walijifunza umuhimu wa kuzuia changamoto kabla hazijawa kubwa kwa kujadili umuhimu wa mpango wa malezi kwa mahakimu “mentorship programe”

Akizungumzia suala hilo, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, alisema ‘Mentorship Programme’ ni muhimu katika kuwasaidia Mahakimu kukua kitaaluma, kuboresha utendaji wao na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika safari yao ya kiutumishi.

Mhe. Mtulya alisema kuwa, malezi ya kitaaluma yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kumsaidia Hakimu kupata ushauri mapema kabla changamoto anazokabiliana nazo hazijawa kubwa na kuathiri utendaji wake au kufikia hatua ya kushughulikiwa na Kamati za Maadili.

“Mahakimu wengi wanaharibikiwa kwa kutopata mlezi wa kumsaidia kabla changamoto haijawa kubwa hadi kufikia kwenye Kamati ya Maadili,” alisema Mhe. Mtulya.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Teddy Mlimba, alisisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi, walezi na wasimamizi wanaoweza kuwasaidia watendaji kukabiliana na changamoto za kazi na maisha kwa wakati.

“Kazi zetu ni ngumu sana na ukipata mtu wa kumtolea mambo au changamoto zako ni jambo kubwa sana, hivyo ni muhimu kupata kiongozi, mlezi na msimamizi wa kukusimamia,” alisisitiza Mhe. Mlimba

Mafunzo hayo yameweka wazi kuwa mjadala kuhusu afya ya akili kwa Majaji na Mahakimu haupaswi kuangaliwa kama suala binafsi pekee, bali kama sehemu ya kujenga mazingira bora ya utoaji wa haki.

Majukumu ya kimahakama yanahitaji umakini mkubwa, uwezo wa kuchambua hoja kwa kina na kufanya maamuzi kwa usawa na bila kuyumbishwa. Kwa msingi huo, kulinda afya ya akili na mwili, kusimamia muda, kutafuta msaada pale inapohitajika na kuwa na mfumo imara wa malezi na ushauri wa kitaaluma ni miongoni mwa hatua zinazoweza kuimarisha ustawi wa watendaji na ufanisi wa kazi za Mahakama.

Hatua hiyo pia inalinda dhamira ya kujenga Mahakama yenye watendaji wenye weledi, maadili na utayari wa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu. Afya ya akili ya watendaji wa Mahakama ni uwekezaji katika haki na kulinda akili iliyo imara ni sehemu ya kulinda haki ya mwananchi.

Mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Kilutheri ya Matema, Wilaya ya Kyela Dkt. Ebenezer Richard Minja (aliyesimama) akitoa mafunzo ya kukabiliana na Msongo wa Mawazo kwa Waheshimiwa Majaji na Mahakimu (hawapo pichani).

Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Mahakimu ambao walioshiriki katika mafunzo hayo ambao ni wananchama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Ndogo ya Mbeya wakifanya zoezi kwa vitendo.

Sehemu ya washiriki katika mafunzo hayo ambao ni Mahakamu wananchama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Tawi la Masjala Ndogo ya Mbeya wakifuatilia mafunzo hayo kwa makini.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kyela Mhe. Roster Mofuga akichangia jambo katika mafunzo hayo, (katikati) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba na (kushoto) ni Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer.

Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (aliyesimama) akizungumza jambo katika mafunzo hayo, kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo.

Viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa katika mafunzo hayo (wa kwanza kushoto) ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, (katikati) ni Jaji wa Mahakama kuu masijala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angaza Mwipopo na Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo (wa kwanza kulia)

(Habari Hii Imehaririwa na INNOCENT KANSHA - Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni